Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: Philemon

1:1 Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu

1:2 na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkupo.

1:3 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana yesu Kristo.

1:4 Kila wakati ninaposali nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu

1:5 maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana wetu Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu.

1:6 Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo.

1:7 Ndugu, upendo wako yameniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.

1:8 Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya.

1:9 Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake.

1:10 Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni.

1:11 Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia.

1:12 Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe.

1:13 Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Habari Njema.

1:14 Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika.

1:15 Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima.

1:16 Na sasa yeye si mtumwa tu, ila ni bora zaidi ya mtumwa: yeye ni ndugu yetu mpenzi. Na wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana.

1:17 Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe.

1:18 Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi.

1:19 Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako.)

1:20 Haya, basi, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo.

1:21 Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba.

1:22 Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni.

1:23 Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu.

1:24 Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu.

1:25 Nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.


Next: Hebrews