Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous 

Swahili Bible: Revelation

1:1 Hizi ni habari za mambo ambayo yalifunuliwa na Yesu Kristo. Mungu alimpa Kristo ufunuo huu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe Yohane, mtumishi wake, mambo hayo,

1:2 naye Yohane, ameyasema yote aliyoyaona. Na hii ndio taarifa yake kuhusu ujumbe wa Mungu na ukweli uliofunuliwa na Yesu Kristo.

1:3 Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki; heri yao wale wanaosikiliza maneno ya ujumbe huu wa kinabii na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati umekaribia ambapo mambo haya yatatukia.

1:4 Mimi Yohane nayaandikia makanisa yaliyoko mkoani Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi,

1:5 na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia. Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu,

1:6 akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina.

1:7 Tazama! Anakuja katika mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma. Makabila yote duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina.

1:8 "Mimi ni Alfa na Omega," asema Bwana Mungu Mwenye Uwezo, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.

1:9 Mimi ni Yohane, ndugu yenu; na kwa kuungana na Kristo nashiriki pamoja nanyi katika kustahimili mateso yanayowapata wale walio wa Utawala wake. Mimi nilikuwa kisiwani Patmo kwa sababu ya kuhubiri ujumbe wa Mungu na ukweli wa Yesu.

1:10 Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta.

1:11 Nayo ilisema, "Andika katika kitabu yote unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamoni, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea."

1:12 Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu,

1:13 na katikati yake kulikuwa na kitu kama mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na ukanda wa dhahabu kifuani.

1:14 Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba safi, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto;

1:15 miguu yake iling'aa kama shaba iliyosafishwa katika tanuru ya moto na kusuguliwa, na sauti yake ilikuwa, kama sauti ya poromoko la maji.

1:16 Katika mkono wake wa kulia, alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling'aa kama jua kali.

1:17 Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, "Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho.

1:18 Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni mzima milele na milele. Ninazo funguo za kifo na Kuzimu.

1:19 Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye.

1:20 Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia, na siri ya vile vinara saba vya taa hii: zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa ni makanisa saba.

2:1 "Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye ashikaye nyota saba katika mkono wake wa kulia, na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu.

2:2 Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo.

2:3 Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo.

2:4 Lakini ninayo hoja moja juu yako: wewe hunipendi tena sasa kama pale awali.

2:5 Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukayaache madhambi yako, na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja kwako na kukiondoa kinara chako mahali pake.

2:6 Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: wewe unayachukia wanayoyatenda Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi.

2:7 "Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda nitawapa haki ya kula matunda ya mti wa uzima ulioko ndani ya bustani ya Mungu.

2:8 "Kwa malaika wa kanisa la Smurna andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye wa kwanza na wa mwisho, ambaye alikufa na akaishi tena.

2:9 Najua taabu zako; najua pia umaskini wako, ingawaje kwa kweli wewe ni tajiri; najua kashfa walizokufanyia wale wanaojiita Wayahudi lakini si Wayahudi wa kweli, bali ni kundi lake Shetani.

2:10 Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka. Sikiliza! Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa, nami nitawapeni taji ya uzima.

2:11 "Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda hawataumizwa na kifo cha pili.

2:12 "Kwa malaika wa kanisa la Pergamoni andika hivi: "Huu ndio ujumbe wake yeye aliye na upanga mkali wenye kuwili.

2:13 Najua unakoishi: Wewe unaishi kwenye makao makuu ya Shetani! Lakini bado unashikilia jina langu; hukuikana imani yako kwangu hata siku zile Antipa shahidi wangu mwaminifu, alipouawa pale mahali anapoishi Shetani.

2:14 Lakini ninayo machache dhidi yako: baadhi yenu ni wafuasi wa Balaamu aliyemfundisha Balaki kuwatega wana wa Israeli wale vyakula vilivyotambikiwa sanamu za kufanya uzinzi.

2:15 Vivyo hivyo, wako pia miongoni mwenu watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai.

2:16 Basi, achana na madhambi yako. La sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga utokao kinywani mwangu.

2:17 "Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda nitawapa ile mana iliyofichika. Nitawapa pia jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya ambalo hakuna mtu aliyelijua isipokuwa tu wale wanaolipokea.

2:18 "Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi: "Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama moto, na miguu yake inang'aa kama shaba iliyosuguliwa.

2:19 Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale awali.

2:20 Lakini nina hoja moja juu yako: wewe unamvumilia yule mwanamke Yezabeli anayejiita nabii wa Mungu. Yeye huwafundisha na kuwapotosha watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu.

2:21 Nimempa muda wa kutubu dhambi zake, lakini hataki kuachana na uzinzi wake.

2:22 Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali. Naam, nitafanya hivyo, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye.

2:23 Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu.

2:24 "Lakini ninyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati mafundisho yake Yezabeli, na ambao hamkujifunza kile wanachokiita Siri ya Shetani, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine.

2:25 Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja.

2:26 "Wanaoshinda, na wale watakaozingatia mpaka mwisho kutenda ninayotaka, nitawapa mamlaka juu ya mataifa.

2:27 Naam, nitawapa uwezo uleule nilioupokea kwa Baba: yaani, watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma na kuyavunjavunja kama chombo cha udongo.

2:28 Tena nitawapa nyota ya asubuhi.

2:29 "Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

3:1 "Kwa malaika wa kanisa la Sarde andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye na roho saba za Mungu na nyota saba. Nayajua mambo yako yote; najua unajulikana kuwa na uhai kumbe umekufa!

3:2 Amka! Imarisha chochote chema kilichokubakia kabla nacho hakijatoweka kabisa. Maana, mpaka sasa, sijayaona matendo yako kuwa ni makamilifu mbele ya Mungu wangu.

3:3 Kumbuka, basi, yale uliyofundishwa na jinsi ulivyoyasikia, uyatii na ubadili nia yako mbaya. Usipokesha nitakujia ghafla kama mwizi, na wala hutaijua saa nitakapokujia.

3:4 Lakini wako wachache huko Sarde ambao hawakuyachafua mavazi yao. Hao wanastahili kutembea pamoja nami wakiwa wamevaa mavazi meupe.

3:5 "Wale wanaoshinda, watavikwa mavazi meupe kama hao. Nami sitayafuta majina yao kutoka katika kitabu cha uzima; tena nitawakiri kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake.

3:6 "Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

3:7 "Kwa malaika wa kanisa la Filadelfia andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, ambaye anao ule ufunguo wa Daudi, na ambaye hufungua na hakuna mtu awezaye kufungua.

3:8 Nayajua mambo yako yote! Sasa, nimefungua mbele yako mlango ambao hakuna mtu awezaye kuufunga; najua kwamba ingawa huna nguvu sana, hata hivyo, umezishika amri zangu, umelitii neno langu wala hukulikana jina langu.

3:9 Sikiliza! Nitawapeleka kwako watu wa kundi lake Shetani, watu ambao hujisema kuwa ni Wayahudi, kumbe ni wadanganyifu. Naam, nitawapeleka kwako na kuwafanya wapige magoti mbele yako wapate kujua kwamba kweli nakupenda wewe.

3:10 Kwa kuwa wewe umezingatia agizo langu la kuwa na uvumilivu, nami pia nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima kuwajaribu wote wanaoishi duniani.

3:11 Naja kwako upesi! Linda, basi, ulicho nacho sasa, ili usije ukanyang'anywa na mtu yeyote taji yako ya ushindi.

3:12 "Wale wanaoshinda nitawafanya wawe minara katika Hekalu la Mungu wangu, na hawatatoka humo kamwe. Pia nitaandika juu yao jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani Yerusalemu mpya, mji ambao utashuka kutoka juu mbinguni kwa Mungu wangu. Tena nitaandika juu yao jina langu jipya.

3:13 "Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

3:14 "Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aitwaye Amina. Yeye ni shahidi mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu.

3:15 Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: baridi au moto.

3:16 Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika!

3:17 Wewe unajisema, Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya kitu chochote. Kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi!

3:18 Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona.

3:19 Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa hiyo kaza moyo, achana na dhambi zako.

3:20 Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami.

3:21 "Wale wanaoshinda nitawaketisha pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi.

3:22 "Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!"

4:1 Baada ya hayo nilitazama nikaona mlango umefunguliwa mbinguni. Na ile sauti niliyoisikia pale awali ambayo ilikuwa kama sauti ya tarumbeta, ikasema, "Njoo hapa juu nami nitakuonyesha mambo yatakayotukia baadaye."

4:2 Mara nikachukuliwa na Roho. Kumbe, huko mbinguni kuna kiti cha enzi na juu yake ameketi mmoja.

4:3 Huyo aliyeketi juu yake alikuwa kama almasi na jiwe zuri jekundu. Upinde wa mvua ulikuwa unang'aa kama zumaridi na ulikizunguka kiti cha enzi pande zote.

4:4 Kulikuwa na duara la viti ishirini na vinne kukizunguka kiti cha enzi, na juu ya viti hivyo wazee ishirini na wanne walikuwa wameketi wamevaa mavazi meupe na taji za dhahabu vichwani.

4:5 Umeme, sauti na ngurumo, vilikuwa vinatoka kwenye hicho kiti cha enzi. Taa saba za moto zilikuwa zinawaka mbele ya hicho kiti cha enzi. Taa hizo ni roho saba za Mungu.

4:6 Mbele ya kiti cha enzi kulikuwa na kitu kama bahari ya kioo, angavu kama jiwe linga'aalo sana. Katika pande zote za hicho kiti cha enzi na kukizunguka, kilikuwa na viumbe hai vinne. Viumbe hivyo vilikuwa vimejaa macho mbele na nyuma.

4:7 Kiumbe cha kwanza kulikuwa kama simba, cha pili kama ng'ombe, cha tatu kilikuwa na sura kama mtu, na cha nne kilikuwa kama tai anayeruka.

4:8 Viumbe hivyo vinne vilikuwa na mabawa sita kila kimoja, na vilikuwa vimejaa macho, ndani na nje. Usiku na mchana, bila kupumzika huimba: "Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana, Mungu Mwenye Uwezo, aliyekuwako, aliyeko na anayekuja!"

4:9 Kila mara viumbe vinne vilipoimba nyimbo za kumtukuza, kumheshimu na kumshukuru huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, ambaye anaishi milele na milele,

4:10 wale wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele; na huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema:

4:11 "Wewe ni Bwana na Mungu wetu, unastahili utukufu na heshima na nguvu; maana wewe uliumba vitu vyote, na kwa matakwa yako kila kitu kimepewa uhai na uzima."

5:1 Kisha katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, nikaona kitabu; nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa na mihuri saba.

5:2 Tena nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa: "Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?"

5:3 Lakini hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini Kuzimu, aliyeweza kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani.

5:4 Basi, mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili kukifungua, au kukitazama ndani.

5:5 Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, "Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, mjukuu maarufu wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu."

5:6 Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwana kondoo amesimama, akizungukwa kila upande na vile viumbe hai vinne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani.

5:7 Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi.

5:8 Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, vile viumbe hai vinne pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja, alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu.

5:9 Basi, wakaimba wimbo huu mpya: "Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu na kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechinjwa, na kwa damu yako umemnunulia Mungu watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

5:10 Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani wamtumikie Mungu wetu nao watatawala duniani."

5:11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi isiyohesabika, maelfu na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha enzi, vile viumbe hai vinne na wale wazee;

5:12 wakasema kwa sauti kuu: "Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa."

5:13 Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini kuzimuni na baharini--viumbe vyote ulimwenguni--vikisema: "Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi milele na milele."

5:14 Na vile viumbe vinne hai vikasema, "Amina!" Na wale wazee wakaanguka kifudifudi, wakaabudu.

6:1 Kisha nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia kimoja cha vile viumbe hai vinne kikisema kwa sauti kama ya ngurumo, "Njoo!"

6:2 Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpanda farasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi aendelee kushinda.

6:3 Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, "Njoo!"

6:4 Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpanda farasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, akapewa upanga mkubwa.

6:5 Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, "Njoo!" Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpanda farasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake.

6:6 Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa vile viumbe hai vinne. Nayo ilisema, "Kibaba kimoja cha unga wa ngano wa kiasi cha fedha dinari moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa dinari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!"

6:7 Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema, "Njoo!"

6:8 Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la mpanda farasi wake lilikuwa kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.

6:9 Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya madhabahu ya kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe wa Mungu, na kwa sababu ya ushuhuda waliotoa.

6:10 Basi, wakalia kwa sauti kubwa: "Ee Bwana, uliye mtakatifu na mwaminifu, mpaka lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia kwa ajili ya kuuawa kwetu?"

6:11 Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri kwa muda mfupi, mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu ambao watawaua kama wao wenyewe walivyouawa.

6:12 Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia; mwezi wote ukawa mwekundu kama damu;

6:13 nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali.

6:14 Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake.

6:15 Kisha wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye majabali milimani.

6:16 Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, "Tuangukieni, mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo!

6:17 Maana siku maalum ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?"

7:1 Baada ya hayo nikawaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za dunia wakishika pepo nne za dunia ili upepo usivume hata kidogo: wala katika nchi, wala baharini, wala kwenye miti.

7:2 Kisha nikamwona malaika mwingine akipanda juu kutoka mashariki akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai. Akapaaza sauti na kuwaambia hao malaika wanne waliokabidhiwa jukumu la kuiharibu nchi na bahari,

7:3 "Msiharibu nchi, wala bahari, wala miti, mpaka tutakapokwisha wapiga mhuri watumishi wa Mungu wetu katika paji la uso."

7:4 Kisha nikasikia idadi ya hao waliopigwa mhuri: Watu mia moja arobaini na nne elfu wa makabila yote ya watu wa Israeli.

7:5 Kabila la Yuda walikuwa watu kumi na mbili elfu; kabila la Reubeni, kumi na mbili elfu, kabila la Gadi, kumi na mbili elfu;

7:6 Kabila la Asheri, kumi na mbili elfu; kabila la Naftali, kumi na mbili elfu; kabila la Manase, kumi na mbili elfu;

7:7 kabila la Simeoni, kumi na mbili elfu, kabila la Lawi, kumi na mbili elfu, kabila la Isakari, kumi na mbili elfu;

7:8 kabila la Zabuloni, kumi na mbili elfu; kabila la Yosefu, kumi na mbili elfu, na kabila la Benyamini, kumi na mbili elfu.

7:9 Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wakiwa wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao.

7:10 Wakapaaza sauti: "Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!"

7:11 Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na vile viumbe hai vinne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu,

7:12 wakisema, "Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!"

7:13 Mmoja wa hao wazee akaniuliza, "Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?"

7:14 Nami nikamjibu, "Mheshimiwa, wewe wajua!" Naye akaniambia, "Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa.

7:15 Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika Hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda.

7:16 Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena,

7:17 kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao."

8:1 Na Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa saba, kukawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.

8:2 Kisha nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu wamepewa tarumbeta saba.

8:3 Malaika mwingine akafika, akiwa anachukua chetezo cha dhahabu, akasimama mbele ya madhabahu ya kufukizia ubani. Naye akapewa ubani mwingi autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu, juu ya madhabahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi.

8:4 Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu, kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu.

8:5 Kisha malaika akakichukua hicho chetezo, akakijaza moto wa madhabahuni akakitupa duniani. Kukawa na ngurumo, sauti, umeme na tetemeko la ardhi.

8:6 Kisha wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka tayari kupiga mbiu ya mgambo.

8:7 Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa mvua ya mawe na moto, pamoja na damu, ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua, na majani yote mabichi yakaungua.

8:8 Malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto ukatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa damu,

8:9 theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa na theluthi moja ya meli zikaharibiwa.

8:10 Kisha malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota kubwa ikiwaka kama bonge la moto, ikaanguka kutoka mbinguni, na kutua juu ya theluthi moja ya mito na chemchemi za maji.

8:11 (Nyota hiyo inaitwa "Uchungu.") Basi, theluthi moja ya maji yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa sababu yaligeuka kuwa machungu.

8:12 Kisha malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo theluthi moja ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza ukapoteza theluthi moja ya mng'ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga, hali kadhalika na theluthi moja ya usiku.

8:13 Kisha nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa angani anasema kwa sauti kubwa, "Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani wakati malaika watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!"

9:1 Kisha malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la Kuzimu.

9:2 Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la Kuzimu, kukatoka moshi wa tanuru kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa Kuzimu.

9:3 Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani wakapewa nguvu kama ya ng'e.

9:4 Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso.

9:5 Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na ng'e.

9:6 Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia.

9:7 Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.

9:8 Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba.

9:9 Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani.

9:10 Walikuwa na mikia na miiba kama ng'e, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano.

9:11 Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani mwangamizi.

9:12 Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.

9:13 Kisha malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu.

9:14 Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, "Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Eufrate!"

9:15 Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo, wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanaadamu.

9:16 Nilisikia idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa milioni mia mbili.

9:17 Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na njano kama kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na kiberiti vilikuwa vinatoka kinywani mwao.

9:18 Theluthi moja ya wanaadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu yaani, moto, moshi na kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao;

9:19 maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilikuwa na vichwa kama nyoka, na waliitumia hiyo kuwadhuru watu.

9:20 Wanaadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakugeuka na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; bali wakaendelea kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea.

9:21 Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi.

10:1 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu, na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama moto.

10:2 Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari, na wa kushoto juu ya nchi kavu,

10:3 na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo.

10:4 Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: "Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!"

10:5 Kisha yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni,

10:6 akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, "Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha!

10:7 Lakini wakati ule malaika wa saba atakapotoa sauti yake, wakati atakapopiga tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii."

10:8 Kisha ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni pale awali ikasema nami tena: "Nenda ukakichukue kile kitabu kilichofunguliwa, kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya nchi kavu."

10:9 Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho kitabu kidogo. Naye akaniambia, "Kichukue, ukile; kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!"

10:10 Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi mwa huyo malaika, nikakila; nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali, lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu.

10:11 Kisha nikaambiwa, "Inakubidi tena kutangaza ujumbe wa Mungu kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!"

11:1 Kisha nikapewa mwanzi uliokuwa kama kijiti cha kupimia, nikaambiwa, "Inuka, ukalipime Hekalu la Mungu, madhabahu ya kufukizia ubani, na ukawahesabu watu wanaoabudu ndani ya Hekalu.

11:2 Lakini uache ukumbi ulio nje ya Hekalu; usiupime, maana huo umekabidhiwa watu wa mataifa mengine, ambao wataukanyanga mji Mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili.

11:3 Nami nitawatuma mashahidi wangu wawili ili watangaze ujumbe wa Mungu kwa muda huo wa siku elfu moja mia mbili na sitini wakiwa wamevaa mavazi ya magunia."

11:4 Hao mashahidi wawili ni miti miwili ya Mizeituni na taa mbili zinazosimama mbele ya Bwana wa dunia.

11:5 Kama mtu akijaribu kuwadhuru, moto hutoka kinywani mwao na kuwaangamiza adui zao; na kila mtu atakayejaribu kuwadhuru atakufa namna hiyo.

11:6 Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati wanapotangaza ujumbe wa Mungu. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza chemchemi zote za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna duniani kila mara wapendavyo.

11:7 Lakini wakisha maliza kutangaza ujumbe huo, mnyama atokaye shimoni kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua.

11:8 Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo Bwana wao alisulubiwa; jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri.

11:9 Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe.

11:10 Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili. Watafanya sherehe na kupelekeana zawadi maana manabii hawa wawili walikuwa wamewasumbua mno watu wa dunia.

11:11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu.

11:12 Kisha hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikiwaambia, "Njoni hapa juu!" Nao wakapanda juu mbinguni katika wingu, maadui wao wakiwa wanawatazama.

11:13 Wakati huohuo, kukatokea tetemeko kubwa la ardhi, sehemu moja ya kumi ya ardhi ikaharibiwa. Watu elfu saba wakauawa kwa tetemeko hilo la ardhi. Watu waliosalia wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.

11:14 Maafa ya pili yamepita; lakini tazama! Maafa ya tatu yanafuata hima.

11:15 Kisha malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu zikasikika mbinguni zikisema, "Sasa utawala juu ya ulimwengu ni wa Bwana wetu na Kristo wake. Naye atatawala milele na milele!"

11:16 Kisha wale wazee ishirini na wanne walioketi mbele ya Mungu katika viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu,

11:17 wakisema: "Bwana Mungu Mwenye uwezo, uliyeko na uliyekuwako! Tunakushukuru, maana umetumia nguvu yako kuu ukaanza kutawala!

11:18 Watu wa mataifa waliwaka hasira, maana wakati wa ghadhabu yako umefika, wakati wa kuwahukumu wafu. Ndio wakati wa kuwatuza watumishi wako manabii, watu wako na wote wanaolitukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo. Ni wakati wa kuwaangamiza wale wanaoangamiza dunia."

11:19 Hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la Agano lake likaonekana Hekaluni mwake. Kisha kukatokea umeme, sauti, ngurumo, tetemeko la ardhi, na mvua kubwa ya mawe.

12:1 Kisha ishara kubwa ikaonekana mbinguni. Palikuwa hapo mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake!

12:2 Alikuwa mja mzito, na akapaaza sauti kwa maumivu na uchungu wa kujifungua mtoto.

12:3 Ishara nyingine ikatokea mbinguni: joka kubwa jekundu na lenye pembe kumi na vichwa saba; na kila kichwa kilikuwa na taji.

12:4 Joka hilo liliburuta kwa mkia wake theluthi moja ya nyota za anga na kuzitupa duniani. Nalo lilisimama mbele ya huyo mama aliyekuwa karibu kujifungua mtoto, tayari kabisa kummeza mtoto, mara tu atakapozaliwa.

12:5 Kisha mama huyo akajifungua mtoto wa kiume, ambaye atayatawala mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Lakini mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu na kwenye kiti chake cha enzi.

12:6 Huyo mama akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali pa usalama ambapo angehifadhiwa kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini.

12:7 Kisha kukazuka vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake walipigana na hilo joka, nalo likawashambulia pamoja na malaika wake.

12:8 Lakini joka hilo halikuweza kuwashinda, na hatimaye hapakuwa tena na nafasi mbinguni kwa ajili yake na malaika wake.

12:9 Basi, joka hilo kuu likatupwa nje. Joka hilo ndiye yule nyoka wa kale ambaye huitwa pia Ibilisi au Shetani. Ndiye anayeudanganya ulimwengu wote. Naam, alitupwa duniani, na malaika wake wote pamoja naye.

12:10 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: "Sasa ukombozi utokao kwa Mungu umefika! Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika. Na Kristo wake ameonyesha mamlaka yake! Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu, aliyesimama mbele ya Mungu akiwashtaki usiku na mchana, sasa ametupwa nje.

12:11 Ndugu zetu wameshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana, wakawa tayari kufa.

12:12 Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba siku zake zilizobakia ni chache."

12:13 Joka lilipotambua kwamba limetupwa chini duniani, likaanza kumwinda yule mama aliyekuwa amejifungua mtoto wa kiume.

12:14 Lakini mama huyo akapewa mabawa mawili ya tai apate kuruka mbali sana na hilo joka, mpaka mahali, pake jangwani ambapo angehifadhiwa salama kwa muda wa miaka mitatu na nusu.

12:15 Basi, joka likatapika maji mengi kama mto, yakamfuata huyo mama nyuma ili yamchukue.

12:16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mama: ikajifunua kama mdomo na kuyameza maji hayo yaliyotoka kinywani mwa hilo joka.

12:17 Basi, joka hilo likamkasirikia huyo mama, likajiondokea, likaenda kupigana na wazawa wengine wa huyo mama, yaani wote wanaotii amri za Mungu na kuuzingatia ukweli wa Yesu.

13:1 (G12-18) Na likajisimamia ukingoni mwa bahari. (G13-1) Kisha nikaona mnyama mmoja akitoka baharini. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na kila pembe ilikuwa na taji. Jina la kashfa lilikuwa limeandikwa juu ya vichwa hivyo.

13:2 Mnyama huyo niliyemwona alikuwa kama chui; miguu yake ilikuwa kama ya dubu, na kinywa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu yake, kiti chake cha enzi na uwezo mkuu.

13:3 Kichwa kimojawapo cha huyo mnyama kilionekana kama kilikwisha jeruhiwa vibaya sana, lakini jeraha hilo lilikuwa limepona. Dunia nzima ilishangazwa na huyo mnyama na kumfuata.

13:4 Watu wote wakaliabudu lile joka kwa sababu lilimpa huyo mnyama uwezo wake. Wakamwabudu pia huyo mnyama wakisema, "Nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana naye?"

13:5 Kisha huyo mnyama akaruhusiwa kusema maneno ya kujigamba na kumkufuru Mungu; akaruhusiwa kuwa na mamlaka kwa muda wa miezi arobaini na miwili.

13:6 Basi, akaanza kumtukana Mungu, kulitukana jina lake, makao yake, na wote wakaao mbinguni.

13:7 Aliruhusiwa kuwapiga vita na kuwashinda watu wa Mungu. Alipewa mamlaka juu ya watu wa kila kabila, ukoo, lugha na taifa.

13:8 Wote waishio duniani watamwabudu isipokuwa tu wale ambao majina yao yameandikwa tangu mwanzo wa ulimwengu katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo aliyechinjwa.

13:9 "Aliye na masikio, na asikie!

13:10 Waliokusudiwa kuchukuliwa mateka lazima watatekwa; waliokusudiwa kuuawa kwa upanga lazima watauawa kwa upanga. Kutokana na hayo ni lazima watu wa Mungu wawe na uvumilivu na imani."

13:11 Kisha nikamwona mnyama mwingine anatoka ardhini. Alikuwa na pembe mbili kama pembe za kondoo, na aliongea kama joka.

13:12 Alikuwa na mamlaka kamili kutoka kwa yule mnyama wa kwanza, na akautumia uwezo huo mbele ya huyo mnyama. Akailazimisha dunia yote na wote waliomo humo kumwabudu huyo mnyama wa kwanza ambaye alikuwa na jeraha la kifo lililokuwa limepona.

13:13 Basi, huyu mnyama wa pili akafanya miujiza mikubwa hata akasababisha moto kutoka mbinguni ushuke duniani mbele ya watu.

13:14 Aliwapotosha wakazi wa dunia kwa miujiza hiyo aliyojaliwa kutenda mbele ya mnyama wa kwanza. Aliwaambia wakazi wa dunia watengeneze sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi tena.

13:15 Kisha alijaliwa kuipulizia uhai hiyo sanamu ya yule mnyama wa kwanza, hata ikaweza kuongea na kuwaua watu wote ambao hawakuiabudu.

13:16 Aliwalazimisha wote, wadogo na wakubwa, matajiri na maskini, watu huru na watumwa, watiwe alama juu ya mikono yao ya kulia au juu ya paji za nyuso zao.

13:17 Akapiga marufuku mtu yeyote kununua au kuuza kitu isipokuwa tu mtu aliyetiwa alama hiyo, yaani jina la yule mnyama au tarakimu ya jina hilo.

13:18 Hapa ni lazima kutumia ujasiri! Mwenye akili anaweza kufafanua maana ya tarakimu ya mnyama huyo, maana ni tarakimu yenye maana ya mtu fulani. Tarakimu hiyo ni mia sita sitini na sita.

14:1 Kisha nikaona mlima Sioni, na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu mia moja arobaini na nne elfu ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake.

14:2 Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama sauti ya maji mengi na kama sauti ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao.

14:3 Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu mia moja arobaini na nne elfu waliokombolewa duniani.

14:4 Watu hao ndio wale waliojiweka safi kwa kutoonana kimwili na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo.

14:5 Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote.

14:6 Kisha nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu wote waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote, watu wa lugha zote na rangi zote.

14:7 Akasema kwa sauti kubwa, "Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na nchi, bahari na chemchemi za maji."

14:8 Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, "Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote wainywe divai yake--divai kali ya uzinzi wake!"

14:9 Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, "Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake,

14:10 yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu, ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo.

14:11 Moshi wa moto unaowatesa kupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake, na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana."

14:12 Kutokana na hayo, ni lazima watu wa Mungu, yaani watu wanaotii amri ya Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu.

14:13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, "Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana." Naye Roho asema, "Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata."

14:14 Kisha nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo kulikuwa na kiumbe kama mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkononi mwake.

14:15 Kisha malaika mwingine akatoka Hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, "Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva."

14:16 Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa.

14:17 Kisha malaika mwingine akatoka katika Hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali.

14:18 Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, "Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!"

14:19 Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu.

14:20 Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko mrefu kiasi cha mita mia tatu na kina chake kiasi cha mita mia mbili.

15:1 Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa makubwa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo makubwa saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa.

15:2 Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu.

15:3 Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo: "Bwana Mungu Mwenye Uwezo, matendo yako ni makuu mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli!

15:4 Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana matendo yako ya haki yameonekana na wote."

15:5 Baada ya hayo nikaona Hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ionyeshayo kuwapo kwa Mungu.

15:6 Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo Hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung'aa, na kanda za dhahabu vifuani mwao.

15:7 Kisha, mmojawapo wa vile viumbe vinne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele.

15:8 Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia Hekaluni mpaka mwisho wa mabaa makubwa saba ya wale malaika saba.

16:1 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, "Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani."

16:2 Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama, na wale walioiabudu sanamu yake.

16:3 Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa.

16:4 Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu.

16:5 Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema, "Ewe mtakatifu, Uliyeko na uliyekuwako! Wewe ni mwenye haki katika hukumu hii uliyotoa.

16:6 Maana waliimwaga damu ya watu wako na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; wamestahili hivyo!"

16:7 Kisha nikasikia sauti madhabahuni ikisema, "Naam, Bwana Mungu Mwenye Uwezo! Hukumu zako ni za kweli na haki!"

16:8 Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake.

16:9 Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo makubwa. Lakini hawakuziacha dhambi zao na kumtukuza Mungu.

16:10 Kisha malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu za maumivu,

16:11 wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakuyaacha matendo yao mabaya.

16:12 Kisha malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ilitengenezwa kwa ajili ya wafalme wa mashariki.

16:13 Kisha nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama, na kinywani mwa yule nabii wa uongo.

16:14 Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita kuu Siku ile ya Mungu Mwenye Uwezo.

16:15 "Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko mbele ya watu."

16:16 Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni.

16:17 Kisha malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, Hekaluni, ikisema, "Mwisho umefika!"

16:18 Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu.

16:19 Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha kikombe cha divai ya ghadhabu yake kuu.

16:20 Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena.

16:21 Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini kila moja, ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya mvua hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno.

17:1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, "Njoo, mimi nitakuonyesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi.

17:2 Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake."

17:3 Kisha, Roho akanikumba, akaniongoza mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.

17:4 Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonyesha uzinzi wake.

17:5 Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo "Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani."

17:6 Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumtangaza Yesu. Nilipomwona nilishangaa mno.

17:7 Lakini malaika akaniambia, "Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi.

17:8 Huyo mnyama uliyemwona alikuwa hai hapo awali, lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali, aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena!

17:9 "Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima saba, na huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme saba.

17:10 Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja anatawala bado, na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki kwa muda mfupi.

17:11 Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda zake kuharibiwa.

17:12 "Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja pamoja na yule mnyama.

17:13 Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na mamlaka yao yote.

17:14 Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale aliowaita na kuwachagua, ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme."

17:15 Malaika akaniambia pia, "Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule mzinzi, ni mataifa, watu wa kila rangi na lugha.

17:16 Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto.

17:17 Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake, yaani kwa kukubaliana wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya kutawala, mpaka hapo neno la Mungu litakapotimia.

17:18 "Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu unaowatawala wafalme wa dunia."

18:1 Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng'ao wake.

18:2 Basi, akapaaza sauti kwa nguvu akisema, "Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno.

18:3 Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo."

18:4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema, "Watu wangu, ondokeni kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi zake, msije mkaipata adhabu yake.

18:5 Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimelundikana mpaka mbinguni, na Mungu ameyakumbuka maovu yake.

18:6 Mtendeeni kama alivyowatendea ninyi; mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda. Jazeni kikombe chake kwa kinywaji kikali mara mbili zaidi ya kile alichowapeni.

18:7 Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, na kuishi kwake kwa anasa. Maana anajisemea moyoni: Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi si mjane, wala sitapatwa na uchungu!

18:8 Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: ugonjwa, huzuni na njaa. Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ni Mwenye Uwezo."

18:9 Wafalme wa Dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya anasa wataomboleza na kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo unaoteketea.

18:10 Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake, na kusema, "Ole! Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda wa saa moja tu adhabu yako imekupata."

18:11 Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana hakuna mtu anayenunua tena bidhaa zao;

18:12 hakuna tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na lulu, kitani na nguo za rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; vyombo vya kila aina ya miti ya pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma na marmari;

18:13 mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na ngano, ng'ombe na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na hata maisha ya watu.

18:14 Wafanyabiashara wanamwambia: "Faida yote uliyotazamia imetoweka, na utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!"

18:15 Wafanya biashara waliotajirika kutokana na mji huo, watasimama mbali kwa sababu ya hofu ya mateso yake, watalalamika na kuomboleza,

18:16 wakisema, "Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za kitani, za rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu!

18:17 Kwa saa moja tu utajiri wako umetoweka!" Halafu manahodha wote na wasafiri wao, wanamaji na wote wanaofanya kazi baharini, walisimama kwa mbali,

18:18 na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: "Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!"

18:19 Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza: "Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu umepoteza kila kitu!"

18:20 Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda ninyi!

18:21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu sana akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, "Ndivyo, Babuloni atakavyotupwa na kupotea kabisa.

18:22 Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako.

18:23 Mwanga wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi na bibi arusi hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako walikuwa wakuu duniani, na kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!"

18:24 Mji huo uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu ya watu wa Mungu na damu ya watu wote waliouawa duniani.

19:1 Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema, "Haleluya! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!

19:2 Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi mkuu ambaye alikuwa ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa sababu ya kumwaga damu ya watumishi wake!"

19:3 Wakasema, "Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo utapanda juu milele na milele!"

19:4 Na wale wazee ishirini na wanne, na vile viumbe hai vinne, wakajitupa chini, wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi wakisema, "Amina! Asifiwe Mungu!"

19:5 Kisha kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: "Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa."

19:6 Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, "Haleluya! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Uwezo ni Mfalme!

19:7 Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa arusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari.

19:8 Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung'aa!" (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watu wa Mungu.)

19:9 Kisha malaika akaniambia, "Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!" Tena akaniambia, "Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu."

19:10 Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, "Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunauzingatia ukweli ule alioufunua Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ukweli alioufunua Yesu ndio unaowaangazia manabii."

19:11 Kisha nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpanda farasi wake aliitwa "Mwaminifu" na "Kweli". Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki.

19:12 Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe.

19:13 Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni "Neno la Mungu."

19:14 Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na walikuwa wamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi.

19:15 Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Uwezo.

19:16 Juu ya vazi lake, na juu ya mguu wake, alikuwa ameandikwa jina: "Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana."

19:17 Kisha nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaaza sauti na kuwaambia ndege wote waliokuwa wanaruka juu angani, "Njoni! Kusanyikeni pamoja kwa karamu kuu ya Mungu.

19:18 Njoni mkaitafune miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye nguvu, ya farasi na wapanda farasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu wote: walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa."

19:19 Kisha nikaona yule mnyama pamoja na mfalme wa dunia na askari wao wamekusanyika pamoja kusudi wapigane na yule aliyekuwa ameketi juu ya farasi, pamoja na jeshi lake.

19:20 Lakini huyo mnyama akachukuliwa mateka, pamoja na nabii wa uongo aliyekuwa akifanya miujiza mbele yake. (Kwa miujiza hiyo, alikuwa amewapotosha wale waliokuwa na chapa ya huyo mnyama, na ambao walikuwa wameiabudu sanamu yake.) Huyo mnyama pamoja na huyo nabii walitupwa wote wawili, wakiwa wazimawazima, ndani ya ziwa linalowaka moto wa kiberiti.

19:21 Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule anayepanda farasi. Ndege wote wakajishibisha kwa nyama zao.

20:1 Kisha nikamwona malaika mmoja anashuka kutoka mbinguni akiwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake.

20:2 Akalikamata lile joka--nyoka wa kale, yaani Ibilisi au Shetani--akalifunga kwa muda wa miaka elfu moja.

20:3 Malaika akalitupa Kuzimu, akaufunga mlango wa kuingilia huko na kuutia mhuri ili lisiweze tena kuyapotosha mataifa mpaka hapo miaka elfu moja itakapotimia. Lakini baada ya miaka hiyo ni lazima lifunguliwe tena, lakini kwa muda mfupi tu.

20:4 Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa wamenyongwa kwa sababu ya kumtangaza Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa alama yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena uhai, wakatawala pamoja na Kristo kwa muda wa miaka elfu moja.

20:5 (Wale wengine waliokufa hawakupata uhai mpaka miaka elfu moja itimie.) Huu ndio ufufuo wa kwanza.

20:6 Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja.

20:7 Wakati miaka elfu mia moja itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake.

20:8 Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote yaliyotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga wa pwani.

20:9 Walitawanyika katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watu wa Mungu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawaangamiza.

20:10 Ibilisi, aliyekuwa anawapotosha, akatupwa ndani ya ziwa linalowaka moto wa kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo, nao watateswa mchana na usiku, milele na milele.

20:11 Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe, na yule aketiye juu yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana tena.

20:12 Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu cha uzima, kikafunguliwa pia. Wafu wakahukumiwa kadiri ya matendo yao, kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo.

20:13 Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; kifo na kuzimu vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana na matendo yake.

20:14 Kisha kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili.

20:15 Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika ziwa la moto.

21:1 Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuweko tena.

21:2 Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe.

21:3 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema, "Tazama! Mungu amefanya makao yake kati ya watu. Atakaa kati yao, nao watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao.

21:4 Yeye atayafuta machozi yao yote; maana hakutakuwako tena na kifo, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!"

21:5 Kisha yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi akasema, "Tazama, nafanya yote mapya." Tena akaniambia, "Andika hili, maana maneno haya ni ya kuaminika na ya kweli!"

21:6 Kisha akaniambia, "Yametimia! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Aliye na kiu nitampa kinywaji cha bure kutoka katika chemchemi ya maji ya uzima.

21:7 Yeyote atakayeshinda atapokea hiki, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

21:8 Lakini watu waoga, wasioamini, wapotovu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote, mahali pao patakuwa ndani ya lile ziwa linalowaka moto na kiberiti; hicho ndicho kifo cha pili."

21:9 Kisha mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba yaliyokuwa yamejaa mabaa saba ya mwisho, akaja na kuniambia, "Njoo! Mimi nitakuonyesha bibi arusi, mkewe Mwanakondoo!"

21:10 Basi, Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionyesha mji mtakatifu, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni,

21:11 uking'aa kwa utukufu wa Mungu. Mwangaza wake ulikuwa kama wa jiwe la thamani kubwa kama yaspi, angavu kama kioo.

21:12 Ulikuwa na ukuta mrefu na mkubwa, wenye milango kumi na miwili, na malaika wanangojea kumi na wawili. Majina ya wangoja milango kumi na mawili ya Israeli yalikuwa yameandikwa juu ya milango hiyo.

21:13 Kila upande ulikuwa na milango mitatu: upande wa mashariki, milango mitatu, kaskazini milango mitatu, kusini milango mitatu na magharibi milango mitatu.

21:14 Kuta za mji huo zilikuwa zimejengwa juu ya mawe ya msingi kumi na mawili, na juu ya mawe hayo yalikuwa yameandikwa majina na mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.

21:15 Basi, yule malaika aliyekuwa anasema nami alikuwa na kijiti cha dhahabu cha kupimia, kwa ajili ya kuupima huo mji, milango yake na kuta zake.

21:16 Mji wenyewe ulikuwa wa mraba, upana na urefu wake sawa. Basi, malaika akaupima mji huo kwa kijiti chake: ulikuwa na urefu, upana na urefu wa kwenda juu, kama kilomita elfu mbili na mia nne.

21:17 Kisha akaupima ukuta wake pia; nao ulikuwa mita sitini kwa kipimo cha macho cha kibinadamu ambacho malaika alitumia.

21:18 Ukuta huo ulikuwa umejengwa kwa mawe mekundu ya thamani, na mji wenyewe ulikuwa umejengwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo.

21:19 Mawe ya msingi wa ukuta huo yalikuwa yamepambwa kwa kila aina ya mawe ya thamani. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa jiwe la thamani jekundu, la pili yakuti samawati, la tatu kalkedoni, la nne zamaradi,

21:20 la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolito, la nane zabarijadi, la tisa topazi, la kumi krisopraso, la kumi na moja yasinto, na la kumi na mbili amethisto.

21:21 Na ile milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili; kila mlango ulikuwa umetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji ilikuwa imetengenezwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo.

21:22 Sikuona hekalu katika mji huo, maana Bwana Mungu Mwenye Uwezo na yule Mwanakondoo ndio Hekalu lake.

21:23 Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuangazia, maana utukufu wa Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwanakondoo.

21:24 Watu wa mataifa watatembea katika mwanga wake, na wafalme wa dunia watauletea utajiri wao.

21:25 Milango ya mji huo itakuwa wazi mchana wote; maana hakutakuwa na usiku humo.

21:26 Fahari na utajiri wa watu wa mataifa utaletwa humo ndani.

21:27 Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni wale tu walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo ndio watakaoingia ndani.

22:1 Kisha malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima maangavu kama kioo yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo.

22:2 Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uzima unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa.

22:3 Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu.

22:4 Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao.

22:5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele.

22:6 Kisha malaika akaniambia, "Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde.

22:7 "Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki."

22:8 Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionyesha mambo hayo, nikataka kumwabudu.

22:9 Lakini yeye akaniambia, "Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!"

22:10 Tena akaniambia, "Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia.

22:11 Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu."

22:12 "Sikiliza!" Asema Yesu, "Naja upesi, pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake.

22:13 Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wa kwanza na wa mwisho."

22:14 Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, kwani watakuwa na haki ya kula tunda la mti wa uzima, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake.

22:15 Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji.

22:16 "Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!"

22:17 Roho na Bibiarusi waseme, "Njoo!" Kila mtu asikiaye hili, na aseme, "Njoo!" Kisha, yeyote aliye na kiu na aje; anayetaka maji ya uzima na apokee bila malipo yoyote.

22:18 Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

22:19 Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang'anya sehemu yake katika ule mti wa uzima, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki.

22:20 Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: "Naam! Naja upesi." Amina. Na iwe hivyo! Njoo Bwana Yesu!

22:21 Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amen.