Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: Hebrews

1:1 Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii,

1:2 lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu na akamteua avimiliki vitu vyote.

1:3 Yeye ni mng'ao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwapatia binadamu msamaha wa dhambi zao, aliketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu.

1:4 Mwana ni mkuu zaidi kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu zaidi kuliko jina lao.

1:5 Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Wewe ni Mwanangu; Mimi leo nimekuwa Baba yako." Wala hakusema juu ya malaika yeyote: "Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu."

1:6 Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, alisema: "Malaika wote wa Mungu wanapaswa kumwabudu."

1:7 Lakini kuhusu malaika, Mungu alisema: "Mungu awafanya malaika wake kuwa pepo, na watumishi wake kuwa ndimi za moto."

1:8 Lakini kumhusu Mwana, Mungu alisema: "Utawala wako ee Mungu, wadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki.

1:9 Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako."

1:10 Pia alisema: "Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako.

1:11 Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi.

1:12 Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma."

1:13 Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako."

1:14 Malaika ni roho tu wanaomtumikia Mungu, na Mungu huwatuma wawasaidie wale watakaopokea wokovu.

2:1 Kwa sababu hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini zaidi yote tuliyosikia, ili tusije tukapotoshwa.

2:2 Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulionyeshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili.

2:3 Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli.

2:4 Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake.

2:5 Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake.

2:6 Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: "Mtu ni nini ee Mungu, hata umfikirie; mwanaadamu ni nini hata umjali?

2:7 Ulimfanya kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika; ukamvika taji ya utukufu na heshima,

2:8 ukaweka kila kitu chini ya miguu yake, avitawale." Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa.

2:9 Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka.

2:10 Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu.

2:11 Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao ndugu zake;

2:12 kama asemavyo: "Ee Mungu, nitawatangazia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao."

2:13 Tena asema: "Nitamwekea Mungu tumaini langu." Na tena: "Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu."

2:14 Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili kwa njia ya kifo chake amwangamize Ibilisi, ambaye ana mamlaka juu ya kifo,

2:15 na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo.

2:16 Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kwa ajili ya kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko; "Anawasaidia wazawa wa Abrahamu."

2:17 Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe.

2:18 Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.

3:1 Ndugu zangu watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu ambaye Mungu alimtuma awe Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama.

3:2 Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.

3:3 Mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Hali kadhalika naye Yesu anastahili heshima kubwa zaidi kuliko Mose.

3:4 Kila nyumba hujengwa na mjenzi fulani--na Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote.

3:5 Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye.

3:6 Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi ni nyumba yake kama tukizingatia uhodari wetu na uthabiti wetu katika kile tunachotumainia.

3:7 Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo,

3:8 msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu; kama walivyokuwa siku ile kule jangwani,

3:9 Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, asema Bwana, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu kwa miaka arobaini.

3:10 Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu.

3:11 Basi, nilikasirika, nikaapa: Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."

3:12 Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai.

3:13 Maadamu hiyo "Leo" inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi.

3:14 Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni.

3:15 Maandiko yasema hivi: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu."

3:16 Ni akina nani basi, waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri.

3:17 Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arobaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani.

3:18 Mungu alipoapa: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko," alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi.

3:19 Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.

4:1 Mungu alituahidia kwamba tutaweza kupata pumziko hilo alilosema. Basi, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo.

4:2 Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani.

4:3 Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema: "Nilikasirika, nikaapa: Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko." Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu.

4:4 Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: "Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote."

4:5 Tena jambo hili lasemwa pia: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."

4:6 Wale waliotangulia kuhubiriwa Habari Njema hawakupata pumziko hilo kwa sababu hawakuamini. Wapo, basi, wengine ambao wangejaliwa kulipata.

4:7 Jambo hili ni wazi, kwani Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa "Leo". Miaka mingi baadaye Mungu alisema juu ya hiyo siku kwa maneno ya Daudi katika Maandiko yaliyokwisha tajwa: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu."

4:8 Kama Yoshua angaliwapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine.

4:9 Kwa hiyo, basi, bado lipo pumziko kwa watu wa Mungu kama kule kupumzika kwake Mungu siku ya saba.

4:10 Maana, kila anayepata pumziko aliloahidi Mungu atapumzika baada ya kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika baada ya yake.

4:11 Basi, tujitahidi kupata pumziko hilo, ili asiwepo yeyote miongoni mwenu atakayeshindwa, kama walivyofanya wao kwa sababu ya ukosefu wao wa imani.

4:12 Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na mafuta. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya watu.

4:13 Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake. Kwake, sisi sote tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu.

4:14 Basi, tunapaswa kuzingatia kwa uthabiti imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka kwa Mungu mwenyewe--Yesu, Mwana wa Mungu.

4:15 Huyu Kuhani Mkuu wetu si mmoja ambaye hawezi kutuunga mkono katika unyonge wetu, ila ni Kuhani Mkuu ambaye alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi.

4:16 Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu, palipo na neema, ili tukajipatie huruma na neema ya kutusaidia wakati wa lazima.

5:1 Kila kuhani mkuu huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa niaba yao, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi zao.

5:2 Maadamu yeye mwenyewe yu dhaifu anaweza kuwaonea huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa.

5:3 Na kwa vile yeye mwenyewe ni dhaifu, anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake.

5:4 Hakuna mtu awezaye kujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.

5:5 Hali kadhalika naye Kristo hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimwambia: "Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako."

5:6 Alisema pia mahali pengine: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

5:7 Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu.

5:8 Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso.

5:9 Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii,

5:10 naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.

5:11 Tunayo Mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu ninyi si wepesi wa kuelewa.

5:12 Sasa mngalipaswa kuwa tayari walimu, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo ya ujumbe wa Mungu. Badala ya kula chakula kigumu, mnapaswa bado kunywa maziwa.

5:13 Kila anayepaswa kunywa maziwa huyo ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini.

5:14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, ambao wanaweza kubainisha mema na mabaya.

6:1 Basi, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa na kuyaacha nyuma yale mafundisho ya mwanzo ya Kikristo. Hatuhitaji kuweka msingi tena kwa kurudia yale mafundisho ya mwanzo kama vile kuachana na matendo ya kifo, kumwamini Mungu;

6:2 mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele.

6:3 tusonge mbele! Hayo tutayafanya, Mungu akitujalia.

6:4 Maana watu wanaoiasi imani yao inawezekanaje kuwarudisha watubu tena? Watu hao walikwisha kuwa katika mwanga wa Mungu, walikwisha onja zawadi ya mbinguni na kushirikishwa Roho Mtakatifu;

6:5 walikwisha onja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao,

6:6 kisha wakaiasi imani yao! Haiwezekani kuwarudisha watubu tena, kwa sababu wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu na kumwaibisha hadharani.

6:7 Mungu huibariki ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima.

6:8 Lakini kama ardhi hiyo ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto.

6:9 Lakini, ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tunalo tumaini kubwa juu ya hali yenu. Tunajua kwamba mmepokea baraka zile bora za wokovu wenu.

6:10 Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake.

6:11 Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aonyeshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia.

6:12 Msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu na hivyo wanapokea yake aliyoahidi Mungu.

6:13 Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa jina lake mwenyewe, maana hakuna aliye mkuu kuliko Mungu ambaye kwa huyo angeweza kuapa.

6:14 Mungu alisema: "Hakika nitakubariki na nitakupa wazawa wengi."

6:15 Abrahamu alisubiri kwa uvumilivu na hivyo alipokea kile alichoahidiwa na Mungu.

6:16 Watu wanapoapa, huapa kwa mmoja aliye mkuu zaidi kuliko wao, na kiapo hicho husuluhisha ubishi wote.

6:17 Naye Mungu aliimarisha ahadi yake kwa kiapo; na kwa namna hiyo akawaonyesha wazi wale aliowaahidia kwamba hatabadili nia yake.

6:18 Basi, kuna vitu hivi viwili: ahadi na kiapo, ambavyo haviwezi kubadilika na wala juu ya hivyo Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo sisi tuliokimbilia usalama kwake, tunapewa moyo wa kushikilia imara tumaini lililowekwa mbele yetu.

6:19 Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo ni imara na thabiti, nalo lapenya lile pazia la hekalu la mbinguni mpaka patakatifu ndani.

6:20 Yesu ametangulia kuingia humo kwa niaba yetu, na amekuwa kuhani mkuu milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.

7:1 Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye akambariki,

7:2 naye Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina hili Melkisedeki ni "Mfalme wa Uadilifu"; na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya "Mfalme wa Amani.")

7:3 Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima.

7:4 Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Baba Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka vitani.

7:5 Tunajua vilevile kwamba kufuatana na Sheria, wana wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni watoto wa Abrahamu.

7:6 Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu.

7:7 Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu zaidi kuliko yule anayebarikiwa.

7:8 Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi.

7:9 Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye watoto wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia.

7:10 Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye.

7:11 Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa Sheria. Sasa, kama huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu hapangekuwa tena na haja ya kutokea ukuhani mwingine tofauti, ukuhani ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, na si ule wa Aroni.

7:12 Maana ukuhani ukibadilika ni lazima Sheria nayo ibadilike.

7:13 Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani.

7:14 Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani.

7:15 Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea.

7:16 Yeye hakufanywa kuwa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho.

7:17 Maana Maandiko yasema: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

7:18 Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu.

7:19 Maana Sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu.

7:20 Zaidi ya hayo hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo.

7:21 Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia: "Bwana ameapa, wala hataigeuza nia yake: Wewe ni kuhani milele."

7:22 Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.

7:23 Kuna tofauti nyingine pia: hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao.

7:24 Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake.

7:25 Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu.

7:26 Basi, Yesu ndiye Kuhani Mkuu ambaye anatufaa sana katika mahitaji yetu. Yeye ni mtakatifu, hana hatia wala dhambi ndani yake; hayumo katika kundi la wenye dhambi na ameinuliwa mpaka juu mbinguni.

7:27 Yeye si kama wale makuhani wakuu wengine; hana haja ya kutoa dhabihu kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alifanya hivyo mara moja tu wakati alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote.

7:28 Sheria ya Mose huwateua watu waliokuwa dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana ambaye amefanywa mkamilifu milele.

8:1 Basi, jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: sisi tunaye Kuhani Mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu mbinguni.

8:2 Yeye hutoa huduma ya Kuhani Mkuu katika Mahali Patakatifu sana, yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu.

8:3 Kila Kuhani Mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu vipawa na dhabihu, na hivyo Kuhani Mkuu wetu lazima pia awe na kitu cha kutolea.

8:4 Kama yeye angekuwa wa hapa duninani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani wengine wanaotoa sadaka kufuatana na Sheria.

8:5 Huduma zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Ndivyo pia ilivyokuwa kwa Mose. Wakati alipokuwa karibu kuitengeneza ile hema, Mungu alimwambia: "Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano ulioonyeshwa kule mlimani."

8:6 Lakini sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora zaidi kuliko yao, kama vile agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi.

8:7 Maana kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya agano la pili.

8:8 Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: "Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na kabila la Yuda.

8:9 Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku ile nilipowaongoza kwa mkono kutoka nchi ya Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana.

8:10 Na hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

8:11 Hakuna mtu atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: Mjue Bwana. Maana watu wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi.

8:12 Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao."

8:13 Kwa kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni.

9:1 Agano la kwanza lilikuwa na taratibu zake za ibada na pia mahali patakatifu pa ibada palipojengwa na watu.

9:2 Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje iliitwa Mahali Patakatifu. Humo mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyotolewa kwa Mungu.

9:3 Nyuma ya pazia la pili, kulikuwa na hema iliyoitwa Mahali Patakatifu Kupita Pote.

9:4 Humo mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na Sanduku la Agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana; fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vilivyoandikwa agano.

9:5 Juu ya hilo Sanduku kulikuwa na viumbe vilivyodhihirisha kuweko kwa Mungu, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa. Lakini sasa, hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo.

9:6 Mipango hiyo ilitekelezwa kisha ikawa desturi kwa makuhani kuingia kila siku katika hema ya nje kutoa huduma zao.

9:7 Lakini kuhani Mkuu peke yake ndiye anayeingia katika lile hema la pili; naye hufanya hivyo mara moja tu kwa mwaka. Anapoingia ndani huwa amechukua damu ambayo anamtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi ambazo watu wamezitenda bila wao wenyewe kujua.

9:8 Kutokana na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu haijafunguliwa.

9:9 Jambo hili ni mfano wa nyakati za sasa. Linaonyesha kwamba zawadi na dhabihu zinazotolewa kwa Mungu haziwezi kuifanya mioyo ya wale wanaoabudu kuwa mikamilifu,

9:10 kwani haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha. Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu atakaporekebisha vitu vyote.

9:11 Lakini Kristo amekwisha fika, akiwa Kuhani Mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa.

9:12 Yeye aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, tena hakuwa amechukua damu ya mbuzi wala ng'ombe, bali aliingia kwa damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa milele.

9:13 Watu waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu ya mbuzi na ya ng'ombe pamoja na majivu ya ndama.

9:14 Lakini, kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu za Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe dhabihu kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai.

9:15 Kwa hiyo, Kristo ndiye aliyeratibisha agano jipya ili wale walioitwa na Mungu wazipokee baraka za milele walizoahidiwa. Watazipata, kwani kifo kimetokea ambacho huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale.

9:16 Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa.

9:17 Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi.

9:18 Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa.

9:19 Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika Sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa kutumia majani ya mti uitwao husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha Sheria na hao watu wote.

9:20 Mose alisema: "Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii."

9:21 Vilevile Mose aliinyunyizia damu ile hema na vyombo vya ibada.

9:22 Naam, kadiri ya Sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa.

9:23 Vitu hivi ambavyo ni mfano tu wa mambo halisi ya mbinguni, vililazimika kutakaswa kwa namna hiyo. Lakini vitu vya mbinguni huhitaji dhabihu iliyo bora zaidi.

9:24 Maana Kristo hakuingia Mahali Patakatifu palipojengwa kwa mikono ya watu, ambapo ni mfano tu wa kile kilicho halisi. yeye aliingia mbinguni kwenyewe ambako sasa anasimama mbele ya Mungu kwa ajili yetu.

9:25 Kuhani Mkuu wa Wayahudi huingia Mahali Patakatifu kila mwaka akiwa amechukua damu ya mnyama; lakini Kristo hakuingia humo ili ajitoe mwenyewe mara nyingi,

9:26 maana ingalikuwa hivyo, Kristo angalipaswa kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa ulimwengu. Lakini sasa nyakati hizi zinapokaribia mwisho wake, yeye ametokea mara moja tu, kuondoa dhambi kwa kujitoa yeye mwenyewe dhabihu.

9:27 Basi, kama vile kila mtu hufa mara moja tu, kisha husimama mbele ya hukumu ya Mungu,

9:28 vivyo hivyo Kristo naye alijitoa dhabihu mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi za wengi. Atakapotokea mara ya pili si kwa ajili ya kupambana na dhambi, bali ni kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomngojea.

10:1 Sheria ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje, basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu?

10:2 Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma.

10:3 Lakini dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao.

10:4 Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi.

10:5 Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: "Hukutaka dhabihu wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili.

10:6 Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi.

10:7 Hapo nikasema: Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha Sheria."

10:8 Kwanza alisema: "Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi." Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na Sheria.

10:9 Kisha akasema: "Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako." Hivyo Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine moja.

10:10 Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.

10:11 Kila kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi, dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi.

10:12 Lakini Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha akaketi upande wa kulia wa Mungu.

10:13 Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake.

10:14 Basi, kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.

10:15 Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema:

10:16 "Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao."

10:17 Kisha akaongeza kusema: "Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu."

10:18 Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa dhambi.

10:19 Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu.

10:20 Yeye ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake mwenyewe.

10:21 Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu.

10:22 Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.

10:23 Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.

10:24 Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.

10:25 Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia.

10:26 Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi.

10:27 Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga.

10:28 Mtu yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu.

10:29 Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani?

10:30 Maana tunamfahamu yule aliyesema, "Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza," na ambaye alisema pia, "Bwana atawahukumu watu wake."

10:31 Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno!

10:32 Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili.

10:33 Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo.

10:34 Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang'anywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele.

10:35 Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa.

10:36 Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi.

10:37 Maana kama yasemavyo Maandiko: "Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia.

10:38 Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye."

10:39 Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na tunaokolewa.

11:1 Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona.

11:2 Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao.

11:3 Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana.

11:4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu iliyokuwa bora zaidi kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa amekufa, bado ananena.

11:5 Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu.

11:6 Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta.

11:7 Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hakuweza kuyaona bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani.

11:8 Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama.

11:9 Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile.

11:10 Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga.

11:11 Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri.

11:12 Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani.

11:13 Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani.

11:14 Watu wanaosema mambo kama hayo, huonyesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe.

11:15 Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko.

11:16 Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndiyo maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji.

11:17 Kwa imani, Abrahamu alimtoa mwanae Isaka sadaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa dhabihu mwanae wa pekee,

11:18 ingawa Mungu alikuwa amemwambia: "Wazawa wako watatokana na Isaka."

11:19 Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu: na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanae kutoka wafu.

11:20 Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye.

11:21 Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea ile fimbo yake.

11:22 Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake.

11:23 Kwa imani wazazi wa Mose walimficha huyo mtoto kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Walimwona kuwa ni mtoto mzuri, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

11:24 Kwa imani Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao.

11:25 Aliona ni afadhali kuteseka pamoja na watu wa Mungu kuliko kufurahia raha ya dhambi kwa kitambo kidogo.

11:26 Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Masiha kuna faida kubwa zaidi kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye.

11:27 Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana.

11:28 Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli.

11:29 Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu, kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji.

11:30 Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kwa muda wa siku saba.

11:31 Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi.

11:32 Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gedeoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii.

11:33 Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba,

11:34 Walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga. Walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita wakashinda majeshi ya kigeni.

11:35 Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi.

11:36 Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani.

11:37 Walipigwa mawe, walipasuliwa vipandevipande, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi, walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa.

11:38 Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na mlimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi.

11:39 Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidia,

11:40 maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi.

12:1 Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotung'ang'ania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu.

12:2 Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kujali juu ya aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.

12:3 Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa.

12:4 Maana katika kupambana na dhambi, ninyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu.

12:5 Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja ninyi kuwa wanawe? "Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya.

12:6 Maana Bwana humwadhibu kila anayempenda, humpinga kila anayekubali kuwa mwanae."

12:7 Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea ninyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake?

12:8 Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, ninyi si wanawe, bali ni wana haramu.

12:9 Zaidi ya hayo sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi.

12:10 Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake.

12:11 Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili!

12:12 Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu.

12:13 Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe.

12:14 Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo.

12:15 Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake.

12:16 Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja.

12:17 Ninyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.

12:18 Ninyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli, hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani,

12:19 mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno jingine,

12:20 kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa: "Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe."

12:21 Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema, "Naogopa na kutetemeka."

12:22 Lakini ninyi mmefika katika mlima wa Sioni, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika elfu nyingi wasiohesabika.

12:23 Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa kuwa wakamilifu.

12:24 Mmefika kwa Yesu ambaye ameratibisha agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema zaidi kuliko ile ya Abeli.

12:25 Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza yeye ambaye anasema nanyi. Kama wale walikataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni?

12:26 Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: "Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu."

12:27 Neno hili: "tena" linatuonyesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa.

12:28 Sisi basi, na tushukuru kwani tunapokea utawala usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu;

12:29 maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.

13:1 Endeleeni kupendana kidugu.

13:2 Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua.

13:3 Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao.

13:4 Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi.

13:5 Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: "Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa."

13:6 Ndiyo maana tunathubutu kusema: "Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?"

13:7 wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni ujumbe wa Mungu. Fikirieni juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao.

13:8 Yesu Kristo ni yuleyule, jana, leo na milele.

13:9 Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata.

13:10 Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi, hawana haki ya kula vitu vyake.

13:11 Kuhani Mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi.

13:12 Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji.

13:13 Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake.

13:14 Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja.

13:15 Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa na midomo inayoliungama jina lake.

13:16 Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo dhabihu zinazompendeza Mungu.

13:17 Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu.

13:18 Tuombeeni na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima.

13:19 Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.

13:20 Mungu amemfufua Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele.

13:21 Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze mapenzi yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.

13:22 Basi, ndugu, nawasihi mpokee kwa utulivu ujumbe huu wa kuwatieni moyo. Hii ni barua fupi tu ambayo nimewaandikieni.

13:23 Napenda kuwajulisheni kwamba ndugu yetu Timotheo amekwisha funguliwa gerezani. Kama akifika hapa mapema, nitakuja naye nitakapokuja kwenu.

13:24 Wasalimieni viongozi wenu wote pamoja na watu wa Mungu! Ndugu wa Italia wanawasalimuni.

13:25 Tunawatakieni nyote neema ya Mungu.


Next: James