Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: 1 Timothy

1:1 Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu,

1:2 nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu.

1:3 Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao.

1:4 Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani.

1:5 Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli.

1:6 Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana.

1:7 Wanapenda kuwa walimu wa Sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza.

1:8 Twajua kwamba Sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo.

1:9 Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia. Watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale;

1:10 sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wanaowaiba watu, waongo, na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho ya kweli.

1:11 Mafundisho hayo hupatikana katika Habari Njema ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri, Habari Njema ya Mungu mtukufu na mwenye heri.

1:12 Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie,

1:13 ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya.

1:14 Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu.

1:15 Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote,

1:16 lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aonyeshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uzima wa milele.

1:17 Kwake yeye aliye Mfalme wa milele na asiyekufa, yeye aliye Mungu pekee--kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina.

1:18 Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri,

1:19 na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao.

1:20 Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

2:1 Kwanza kabisa, basi naomba dua, sala, maombi na sala za shukrani zitolewe kwa Mungu kwa ajili ya watu wote,

2:2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema.

2:3 Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu,

2:4 ambaye anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli.

2:5 Maana yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu Kristo Yesu,

2:6 ambaye alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao ulipowadia.

2:7 Kwa sababu hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo!

2:8 Basi, popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi.

2:9 Hali kadhalika, nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao; wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa,

2:10 bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu.

2:11 Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza.

2:12 Mimi simruhusu mwanamke amfundishe au amtawale mwanamume; anapaswa kukaa kimya.

2:13 Maana Adamu aliumbwa kwanza, halafu Hawa.

2:14 Na wala si Adamu aliyedanganywa; bali mwanamke ndiye aliyedanganywa, akaivunja sheria ya Mungu.

2:15 Hata hivyo, mwanamke ataokolewa kwa kupata watoto, kama akidumu katika imani, upendo, utakatifu na unyofu.

3:1 Msemo huu ni wa kweli: mtu akitaka kuwa kiongozi katika kanisa, huyo anatamani kazi nzuri.

3:2 Basi, kiongozi wa kanisa anapaswa awe mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu; ni lazima awe mkarimu na anayeweza kufundisha;

3:3 asiwe mlevi au mtu wa matata, bali awe mpole, apendaye amani; asiwe mtu wa kupenda fedha;

3:4 anapaswa awe mtu awezaye kuongoza vema nyumba yake, na kuwafanya watoto wake wawe watii kwa heshima yote.

3:5 Maana kama mtu hawezi kuongoza vema nyumba yake, atawezaje kulitunza kanisa la Mungu?

3:6 Mtu ambaye hajakomaa bado katika imani asifanywe kuwa kiongozi katika kanisa, asije akajaa majivuno na kuhukumiwa kama vile Ibilisi alivyohukumiwa.

3:7 Anapaswa awe mwenye sifa njema kati ya watu walio nje ya kanisa, ili asije akalaumiwa na kuanguka katika mtego wa Ibilisi.

3:8 Wasaidizi katika kanisa wanapaswa pia kuwa watu wenye tabia njema na wanyofu; wasiwe wanywaji mno wa divai au wenye tamaa ya fedha;

3:9 wanapaswa kuzingatia kwa dhamiri njema ukweli wa ndani wa imani.

3:10 Ni lazima kwanza wathibitishwe, na wakionekana kuwa wanafaa, basi, watoe huduma yao.

3:11 Wake zao wanapaswa pia kuwa na tabia njema, wasiowasengenya watu, wenye kiasi na waaminifu katika mambo yote.

3:12 Msaidizi katika kanisa lazima awe na mke moja tu, na awezaye kuongoza vema watoto wake na nyumba yake.

3:13 Maana wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu.

3:14 Ninakuandikia barua hii nikiwa na matumaini ya kuja kwako hivi karibuni.

3:15 Lakini kama nikicheleweshwa, basi, barua hii itakufahamisha mwenendo tunaopaswa kuwa nao katika nyumba ya Mungu, ambayo ni kanisa la Mungu aliye hai, na ambalo ni nguzo na msingi wa ukweli.

3:16 Hakuna mashaka yoyote juu ya ukuu wa siri ya dini yetu: Alionekana katika umbo la kibinadamu alithibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu, akaonekana na malaika. Alihubiriwa kati ya mataifa, aliaminiwa popote ulimwenguni, akachukuliwa juu mbinguni katika utukufu.

4:1 Roho asema waziwazi kwamba siku za baadaye watu wengine wataitupilia mbali imani; watazitii roho danganyifu na kufuata mafundisho ya pepo.

4:2 Mafundisho ya namna hiyo yanaenezwa na watu waongo wadanganyifu, ambao dhamiri zao ziko kama zimechomwa kwa chuma cha moto.

4:3 Watu hao hufundisha kwamba ni makosa kuona na pia kula vyakula fulani. Lakini Mungu aliviumba vyakula hivyo, ili wale walio waumini na ambao wanapata kuujua ukweli, wavitumie kwa shukrani.

4:4 Kila kitu alichoumba Mungu ni chema, wala hakuna kinachohitaji kukataliwa, bali vyote vipokelewe kwa sala ya shukrani,

4:5 kwa sababu neno la Mungu na sala hukifanya kitu hicho kikubalike kwa Mungu.

4:6 Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli, ambayo wewe umeyafuata.

4:7 Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu.

4:8 Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uzima katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja.

4:9 Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa.

4:10 Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini.

4:11 Wape maagizo hayo na mafundisho hayo.

4:12 Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi.

4:13 Tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani Maandiko Matakatifu, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja.

4:14 Usiache kukitumia kile kipaji cha Kristo ndani yako ulichopewa kwa maneno ya manabii na kwa kuwekewa mikono na wazee.

4:15 Fikiri kwa makini juu ya hayo yote na kuyatekeleza kusudi maendeleo yako yaonekane na wote.

4:16 Angalia sana mambo yako mwenyewe, na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo maana ukifanya hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.

5:1 Usimkemee mtu mzee, bali msihi kama vile angekuwa baba yako. Watendee vijana kama ndugu zako,

5:2 wanawake wazee kama mama yako, na wasichana kama dada zako, kwa usafi wote.

5:3 Waheshimu wanawake wajane walio wajane kweli.

5:4 Lakini mjane aliye na watoto au wajukuu, hao wanapaswa kujifunza kutimiza wajibu wao wa kidini kwa jamaa zao wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wao na wazee wao, kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele ya Mungu.

5:5 Mwanamke mjane kweli, asiye na mtu wa kumsaidia, amemwekea Mungu tumaini lake na huendelea kusali na kumwomba msaada usiku na mchana.

5:6 Lakini mwanamke ambaye huishi maisha ya anasa, huyo amekufa, ingawa yu hai.

5:7 Wape maagizo haya, wasije wakawa na lawama.

5:8 Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini.

5:9 Usimtie katika orodha ya wajane, mjane yeyote ambaye hajatimiza miaka sitini. Tena awe amepata kuolewa mara moja tu,

5:10 na awe mwenye sifa nzuri: aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema.

5:11 Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo watataka kuolewa tena,

5:12 na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali.

5:13 Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema.

5:14 Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili adui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu.

5:15 Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani.

5:16 Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachilia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa.

5:17 Wazee wanaowaongoza watu vizuri wanastahili kupata riziki maradufu, hasa wale wanaofanya bidii katika kuhubiri na kufundisha.

5:18 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Usimfunge ng'ombe kinywa anapopura nafaka." na tena "Mfanyakazi astahili malipo yake."

5:19 Usikubali kupokea mashtaka dhidi ya mzee yasipowakilishwa na mashahidi wawili au watatu.

5:20 Wale wanaotenda dhambi waonye hadharani, ili wengine wapate kuogopa.

5:21 Nakuamuru mbele ya Mungu, mbele ya Kristo Yesu, na mbele ya malaika watakatifu uyazingatie maagizo haya bila kuacha hata moja, wala kumpendelea mtu yeyote katika kila unachotenda.

5:22 Usiharakishe kumwekea mtu yeyote mikono kwa ajili ya kumtumikia Bwana. Usishiriki dhambi za wengine; jiweke katika hali safi.

5:23 Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara.

5:24 Dhambi za watu wengine huonekana waziwazi, nazo zawatangulia kwenye hukumu; lakini dhambi za wengine huonekana tu baadaye.

5:25 Vivyo hivyo, matendo mema huonekana waziwazi, na hata yale ambayo si dhahiri hayawezi kufichika.

6:1 Watumwa wote wanapaswa kuwaheshimu wakuu wao ili kusiwe na sababu ya watu kulitukana jina la Mungu na mafundisho yetu.

6:2 Watumwa ambao wakuu wao ni Wakristo wasiwadharau kwani ni ndugu zao. Badala yake, wanapaswa kuwatumikia hata vizuri zaidi, maana hao wanaopata faida kutokana na kazi yao ni waumini ambao wanawapenda. Unapaswa kufundisha na kuhubiri mambo haya.

6:3 Mtu yeyote anayefundisha kinyume cha mambo haya, na ambaye hakubaliani na maneno ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo na mafundisho ya dini,

6:4 huyo amejaa majivuno na wala hajui chochote. Ni mtu wa kupenda ubishi na magombano juu ya maneno matupu, na hiyo husababisha wivu, ugomvi, matusi, shuku mbaya,

6:5 na ubishi usio na kikomo kutoka kwa watu ambao akili zao zimeharibika, na ambao hawana tena ukweli. Wanadhani dini ni njia ya kujipatia utajiri.

6:6 Kweli dini humfanya mtu awe tajiri sana, ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo.

6:7 Maana hatukuleta kitu chochote hapa duniani, wala hatutachukua chochote.

6:8 Kwa hiyo basi, kama tunacho chakula na mavazi, tunapaswa kuridhika navyo.

6:9 Lakini wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu, na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na maangamizi.

6:10 Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote. Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na imani, na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi.

6:11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo. Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, mapendo, subira na unyenyekevu.

6:12 Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uzima wa milele, uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi.

6:13 Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato,

6:14 nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka Siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo.

6:15 Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.

6:16 Yeye peke yake anaishi milele, katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina.

6:17 Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie.

6:18 Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao.

6:19 Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uzima ambao ni uzima wa kweli.

6:20 Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa. Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile wanachokiita watu wengine: "Elimu".

6:21 Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo yake wamepoteza imani. Nawatakieni nyote neema!


Next: 2 Timothy