Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: 1 Thessalonians

1:1 Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana Yesu Kristo.

1:2 Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu.

1:3 Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonyesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti.

1:4 Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake,

1:5 maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu.

1:6 Ninyi mlifuata mfano wetu, na kumwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu.

1:7 Kwa hiyo ninyi mmekuwa mfano mzuri kwa waumini wote wa Makedonia na Akaya.

1:8 Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si tu huko Makedonia na Akaya, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi.

1:9 Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: jinsi mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu mkamgeukia Mungu aliye hai na wa kweli,

1:10 na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, Yesu, ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu, na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya Mungu inayokuja.

2:1 Ndugu, ninyi wenyewe mnafahamu kwamba ziara yetu kwenu haikuwa bure.

2:2 Mnajua jinsi tulivyodhulumiwa na kutukanwa kule Filipi kabla ya kufika kwenu Thesalonike. Ingawa kulikuwa na upinzani mwingi, Mungu wetu alitujalia uhodari wa kuwahubirieni Habari Njema yake.

2:3 Jambo tunalosisitiza kwenu si jambo linalotegemea uongo au nia mbaya; wala hatupendi kumdanganya mtu yeyote.

2:4 Sisi twanena daima kama atakavyo Mungu kwani yeye alituona kwamba tunafaa, akatukabidhi hii Habari Njema. Si nia yetu kuwapendeza watu hata kidogo, bali twataka kumpendeza Mungu ambaye anajua mioyo yetu mpaka ndani.

2:5 Ninyi mnajua kwamba sisi hatukuja kwenu na maneno matamu ya kubembeleza wala hatukutumia maneno ya kijanja ya kuficha ubinafsi fulani; Mungu ni shahidi!

2:6 Hatukutafuta sifa kutoka kwa watu, wala kutoka kwenu, wala kutoka kwa mtu yeyote,

2:7 ingawa sisi tukiwa mitume wa Kristo, tungeweza kudai mambo fulani kwenu. Lakini sisi tulikuwa Wapole kati yenu kama alivyo mama kwa watoto wake.

2:8 Tuliwapenda ninyi sana hata tukawa tayari kuwashirikisha si tu Habari Njema ya Mungu, bali pia na maisha yetu. Ndivyo mlivyokuwa wapenzi wetu!

2:9 Ndugu, mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi na kutaabika. Tulipowaleteeni Habari Njema ya Mungu tulifanya kazi mchana na usiku kusudi tusiwe mzigo kwa mtu yeyote miongoni mwenu.

2:10 Ninyi mnaweza kushuhudia, na Mungu pia ni shahidi, jinsi mwenendo wetu kati yenu ninyi mnaoamini ulivyokuwa mzuri, mwadilifu na usio na lawama.

2:11 Mnajua kwamba sisi tulimtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake mwenyewe.

2:12 Tuliwapeni moyo, tuliwafarijini na kuwahimiza ili mpate kuishi maisha yampendezayo Mungu ambaye aliwaiteni mshiriki Utawala na utukufu wake.

2:13 Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu: tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, ninyi mliusikia mkaupokea, si kama vile ujumbe wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu anafanya kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.

2:14 Ndugu, ninyi mmepatwa na mambo yaleyale yaliyoyapata makanisa ya Mungu kule Yudea, mambo yaliyowapata watu walio wake Kristo Yesu. Ninyi mlidhulumiwa na wananchi wenzenu kama vile wao walivyodhulumiwa na wenzao Wayahudi,

2:15 ambao walimuua Bwana Yesu na manabii, wakatutesa na sisi pia. Watu hao wanamchukiza Mungu, tena ni adui za kila mtu!

2:16 Hata walijaribu kutuzuia kuwahubiria watu wa mataifa mengine ujumbe utakaowaletea wokovu. Ndivyo walivyokamilisha orodha ya dhambi zote walizotenda siku zote. Lakini sasa hasira ya Mungu imewaangukia.

2:17 Ndugu, kuachana kwetu nanyi kulikuwa kwa muda tu, tena kuachana huko kulikuwa kwa mwili tu na si kwa roho. Kitambo kifupi baadaye, tulishikwa na hamu kubwa ya kuwaoneni tena!

2:18 Kwa hiyo tuliamua kuwatembeleeni tena. Nami, Paulo, nilijaribu kuja kwenu zaidi ya mara moja, lakini Shetani alituzuia.

2:19 Je, tutakaposimama mbele ya Bwana Yesu wakati atakapokuja, fahari ya ushindi wetu itakuwa nini? Itakuwa ni ninyi wenyewe; ninyi ndio tumaini letu na furaha yetu.

2:20 Naam, ninyi ni utukufu wetu na furaha yetu!

3:1 Mwishowe hatukuweza kuvumilia zaidi. Basi, tuliamua kubaki kule Athene peke yetu,

3:2 na kumtuma kwenu ndugu yetu Timotheo, ambaye ni mfanyakazi mwenzetu kwa ajili ya Mungu katika kuhubiri Habari Njema ya Kristo. Tulimtuma ili awaimarisheni na kuwafarijini,

3:3 kusudi imani ya mtu yeyote miongoni mwenu isije ikafifia kwa sababu ya taabu hizo. Ninyi mnajua kwamba tunapaswa kupata mateso.

3:4 Maana, tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwaambieni kwamba tutateswa; na kama mjuavyo ndivyo ilivyotukia.

3:5 Ndio maana nilimtuma Timotheo kwenu. Sikuweza kungoja zaidi, na hivyo nilimtuma nipate habari za imani yenu. Isije ikawa labda Mshawishi aliwajaribuni na kazi yote tuliyofanya miongoni mwenu imepotea bure!

3:6 Sasa Timotheo amekwisha rudi, naye ametupa habari za kufurahisha kuhusu imani na upendo wenu. Ametuarifu kwamba mnatukumbuka daima, na kwamba mna hamu ya kutuona sisi kama nasi tulivyo na hamu ya kuwaoneni.

3:7 Basi, habari za imani yenu zimetutia moyo katika taabu na mateso yetu yote,

3:8 kwani sasa tunaishi kweli ikiwa ninyi mnasimama imara katika kuungana na Bwana.

3:9 Sasa twaweza kumshukuru Mungu wetu kwa ajili yenu. Tunamshukuru kwa furaha tuliyo nayo mbele yake kwa sababu yenu.

3:10 Tunazidi kumwomba Mungu usiku na mchana kwa moyo wetu wote ili atupatie fursa ya kuwaoneni uso kwa uso ili tuweze kurekebisha chochote kilichopungua katika imani yenu.

3:11 Tunamwomba Mungu, Baba yetu mwenyewe, na Bwana wetu Yesu atutayarishie njia ya kuja kwenu.

3:12 Bwana awawezeshe ninyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda ninyi.

3:13 Hivyo ataiimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.

4:1 Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi.

4:2 Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

4:3 Mungu anataka ninyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa.

4:4 Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima,

4:5 na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu.

4:6 Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo.

4:7 Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu.

4:8 Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali amdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu.

4:9 Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana.

4:10 Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu tunawaombeni mfanye hata zaidi.

4:11 Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali.

4:12 Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu.

4:13 Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini.

4:14 Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.

4:15 Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana; sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki, wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia.

4:16 Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza.

4:17 Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana.

4:18 Basi, farijianeni kwa maneno haya.

5:1 Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya.

5:2 Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku.

5:3 Watu watakapokuwa wanasema: "Kila kitu ni shwari na salama" ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo.

5:4 Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi.

5:5 Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza.

5:6 Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi.

5:7 Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku.

5:8 Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma.

5:9 Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,

5:10 ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa.

5:11 Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa.

5:12 Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo.

5:13 Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu.

5:14 Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote.

5:15 Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote.

5:16 Furahini daima,

5:17 salini kila wakati

5:18 na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.

5:19 Msimpinge Roho Mtakatifu;

5:20 msidharau unabii.

5:21 Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema,

5:22 na epukeni kila aina ya uovu.

5:23 Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu--roho, mioyo na miili yenu--mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

5:24 Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.

5:25 Ndugu, tuombeeni na sisi pia.

5:26 Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo.

5:27 Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii.

5:28 Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.


Next: 2 Thessalonians