Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: Mark

1:1 Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

1:2 Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: "Tazama, namtuma mjumbe wangu akutangulie; yeye atakutayarishia njia yako.

1:3 Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni mapito yake."

1:4 Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba ni lazima watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao.

1:5 Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.

1:6 Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.

1:7 Naye alihubiri akisema, "Baada yangu anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.

1:8 Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu."

1:9 Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani.

1:10 Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa.

1:11 Sauti ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe."

1:12 Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani,

1:13 akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamtumikia.

1:14 Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema,

1:15 "Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!"

1:16 Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu.

1:17 Yesu akawaambia, "Nifuateni nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu."

1:18 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

1:19 Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.

1:20 Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.

1:21 Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika Sunagogi, akaanza kufundisha.

1:22 Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama walimu wao wa Sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka.

1:23 Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu,

1:24 akapaaza sauti, "Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa Mungu!"

1:25 Yesu akamkemea, "Nyamaza! Mtoke mtu huyu."

1:26 Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka.

1:27 Watu wote wakashangaa, wakaulizana, "Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!"

1:28 Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika wilaya ya Galilaya.

1:29 Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao.

1:30 Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili.

1:31 Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.

1:32 Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo.

1:33 Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango.

1:34 Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.

1:35 Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali.

1:36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta.

1:37 Walipomwona wakamwambia, "Kila mtu anakutafuta."

1:38 Yesu akawaambia, "Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo."

1:39 Basi, akaenda kila mahali Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo.

1:40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba, "Ukitaka, waweza kunitakasa!"

1:41 Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, "Nataka, takasika!"

1:42 Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika.

1:43 Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwonya vikali,

1:44 "Usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani; kisha utoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona."

1:45 Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.

2:1 Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani.

2:2 Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake,

2:3 wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne.

2:4 Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya dari iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka.

2:5 Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Mwanangu, umesamehewa dhambi zako."

2:6 Baadhi ya walimu wa Sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao,

2:7 "Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake."

2:8 Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, "Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu?

2:9 Ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia mtu huyu aliyepooza, Umesamehewa dhambi zako, au kumwambia, Inuka! Chukua mkeka wako utembee?

2:10 Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza,

2:11 "Nakwambia simama, chukua mkeka wako uende nyumbani!"

2:12 Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka, akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema, "Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili."

2:13 Yesu alikwenda tena kando ya ziwa. Umati wa watu ukamwendea, naye akaanza kuwafundisha.

2:14 Alipokuwa akipita, akamwona Lawi mwana wa Alfayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Yesu akamwambia, "Nifuate!" Lawi akasimama, akamfuata.

2:15 Baadaye, Yesu alikuwa amekaa mezani, nyumbani kwa Lawi, kula chakula. Watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wamemfuata Yesu na wengi wao wakawa wamekaa mezani pamoja naye na wanafunzi wake.

2:16 Basi, baadhi ya walimu wa Sheria ambao walikuwa Mafarisayo walipomwona Yesu akila pamoja na watu wenye dhambi na watoza ushuru, wakawauliza wanafunzi wake, "Kwa nini anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?"

2:17 Yesu alipowasikia, akawaambia, "Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi."

2:18 Wakati mmoja wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo walikuwa wanafunga. Basi, watu wakaja, wakamwuliza Yesu, "Kwa nini wanafunzi wa Yohane na wa Mafarisayo wanafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?"

2:19 Yesu akajibu, "Walioalikwa harusini wanawezaje kufunga kama bwana harusi yupo pamoja nao? Wakati wote wawapo pamoja na bwana harusi hawawezi kufunga.

2:20 Lakini wakati utafika ambapo bwana harusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.

2:21 "Hakuna mtu anayekata kiraka kutoka katika nguo mpya na kukishonea katika nguo kuukuu. Kama akifanya hivyo, hicho kiraka kipya kitararuka kutoka hilo vazi kuukuu, nalo litaharibika zaidi.

2:22 Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu. Kama akifanya hivyo, divai itavipasua hivyo viriba, nayo divai pamoja na hivyo viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya!"

2:23 Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano. Walipokuwa wanatembea, wanafunzi wake wakaanza kukwanyua masuke ya ngano.

2:24 Mafarisayo wakawaambia, "Tazama! Kwa nini wanafanya jambo ambalo si halali kufanya wakati wa Sabato?"

2:25 Yesu akawajibu, "Je, hamjapata kusoma juu ya kile alichofanya Daudi wakati alipohitaji chakula? Yeye pamoja na wenzake waliona njaa,

2:26 naye akaingia ndani ya Nyumba ya Mungu, akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Jambo hili lilifanyika wakati Abiathari alikuwa Kuhani Mkuu. Na ni makuhani tu peke yao waliokuwa wameruhusiwa kula mikate hiyo. Lakini Daudi aliila, tena akawapa na wenzake."

2:27 Basi, Yesu akawaambia, "Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu na si binadamu kwa ajili ya Sabato!

2:28 Kwa hiyo, Mwana wa Mtu ni Bwana hata wa Sabato."

3:1 Yesu aliingia tena katika sunagogi na mle ndani mlikuwa na mtu aliyekuwa na mkono uliopooza.

3:2 Humo baadhi ya watu walimngojea amponye mtu huyo siku ya sabato ili wapate kumshtaki.

3:3 Yesu akamwambia huyo mtu aliyekuwa na mkono uliopooza, "Njoo hapa katikati."

3:4 Kisha, akawauliza, "Je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuua?" Lakini wao hawakusema neno.

3:5 Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia huyo mtu, "Nyosha mkono wako!" Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena.

3:6 Mara Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri pamoja na watu wa kikundi cha Herode jinsi ya kumwangamiza Yesu.

3:7 Yesu aliondoka hapo pamoja na wanafunzi wake, akaenda kando ya ziwa, na umati wa watu ukamfuata. Watu hao walikuwa wametoka Yerusalemu, Yudea,

3:8 Idumea, ng'ambo ya mto Yordani, Tiro na Sidoni. Watu hao wengi walimwendea Yesu kwa sababu ya kusikia mambo mengi aliyokuwa ameyatenda.

3:9 Yesu akawaambia wanafunzi wake wamtayarishie mashua moja, ili umati wa watu usije ukamsonga.

3:10 Alikuwa amewaponya watu wengi, na wagonjwa wote wakawa wanamsonga ili wapate kumgusa.

3:11 Na watu waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu walipomwona, walijitupa chini mbele yake na kupaaza sauti, "Wewe ni Mwana wa Mungu!"

3:12 Lakini Yesu akawaamuru kwa ukali wasimjulishe kwa watu.

3:13 Yesu alipanda kilimani, akawaita wale aliowataka. Basi, wakamwendea,

3:14 naye akawateua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, wakae naye, awatume kuhubiri

3:15 na wawe na mamlaka ya kuwafukuza pepo.

3:16 Basi, hao kumi na wawili walioteuliwa ndio hawa: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina, Petro),

3:17 Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo (Yesu aliwapa hawa ndugu wawili jina Boanerge, maana yake "wanangurumo"),

3:18 Andrea na Filipo, Batholomayo, Mathayo, Thoma, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkanani na

3:19 Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.

3:20 Kisha Yesu alikwenda nyumbani. Umati wa watu ukakusanyika tena, hata Yesu na wafuasi wake wasiweze kupata nafasi ya kula chakula.

3:21 Basi, watu wa jamaa yake walipopata habari hiyo wakatoka kwenda kumchukua maana walikuwa wanasema kwamba amepatwa na wazimu.

3:22 Nao walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu, wakasema, "Ana Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo."

3:23 Hapo Yesu akawaita, akawaambia kwa mifano, "Shetani anawezaje kumfukuza Shetani?

3:24 Ikiwa utawala mmoja umegawanyika makundimakundi yanayopigana, utawala huo hauwezi kudumu.

3:25 Tena, ikiwa jamaa moja imegawanyika makundimakundi yanayopingana, jamaa hiyo itaangamia.

3:26 Ikiwa basi, utawala wa Shetani umegawanyika vikundivikundi hauwezi kudumu, bali utaangamia kabisa.

3:27 "Hakuna mtu awezaye kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang'anya mali yake, isipokuwa kwanza amemfunga huyo mtu mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kumnyang'anya mali yake.

3:28 "Kweli nawaambieni, watu watasamehewa dhambi zao zote na kufuru zao zote;

3:29 lakini anayesema mabaya dhidi ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa kamwe; ana hatia ya dhambi ya milele."

3:30 (Yesu alisema hivyo kwa sababu walikuwa wanasema, "Ana pepo mchafu.")

3:31 Mama yake Yesu na ndugu zake walifika hapo, wakasimama nje, wakampelekea ujumbe kutaka kumwona.

3:32 Umati wa watu ulikuwa umekaa hapo kumzunguka. Basi, wakamwambia, "Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kukuona."

3:33 Yesu akawaambia, "Mama yangu na ndugu zangu ni kina nani?"

3:34 Hapo akawatazama watu waliokuwa wamemzunguka, akasema, "Tazameni! Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.

3:35 Mtu yeyote anayefanya anayotaka Mungu, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama yangu."

4:1 Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa.

4:2 Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia,

4:3 "Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu.

4:4 Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila.

4:5 Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Mbegu hizo ziliota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina.

4:6 Jua lilipochomoza, zikachomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka.

4:7 Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka.

4:8 Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikakua na kuzaa: moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia."

4:9 Kisha akawaambia, "Mwenye masikio na asikie!"

4:10 Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano.

4:11 Naye akawaambia, "Ninyi mmejaliwa kujua siri ya Utawala wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano,

4:12 ili, Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe."

4:13 Basi, Yesu akawauliza, "Je, ninyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote?

4:14 Mpanzi hupanda neno la Mungu.

4:15 Watu wengine ni kama wale walio njiani ambapo mbegu zilianguka. Hawa hulisikia hilo neno lakini mara Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao.

4:16 Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu wanapolisikia hilo neno hulipokea kwa furaha.

4:17 Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno mara wanakata tamaa.

4:18 Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaolisikia hilo neno,

4:19 lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda.

4:20 Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia moja."

4:21 Yesu akaendelea kuwaambia, "Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa pishi au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara.

4:22 Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa.

4:23 Mwenye masikio na asikie!"

4:24 Akawaambia pia, "Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa.

4:25 Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa."

4:26 Yesu akaendelea kusema, "Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani.

4:27 Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika.

4:28 Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke.

4:29 Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika."

4:30 Tena, Yesu akasema, "Tuufananishe Utawala wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani?

4:31 Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote.

4:32 Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake."

4:33 Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia.

4:34 Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.

4:35 Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Tuvuke ziwa, twende ng'ambo."

4:36 Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Palikuwapo pia mashua nyingine hapo.

4:37 Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji.

4:38 Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, "Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?"

4:39 Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, "Kimya! Tulia!" Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa.

4:40 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?"

4:41 Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, "Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?"

5:1 Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ng'ambo ya ziwa.

5:2 Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye.

5:3 Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo.

5:4 Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia.

5:5 Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaaza sauti na kujikatakata kwa mawe.

5:6 Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia

5:7 akisema kwa sauti kubwa, "Una shauri gani nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!"

5:8 (Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, "Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.")

5:9 Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Naye akajibu, "Jina langu ni Jeshi, maana sisi tu wengi."

5:10 Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile.

5:11 Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima.

5:12 Basi, hao pepo wakamsihi, "Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie."

5:13 Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini.

5:14 Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia.

5:15 Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa.

5:16 Watu walishuhudia tukio hilo wakaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe.

5:17 Basi, wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao.

5:18 Yesu alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba amruhusu kwenda naye.

5:19 Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia, "Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma."

5:20 Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa.

5:21 Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa.

5:22 Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi, jina lake Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake,

5:23 akamsihi akisema, "Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi."

5:24 Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande.

5:25 Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili.

5:26 Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya.

5:27 Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake.

5:28 Alifanya hivyo, maana alijisemea, "Nikigusa tu vazi lake, nitapona."

5:29 Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake.

5:30 Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, "Nani aliyegusa mavazi yangu?"

5:31 Wanafunzi wake wakamjibu, "Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona wauliza nani aliyekugusa?"

5:32 Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo.

5:33 Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote.

5:34 Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako."

5:35 Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, "Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?"

5:36 Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, "Usiogope, amini tu."

5:37 Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo.

5:38 Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi.

5:39 Akaingia ndani, akawaambia, "Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu."

5:40 Lakini wao wakamcheka. Basi, akawaondoa wote nje, akawachukua baba na mama ya huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana.

5:41 Kisha akamshika mkono, akamwambia, "Talitha, kumi," maana yake, "Msichana, nakwambia, amka!"

5:42 Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi.

5:43 Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula.

6:1 Yesu aliondoka hapo akaenda katika kijiji chake, akifuatwa na wanafunzi wake.

6:2 Siku ya Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sunagogi. Wengi waliomsikia walishangaa, wakasema, "Je, ameyapata wapi mambo haya? Ni hekima gani hii aliyopewa? Tena, anatendaje maajabu haya anayoyafanya?

6:3 Je, huyu si yule seremala mwana wa Maria, na ndugu yao kina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni; Je, dada zake si wanaishi papa hapa kwetu?" Basi, wakawa na mashaka naye.

6:4 Yesu akawaambia, "Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake, kwa jamaa zake na nyumbani mwake."

6:5 Hakuweza kutenda miujiza hapo, ila aliwawekea mikono wagonjwa wachache, akawaponya.

6:6 Alishangaa sana kwa sababu ya kutoamini kwao. Kisha Yesu alivitembelea vijiji vya pale karibu akiwafundisha watu.

6:7 Aliwaita wale wanafunzi kumi na wawili, akaanza kuwatuma wawiliwawili. Aliwapa uwezo wa kuwatoa pepo wachafu,

6:8 na kuwaamuru, "Msichukue chochote mnapokwenda isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kibindoni.

6:9 Vaeni viatu lakini msivae kanzu mbili."

6:10 Tena aliwaambia, "Popote mtakapokaribishwa nyumbani, kaeni humo mpaka mtakapoondoka mahali hapo.

6:11 Mahali popote ambapo watu watakataa kuwakaribisheni au kuwasikiliza, ondokeni hapo na kuyakung'uta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao."

6:12 Basi, wakaondoka, wakahubiri watu watubu.

6:13 Waliwafukuza pepo wengi wabaya; wakawapaka mafuta wagonjwa wengi, wakawaponya.

6:14 Basi, mfalme Herode alisikia juu ya hayo yote, maana sifa za Yesu zilienea kila mahali. Baadhi ya watu walikuwa wakisema, "Yohane Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake."

6:15 Wengine walisema, "Mtu huyu ni Eliya." Wengine walisema, "Huyu ni nabii kama mmojawapo wa manabii wa kale."

6:16 Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, "Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka."

6:17 Hapo awali Herode mwenyewe alikuwa ameamuru Yohane atiwe nguvuni, akamfunga gerezani. Herode alifanya hivyo kwa sababu ya Herodia ambaye Herode alimwoa ingawaje alikuwa mke wa Filipo, ndugu yake.

6:18 Yohane alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kumchukua mke wa ndugu yako."

6:19 Basi Herodia alimchukia sana Yohane, akataka kumwua, asiweze.

6:20 Herode alimwogopa Yohane kwa maana alijua kwamba yeye ni mtu mwema na mtakatifu, na hivyo akamlinda. Herode alipenda kumsikiliza Yohane, ingawaje baada ya kumsikiliza, alifadhaika sana.

6:21 Ikapatikana nafasi, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode. Herode aliwafanyia karamu wazee wa baraza lake, majemadari na viongozi wa Galilaya.

6:22 Basi, binti yake Herodia aliingia, akacheza, akawafurahisha sana Herode na wageni wake. Mfalme akamwambia huyo msichana, "Niombe chochote utakacho, nami nitakupa."

6:23 Tena akamwapia, "Chochote utakachoniomba, nitakupa: hata ikiwa ni nusu ya ufalme wangu."

6:24 Hapo huyo msichana akatoka, akamwuliza mama yake, "Niombe nini?" Naye akamjibu, "Kichwa cha Yohane mbatizaji."

6:25 Msichana akamrudia mfalme mbio akamwomba, "Nataka unipe sasa hivi katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji."

6:26 Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake, na kwa ajili ya wale wageni wake karamuni, hakutaka kumkatalia.

6:27 Basi, mfalme akamwamuru askari kukileta kichwa cha Yohane. Askari akaenda, akamkata kichwa Yohane mle gerezani,

6:28 akakileta katika sinia, akampa msichana naye msichana akampa mama yake.

6:29 Wanafunzi wa Yohane walipopata habari, walikwenda wakachukua mwili wake, wakauzika kaburini.

6:30 Wale mitume walirudi, wakakusanyika mbele ya Yesu wakamwarifu yote waliyotenda na kufundisha.

6:31 Alisema hivyo kwa kuwa kulikuwa na watu wengi mno walikuwa wanafika hapo na kuondoka hata Yesu na wanafunzi wake hawakuweza kupata nafasi ya kula chakula. Basi, Yesu akawaambia, "Twendeni peke yetu mahali pa faragha kula chakula, mkapumzike kidogo."

6:32 Basi, Wakaondoka peke yao kwa mashua, wakaenda mahali pa faragha.

6:33 Lakini watu wengi waliwaona wakienda, wakawatambua. Hivyo wengi wakatoka katika kila mji, wakakimbilia huko Yesu na wanafunzi wake walikokuwa wanakwenda, wakawatangulia kufika.

6:34 Waliposhuka pwani, Yesu aliona umati mkubwa wa watu, akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Akaanza kuwafundisha mambo mengi.

6:35 Saa za mchana zilikwisha pita. Basi, wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwambia, "Hapa ni nyikani, na sasa kunakuchwa.

6:36 Afadhali uwaage watu waende mashambani na katika vijiji vya jirani, wanunue chakula."

6:37 Lakini Yesu akawaambia, "Wapeni ninyi chakula." Nao wakamwuliza, "Je, twende kununua mikate kwa fedha dinari mia mbili, na kuwapa chakula?"

6:38 Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame." Walipokwisha tazama, wakamwambia, "Kuna mikate mitano na samaki wawili."

6:39 Basi, Yesu akawaamuru wanafunzi wawaketishe watu wote makundimakundi penye nyasi.

6:40 Nao wakaketi makundimakundi ya watu mia moja na ya watu hamsini.

6:41 Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu, akaimega mikate, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Na wale samaki wawili pia akawagawia wote.

6:42 Watu wote wakala, wakashiba.

6:43 Wakaokota mabaki ya mikate na samaki pia, wakajaza vikapu kumi na viwili.

6:44 Nao waliokula hiyo mikate walikuwa wanaume elfu tano.

6:45 Mara Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie kwenda Bethsaida, ng'ambo ya ziwa, wakati yeye anauaga umati wa watu.

6:46 Baada ya kuwaaga watu alikwenda mlimani kusali.

6:47 Ilipokuwa jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, naye alikuwa peke yake katika nchi kavu.

6:48 Basi, akawaona wanafunzi wake wakitaabika kwa kupiga makasia, maana upepo ulikuwa unawapinga. Karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea akitembea juu ya maji. Alitaka kuwapita.

6:49 Lakini walimwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu, wakapiga yowe.

6:50 Maana wote walipomwona waliogopa sana. Mara Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!"

6:51 Kisha akapanda mashuani walimokuwa, na upepo ukatulia. Nao wakashangaa sana.

6:52 maana hawakuwa bado wameelewa maana ya ile mikate. Akili zao zilikuwa bado zimepumbazika.

6:53 Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga.

6:54 Walipotoka mashuani, mara watu wakamtambua Yesu.

6:55 Basi, kwa haraka wakazunguka katika nchi ile yote, wakaanza kuwachukua wagonjwa wamelala juu ya mikeka yao, wakawapeleka kila mahali waliposikia Yesu yupo.

6:56 Kila mahali Yesu alipokwenda, vijijini, mijini, au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa uwanjani, wakamsihi waguse walau pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona.

7:1 Baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu.

7:2 Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa.

7:3 Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo.

7:4 Tena hawali kitu chochote kutoka sokoni mpaka wamekiosha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizopokea kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba.

7:5 Basi, Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, "Mbona wanafunzi wako hawayajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?"

7:6 Yesu akawajibu, "Wanafiki ninyi! Nabii Isaya alitabiri ukweli juu yenu alipoandika: Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno matupu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.

7:7 Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.

7:8 Ninyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu."

7:9 Yesu akaendelea kusema, "Ninyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu.

7:10 Maana Mose aliamuru: Waheshimu baba yako na mama yako, na, Anayemlaani baba au mama, lazima afe.

7:11 Lakini ninyi mwafundisha, Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani ni zawadi kwa Mungu),

7:12 basi, halazimiki tena kuwasaidia wazazi wake.

7:13 Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo."

7:14 Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, "Nisikilizeni nyote, mkaelewe.

7:15 Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu toka nje ambacho chaweza kumtia mtu najisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu najisi."

7:16 Mwenye masikio na asikie!

7:17 Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano.

7:18 Naye akawaambia, "Je, hata ninyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu toka nje hakiwezi kumtia unajisi,

7:19 kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?" (Kwa kusema hivyo, Yesu alivihalalisha vyakula vyote.)

7:20 Akaendelea kusema, "Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia najisi.

7:21 Kwa maana kutoka ndani, katika moyo wa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji,

7:22 uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu.

7:23 Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu najisi."

7:24 Yesu aliondoka hapo, akaenda hadi wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha.

7:25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake.

7:26 Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu.

7:27 Yesu akamwambia, "Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa."

7:28 Lakini huyo mama akasema, "Sawa, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto."

7:29 Yesu akamwambia, "Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!"

7:30 Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.

7:31 Kisha Yesu aliondoka wilayani Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli.

7:32 Basi, wakamletea bubu-kiziwi, wakamwomba amwekee mikono.

7:33 Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi.

7:34 Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, "Efatha," maana yake, "Funguka."

7:35 Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa.

7:36 Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo.

7:37 Watu walishangaa sana, wakasema, "Amefanya yote vyema: amewajalia viziwi kusikia, na bubu kusema!"

8:1 Wakati huo umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia,

8:2 "Nawahurumia watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu, wala hawana chakula.

8:3 Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali."

8:4 Wanafunzi wake wakamwuliza, "Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?"

8:5 Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Nao wakamjibu, "Saba."

8:6 Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia.

8:7 Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile.

8:8 Watu wakala, wakashiba. Wakaokota mabaki yaliyosalia wakajaza makapu saba.

8:9 Nao waliokula walikuwa watu wapatao elfu nne. Yesu akawaaga,

8:10 na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha.

8:11 Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka awafanyie ishara kuonyesha anayo idhini kutoka mbinguni.

8:12 Yesu akahuzunika rohoni, akasema, "Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote!"

8:13 Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.

8:14 Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua.

8:15 Yesu akawaonya, "Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode."

8:16 Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, "Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate."

8:17 Yesu alitambua hayo, akawaambia, "Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu imeshupaa?

8:18 Je, Mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki

8:19 wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu elfu tano? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki ya makombo?" Wakamjibu, "Kumi na viwili."

8:20 "Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu elfu nne, mlikusanya makapu mangapi ya makombo?" Wakamjibu, "Saba."

8:21 Basi, akawaambia, "Na bado hamjaelewa?"

8:22 Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu mmoja, wakamwomba amguse.

8:23 Yesu akamshika mkono huyo kipofu, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, "Je, unaweza kuona kitu?"

8:24 Huyo kipofu akatazama, akasema, "Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea."

8:25 Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa.

8:26 Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, "Usirudi kijijini!"

8:27 Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema mimi ni nani?"

8:28 Wakamjibu, "Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Eliya na wengine mmojawapo wa manabii."

8:29 Naye akawauliza, "Na ninyi je, mnasema mimi ni nani?" Petro akamjibu, "Wewe ndiwe Kristo."

8:30 Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.

8:31 Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake: "Ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Atauawa na baada ya siku tatu atafufuka."

8:32 Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Basi, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea.

8:33 Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, "Ondoka mbele yangu, Shetani! Fikira zako si za kimungu ila ni za kibinadamu!"

8:34 Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, "Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.

8:35 Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa.

8:36 Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake?

8:37 Ama mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake?

8:38 Mtu yeyote katika kizazi hiki kiovu na kisichomjali Mungu anayenionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu."

9:1 Yesu akaendelea kuwaambia, "Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa enzi."

9:2 Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao,

9:3 mavazi yake yakang'aa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe.

9:4 Eliya na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu.

9:5 Petro akamwambia Yesu, "Mwalimu, ni vizuri sana kwamba tuko hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya."

9:6 Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema.

9:7 Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, "Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni."

9:8 Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao.

9:9 Walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka wafu.

9:10 Basi, wakashika agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana wao kwa wao maana ya kufufuka kutoka wafu.

9:11 Wakamwuliza Yesu, "Mbona walimu wa Sheria wanasema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?"

9:12 Naye akawajibu, "Naam, Eliya anakuja kwanza kutayarisha yote. Hata hivyo, kwa nini basi imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Mwana wa Mtu atapatwa na mateso mengi na kudharauliwa?

9:13 Lakini nawaambieni, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyotaka kama ilivyoandikwa juu yake."

9:14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliona umati mkubwa wa watu hapo. Na baadhi ya walimu wa Sheria walikuwa wanajadiliana nao.

9:15 Mara tu ule umati wa watu ulipomwona, wote walishangaa sana, wakamkimbilia wamsalimu.

9:16 Yesu akawauliza, "Mnajadiliana nini nao?"

9:17 Hapo mtu mmoja katika ule umati wa watu akamjibu, "Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo aliyemfanya kuwa bubu.

9:18 Kila mara anapomvamia, humwangusha chini na kumfanya atokwe na povu kinywani, akisaga meno na kuwa mkavu mwili wote. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo lakini hawakuweza."

9:19 Yesu akawaambia, "Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu."

9:20 Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto,

9:21 "Amepatwa na mambo hayo tangu lini?" Naye akamjibu, "Tangu utoto wake.

9:22 Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!"

9:23 Yesu akamwambia, "Eti ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani."

9:24 Hapo, huyo baba akalia kwa sauti, "Naamini! Lakini imani yangu haitoshi, nisaidie!"

9:25 Yesu alipouona umati wa watu unaongezeka upesi mbele yake, alimkemea yule pepo mchafu, "Pepo unayemfanya huyu mtoto kuwa bubu-kiziwi, nakuamuru, mtoke mtoto huyu wala usimwingie tena!"

9:26 Hapo huyo pepo alipaaza sauti, akamwangusha huyo mtoto chini, kisha akamtoka. Mtoto alionekana kama maiti, hata wengine walisema, "Amekufa!"

9:27 Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.

9:28 Yesu alipoingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, "Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?"

9:29 Naye akawaambia, "Pepo wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala tu."

9:30 Yesu na wanafunzi wake waliondoka hapo, wakaendelea na safari kupitia wilaya ya Galilaya. Yesu hakupenda watu wajue alipokuwa,

9:31 kwa sababu alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Aliwaambia, "Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu ambao watamuua; lakini siku ya tatu baada ya kuuawa atafufuka."

9:32 Wanafunzi hawakufahamu jambo hilo. Wakaogopa kumwuliza.

9:33 Basi, walifika Kafarnaumu. Na alipokuwa nyumbani, aliwauliza, "Mlikuwa mnajadiliana nini njiani?"

9:34 Lakini wao wakanyamaza, maana njiani walikuwa wamebishana ni nani aliye mkuu kati yao.

9:35 Yesu akaketi chini, akawaita wale kumi na wawili, akawaambia, "Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza lazima awe wa mwisho na kuwa mtumishi wa wote."

9:36 Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kati yao, akamku mbatia, halafu akawaambia,

9:37 "Anayempokea mtoto kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, hanipokei mimi tu, bali anampokea yule aliyenituma."

9:38 Yohane akamwambia, "Mwalimu, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako, nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu."

9:39 Lakini Yesu akasema, "Msimkataze, maana hakuna mtu anayefanya muujiza kwa jina langu, na papo hapo akaweza kusema mabaya juu yangu.

9:40 Maana, asiyepingana nasi, yuko upande wetu.

9:41 Mtu yeyote atakeyewapeni kikombe cha maji ya kunywa kwa sababu ninyi ni watu wake Kristo, hakika hatakosa kupata tuzo lake.

9:42 "Mtu yeyote atakayemfanya mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini atende dhambi, ingekuwa afadhali kwa mtu huyo kufungiwa shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutupwa baharini.

9:43 Mkono wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia kwenye uzima bila mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda katika moto wa Jehanamu.

9:44 Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.

9:45 Na mguu wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uzima bila mguu mmoja, kuliko kuwa na miguu yote miwili na kutupwa katika moto wa Jehanamu.

9:46 Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.

9:47 Na jicho lako likikukosesha, ling'oe! Afadhali kuingia katika utawala wa Mungu ukiwa na jicho moja tu, kuliko kuwa na macho yako yote mawili na kutupwa katika moto wa Jehanamu.

9:48 Humo wadudu wake hawafi, na moto hauzimiki.

9:49 "Maana kila mmoja atakolezwa kwa moto.

9:50 Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? Muwe na chumvi ndani yenu na kudumisha amani kati yenu."

10:1 Yesu alitoka hapo akaenda mkoani Yudea na hata ng'ambo ya mto Yordani. Umati wa watu ukamwendea tena, naye akawafundisha tena kama ilivyokuwa desturi yake.

10:2 Basi, Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, "Je, ni halali mtu kumpa talaka mkewe?"

10:3 Yesu akawajibu, "Mose aliwapa maagizo gani?"

10:4 Nao wakasema, "Mose aliagiza mume kumpatia mkewe hati ya talaka na kumwacha."

10:5 Yesu akawaambia, "Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.

10:6 Lakini tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke.

10:7 Hivyo mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe,

10:8 nao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja.

10:9 Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe."

10:10 Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo.

10:11 Naye akawaambia, "Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe.

10:12 Na mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini."

10:13 Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea.

10:14 Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa.

10:15 Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia katika Ufalme huo."

10:16 Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki.

10:17 Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, "Mwalimu mwema, nifanyeje ili niupate uzima wa milele?"

10:18 Yesu akamjibu, "Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.

10:19 Unazijua amri: Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Usidanganye; Waheshimu baba na mama yako."

10:20 Naye akamjibu, "Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu."

10:21 Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia, "Umepungukiwa na kitu kimoja: nenda ukauze vitu ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate."

10:22 Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi.

10:23 Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, "Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!"

10:24 Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, "Watoto wangu, ni vigumu sana kuingia katika Ufalme wa Mungu!

10:25 Ni rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu."

10:26 Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, "Ni nani basi, atakayeweza kuokoka?"

10:27 Yesu akawatazama, akawaambia, "Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana."

10:28 Petro akamwambia, "Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata!"

10:29 Yesu akasema, "Kweli nawaambieni, kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au mama, au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema,

10:30 atapokea mara mia zaidi wakati huu wa sasa nyumba, ndugu, dada, mama, watoto na mashamba pamoja na mateso; na katika wakati ujao atapokea uzima wa milele.

10:31 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza."

10:32 Basi, walikuwa njiani kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata:

10:33 "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa.

10:34 Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumwua. Na baada ya siku tatu atafufuka."

10:35 Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, "Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba."

10:36 Yesu akawauliza, "Mnataka niwafanyie nini?"

10:37 Wakamjibu, "Uturuhusu tuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wa Ufalme wako."

10:38 Yesu akawaambia, "Hamjui mnachoomba! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?"

10:39 Wakamjibu, "Tunaweza." Yesu akawaambia, "Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa.

10:40 Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga, bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa."

10:41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane.

10:42 Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao.

10:43 Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu, sharti awe mtumishi wenu.

10:44 Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote.

10:45 Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila alikuja kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi."

10:46 Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mwombaji aitwaye Bartimayo mwana wa Timayo alikuwa ameketi kando ya barabara.

10:47 Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaaza sauti, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!"

10:48 Watu wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaaza sauti, "Mwana wa Daudi, nihurumie!"

10:49 Yesu alisimama, akasema, "Mwiteni." Basi, wakamwita huyo kipofu, wakamwambia, "Jipe moyo! Simama, anakuita."

10:50 Naye akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu.

10:51 Yesu akamwuliza, "Unataka nikufanyie nini?" Huyo kipofu akamwambia, "Mwalimu, naomba nipate kuona."

10:52 Yesu akamwambia, "Nenda, imani yako imekuponya." Mara huyo kipofu akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani.

11:1 Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake,

11:2 akawaambia, "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwana punda amefungwa ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete.

11:3 Kama mtu akiwauliza, Mbona mnafanya hivyo? Mwambieni, Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara."

11:4 Basi, wakaenda, wakamkuta mwana punda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua,

11:5 baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza "Kwa nini mnamfungua huyo mwana punda?"

11:6 Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao.

11:7 Wakampelekea Yesu huyo mwana punda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwana punda, na Yesu akaketi juu yake.

11:8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani.

11:9 Watu wote waliotangulia na wale waliofuata wakapaaza sauti zao wakisema, "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana!

11:10 Ubarikiwe Ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni!"

11:11 Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka Hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.

11:12 Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa.

11:13 Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila majani matupu, kwa vile hayakuwa majira ya mtini kuzaa matunda.

11:14 Hapo akauambia mtini, "Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako." Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo.

11:15 Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia Hekaluni, akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.

11:16 Hakumruhusu mtu yeyote kupitia Hekaluni akichukua kitu.

11:17 Kisha akawafundisha, "Imeandikwa: Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote! Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi!"

11:18 Makuhani wakuu na walimu wa Sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake.

11:19 Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini.

11:20 Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi.

11:21 Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, "Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!"

11:22 Yesu akawaambia, "Mwaminini Mungu.

11:23 Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: Ng'oka ukajitose baharini bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo.

11:24 Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa.

11:25 Mnaposimama kusali, sameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu.

11:26 Lakini msipowasamehe wengine, hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu."

11:27 Basi, wakafika tena Yerusalemu. Yesu alipokuwa akitembea Hekaluni, makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee walimwendea,

11:28 wakamwuliza, "Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?"

11:29 Lakini Yesu akawaambia, "Nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, na pia nitawaambieni ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.

11:30 Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka mbinguni ama kwa watu? Nijibuni."

11:31 Wakaanza kujadiliana, "Tukisema, Yalitoka mbinguni, atatuuliza, Basi, mbona hamkumsadiki?

11:32 Na tukisema, Yalitoka kwa watu..." (Waliogopa umati wa watu maana wote waliamini kwamba Yohane alikuwa kweli nabii.)

11:33 Basi, wakamjibu Yesu, "Sisi hatujui." Naye Yesu akawaambia, "Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani."

12:1 Yesu alianza kusema nao kwa mifano: "Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu. Akalizungushia ukuta, na katikati yake akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga mnara pia. Akalikodisha shamba hilo kwa wakulima, akasafiri hadi nchi ya mbali.

12:2 Wakati wa mavuno, alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima akamletee sehemu ya mazao ya shamba lake.

12:3 Wale wakulima wakamkamata, wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu.

12:4 Akatuma tena mtumishi mwingine; huyu wakamuumiza kichwa na kumtendea vibaya.

12:5 Mwenye shamba akatuma mtumishi mwingine tena, na huyo wakamuua. Wengine wengi waliotumwa, baadhi yao walipigwa, na wengi wakauawa.

12:6 Alibakiwa bado na mtu mmoja, yaani mwanawe mpendwa. Mwishowe akamtuma huyo akisema, Watamheshimu mwanangu.

12:7 Lakini hao wakulima wakaambiana, Huyu ndiye mrithi, basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu!

12:8 Kwa hiyo wakamkamata, wakamuua na kumtupa nje ya lile shamba la mizabibu.

12:9 "Basi, mwenye shamba atafanya nini? Atakuja kuwaangamiza hao wakulima na kulikodisha hilo shamba la mizabibu kwa watu wengine.

12:10 Je, hamjasoma Maandiko haya? Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.

12:11 Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu."

12:12 Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee walifahamu ya kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu. Kwa hiyo walijaribu kumtia nguvuni, lakini waliogopa umati wa watu. Basi, wakamwacha wakaenda zao.

12:13 Basi, baadhi ya Mafarisayo na wafuasi wa kikundi cha Herode walitumwa ili wamtege Yesu kwa maneno yake.

12:14 Wakamwendea, wakamwambia, "Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu unayesema ukweli mtupu, wala humjali mtu yeyote. Wala cheo cha mtu si kitu kwako, lakini wafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la? Tulipe au tusilipe?"

12:15 Lakini Yesu alijua unafiki wao, akawaambia, "Mbona mnanijaribu? Nionyesheni sarafu."

12:16 Wakamwonyesha. Naye akawauliza, "Sura na chapa hii ni ya nani?" Wakamjibu, "Ni ya Kaisari."

12:17 Basi, Yesu akawaambia, "Mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari na Mungu yaliyo yake Mungu." Wakashangazwa sana naye.

12:18 Masadukayo wasemao kwamba hakuna ufufuo walimwendea Yesu, wakamwuliza,

12:19 "Mwalimu, Mose alituagiza hivi: Mtu akifa na kuacha mke bila mtoto, ndugu yake lazima amchukue huyo mama mjane amzalie watoto ndugu yake marehemu.

12:20 Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa, akafa bila kuacha mtoto.

12:21 Ndugu wa pili akamwoa huyo mjane, naye pia akafa bila kuacha mtoto; na ndugu watatu hali kadhalika.

12:22 Wote saba walikufa bila kuacha mtoto. Mwishowe yule mama mjane naye akafa.

12:23 Basi, siku watu watakapofufuka, mama huyo atakuwa mke wa nani? Maana wote saba walikuwa wamemwoa."

12:24 Yesu akawaambia, "Ninyi mmekosea sana, kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu.

12:25 Maana wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika wa mbinguni.

12:26 Lakini kuhusu kufufuliwa kwa wafu, je, hamjasoma kitabu cha Mose katika sehemu inayohusu kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto? Mungu alimwambia Mose, Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.

12:27 Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Ninyi mmekosea sana!"

12:28 Mmojawapo wa walimu wa Sheria alifika, akasikia mabishano yao. Alipoona kwamba Yesu aliwajibu vyema, akajitokeza akamwuliza, "Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?"

12:29 Yesu akamjibu, "Ya kwanza ndiyo hii: Sikiliza, Israeli! Bwana Mungu wetu ndiye peke yake Bwana.

12:30 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote.

12:31 Na ya pili ndiyo hii: Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi."

12:32 Basi, yule mwalimu wa Sheria akamwambia, "Vyema Mwalimu! Umesema kweli kwamba Mungu ni mmoja tu wala hakuna mwingine ila yeye.

12:33 Na ni lazima mtu kumpenda Mungu kwa moyo wote, kwa akili yote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani yake kama anavyojipenda mwenyewe. Jambo hili ni muhimu zaidi kuliko dhabihu na sadaka zote za kuteketezwa."

12:34 Yesu alipoona kwamba huyu mtu alimjibu kwa ujasiri, akamwambia, "Wewe huko mbali na Ufalme wa Mungu." Baada ya hayo, hakuna mtu aliyethubutu tena kumwuliza kitu.

12:35 Wakati Yesu alipokuwa akifundisha Hekaluni, aliuliza, "Mbona walimu wa Sheria wanasema ya kwamba Kristo ni mwana wa Daudi?

12:36 Daudi mwenyewe akiongozwa na Roho Mtakatifu alisema: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, Mpaka nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako."

12:37 "Daudi mwenyewe anamwita Kristo Bwana. Basi, Kristo atakuwaje mwanae?" Umati wa watu ulikuwa ukimsikiliza kwa furaha.

12:38 Katika mafundisho yake, Yesu alisema, "Jihadharini na walimu wa Sheria ambao hupenda kupitapita wamejivalia kanzu ndefu na kusalimiwa na watu kwa heshima sokoni; hupenda kuketi mahali pa heshima katika masunagogi,

12:39 na kuchukua nafasi za heshima katika karamu.

12:40 Huwanyonya wajane huku wakijisingizia kusali sala ndefu. Siku ya hukumu watapata adhabu kali!"

12:41 Yesu alikuwa ameketi karibu na sanduku la hazina. Akawa anatazama jinsi watu wengi walivyokuwa wakitoa fedha na kuzitia katika hazina ya Hekalu. Matajiri wengi walitoa fedha nyingi.

12:42 Hapo akaja mama mmoja mjane maskini, akatoa sarafu mbili ndogo za fedha.

12:43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, "Kweli nawaambieni, huyu mama mjane maskini ametoa zaidi kuliko wengine wote waliotia fedha katika sanduku la hazina.

12:44 Maana wote walitoa kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa yote aliyokuwa nayo, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi."

13:1 Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!"

13:2 Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa."

13:3 Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha,

13:4 "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?"

13:5 Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.

13:6 Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, Mimi ndiye! nao watawapotosha watu wengi.

13:7 Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado.

13:8 Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto.

13:9 "Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao.

13:10 Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote.

13:11 Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu.

13:12 Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.

13:13 Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.

13:14 "Mtakapoona Chukizo Haribifu limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani.

13:15 Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu.

13:16 Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.

13:17 Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!

13:18 Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi.

13:19 Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena.

13:20 Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo.

13:21 "Basi mtu akiwaambieni, Tazama, Kristo yupo hapa! au Yupo pale! msimsadiki.

13:22 Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana.

13:23 Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea.

13:24 "Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza.

13:25 Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.

13:26 Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu.

13:27 Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.

13:28 "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.

13:29 Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana.

13:30 Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.

13:31 Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

13:32 "Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.

13:33 Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini.

13:34 Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho.

13:35 Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi.

13:36 Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala.

13:37 Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!"

14:1 Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Makuhani wakuu na walimu wa Sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue.

14:2 Lakini walisema, "Tusimtie nguvuni wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia."

14:3 Yesu alikuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, Mkoma. Alipokuwa mezani kula chakula, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya nardo safi ya thamani kubwa alikuja, akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu marashi hayo kichwani.

14:4 Baadhi ya watu waliokuwa hapo walikasirika wakajisemea, "Kwa nini kupoteza ovyo marashi haya?

14:5 Yangaliweza kuuzwa kwa fedha kiasi cha denari mia tatu, wakapewa maskini!" Wakamkemea huyo mama.

14:6 Lakini Yesu akawaambia, "Mwacheni; kwa nini mnamsumbua? Amenitendea jambo jema.

14:7 Maskini mnao daima pamoja nanyi; mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima.

14:8 Yeye amefanya alivyoweza; ameupaka mwili wangu marashi kuutayarisha kwa maziko.

14:9 Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni Habari Njema itakapohubiriwa, kitendo hiki alichofanya kitatajwa kwa ajili ya kumkumbuka."

14:10 Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, alienda kwa makuhani wakuu ili kumsaliti Yesu.

14:11 Makuhani wakuu waliposikia habari hiyo, walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Basi, Yuda akaanza kutafuta nafasi ya kumsaliti Yesu.

14:12 Siku ya kwanza ya sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wakati ambapo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza, "Wataka tukuandalie wapi karamu ya Pasaka?"

14:13 Basi Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akiwaambia, "Nendeni mjini, nanyi mtakutana na mtu anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni

14:14 mpaka katika nyumba atakayoingia, mkamwambie mwenye nyumba, Mwalimu anasema: wapi chumba changu ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?

14:15 Naye atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani kilichotayarishwa na kupambwa. Tuandalieni humo."

14:16 Wanafunzi wakaondoka, wakaenda mjini, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Wakaandaa karamu ya Pasaka.

14:17 Ilipokuwa jioni, Yesu alifika pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.

14:18 Walipokuwa mezani wakila, Yesu alisema, "Kweli nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti."

14:19 Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, "Je, ni mimi?"

14:20 Yesu akawaambia, "Ni mmoja wenu ninyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli.

14:21 Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!"

14:22 Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, "Twaeni; huu ni mwili wangu."

14:23 Kisha akatwaa kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa; nao wote wakanywa katika kikombe hicho.

14:24 Akawaambia, "Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi.

14:25 Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika Ufalme wa Mungu."

14:26 Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.

14:27 Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Ninyi nyote mtakuwa na mashaka nami; maana Maandiko Matakatifu yasema: Nitampiga mchungaji nao kondoo watatawanyika.

14:28 Lakini nikisha fufuka, nitawatangulieni kule Galilaya."

14:29 Petro akamwambia "Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakukana kamwe!"

14:30 Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu."

14:31 Lakini Petro akasisitiza, "Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakuacha kamwe." Wanafunzi wote pia wakasema vivyo hivyo.

14:32 Basi, wakafika katika bustani iitwayo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kaeni hapa wakati mimi nasali."

14:33 Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.

14:34 Akawaambia, "Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe."

14:35 Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi, akasali kwamba, kama ingewezekana, asiipitie saa hiyo ya mateso.

14:36 Akasema, "Baba yangu, kwako mambo yote yanawezekana. Uniondolee kikombe hiki; lakini isiwe kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe."

14:37 Kisha akarudi kwa wanafunzi wale watatu, akawakuta wamelala. Basi, akamwuliza Petro, "Simoni, je umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?"

14:38 Kisha akawaambia, "Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu."

14:39 Akaenda kusali tena akirudia maneno yaleyale.

14:40 Kisha akarudi tena, akawakuta wamelala. Macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Hawakujua la kumjibu.

14:41 Alipowajia mara ya tatu aliwaambia, "Mnalala bado na kupumzika? Sasa imetosha! Saa imefika! Mwana wa Mtu anakabidhiwa kwa watu waovu.

14:42 Amkeni, twendeni zetu. Tazameni, yule atakayenisaliti amekaribia."

14:43 Yesu alipokuwa bado anasema, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee.

14:44 Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: "Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni, mkampeleke chini ya ulinzi."

14:45 Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akasema, "Mwalimu!" Kisha akambusu.

14:46 Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.

14:47 Mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja na Yesu akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

14:48 Yesu akawaambia, "Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi?

14:49 Kila siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini sasa lazima Maandiko Matakatifu yatimie."

14:50 Hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.

14:51 Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anamfuata Yesu akiwa amevaa shuka. Nao wakajaribu kumkamata.

14:52 Lakini yeye akaponyoka, akaiachilia ile shuka, akakimbia uchi.

14:53 Basi, wakampeleka Yesu kwa Kuhani Mkuu ambapo makuhani wakuu wote, wazee na walimu wa Sheria walikuwa wamekutanika.

14:54 Petro alimfuata Yesu kwa mbali, akaingia ndani ya ya wa Kuhani Mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto.

14:55 Makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu wapate kumwua, lakini hawakupata.

14:56 Watu wengi walitoa ushahidi wa uongo juu ya Yesu, lakini ushahidi wao haukupatana.

14:57 Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uongo wakisema:

14:58 "Tulimsikia mtu huyu akisema, Nitaliharibu Hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine lisilojengwa kwa mikono."

14:59 Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukupatana.

14:60 Basi, Kuhani Mkuu akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu, "Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?"

14:61 Lakini yeye akakaa kimya; hakusema hata neno moja. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, "Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Mtukufu?"

14:62 Yesu akajibu, "Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa Mwenyezi, akija katika mawingu ya mbinguni."

14:63 Hapo Kuhani Mkuu akararua joho lake, akasema, "Tuna haja gani tena ya mashahidi?

14:64 Mmesikia kufuru yake! Ninyi mwaonaje?" Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa.

14:65 Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, "Bashiri ni nani aliyekupiga!" Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi.

14:66 Petro alipokuwa bado chini ukumbini, mmoja wa wajakazi wa kuhani Mkuu alikuja.

14:67 Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, "Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti."

14:68 Lakini Petro akakana, "Sijui, wala sielewi unayosema!" Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika.

14:69 Yule mjakazi alipomwona tena Petro, akaanza tena kuwaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, "Mtu huyu ni mmoja wao."

14:70 Petro akakana tena. Baadaye kidogo, watu waliokuwa wamesimama hapo wakamwambia Petro, "Hakika wewe ni mmoja wao, maana wewe ni Mgalilaya."

14:71 Lakini Petro akaanza kulaani na kuapa akisema, "Mimi simjui mtu huyu mnayesema habari zake."

14:72 Hapo jogoo akawika mara ya pili. Basi, Petro akakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa amemwambia: "Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu." Petro akabubujika machozi.

15:1 Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja na wazee, walimu wa Sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato.

15:2 Pilato akamwuliza Yesu, "Je, wewe ni mfalme wa Wayahudi?" Yesu akajibu, "Wewe umesema."

15:3 Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi.

15:4 Pilato akamwuliza tena Yesu, "Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi juu yako."

15:5 Lakini Yesu hakujibu neno, hata pilato akashangaa.

15:6 Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka.

15:7 Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji.

15:8 Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake.

15:9 Pilato akawauliza, "Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?"

15:10 Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu.

15:11 Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba.

15:12 Pilato akawauliza tena, "Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?"

15:13 Watu wote wakapaaza sauti tena: "Msulubishe!"

15:14 Lakini Pilato akawauliza, "Kwa nini! Amefanya kosa gani?" Lakini wao wakazidi kupaaza sauti, "Msulubishe!"

15:15 Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe.

15:16 Kisha askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima cha askari.

15:17 Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea kichwani.

15:18 Wakaanza kumsalimu, "Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!"

15:19 Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na kumsujudia.

15:20 Baada ya kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.

15:21 Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene. Yeye alikuwa baba wa Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani. Basi, wakamlazimisha auchukue msalaba wa Yesu.

15:22 Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la Kichwa."

15:23 Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye akaikataa.

15:24 Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini.

15:25 Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha.

15:26 Na mshtaka wake ulikuwa umeandikwa: "Mfalme wa Wayahudi."

15:27 Pamoja naye waliwasulubisha wanyang'anyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto.

15:28 Hapo yakatimia Maandiko Matakatifu yanayosema, "Aliwekwa kundi moja na waovu."

15:29 Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, "Aha! Wewe mwenye kuvunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu!

15:30 Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!"

15:31 Nao makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria walimdhihaki wakisema, "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi!

15:32 Eti yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke msalabani ili tuone na kuamini." Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana.

15:33 Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa kulikuwa giza nchini kote.

15:34 Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eloi, Eloi, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?"

15:35 Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, "Sikiliza! Anamwita Eliya!"

15:36 Mtu mmoja akakimbia, akachovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, "Hebu tuone kama Eliya atakuja kumteremsha msalabani!"

15:37 Yesu akapaaza sauti kubwa, akakata roho.

15:38 Basi, pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini.

15:39 Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake aliona jinsi Yesu alivyolia kwa sauti na kukata roho, akasema, "Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!"

15:40 Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria toka mji wa Magdala, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose.

15:41 Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye.

15:42 Wakati wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku inayotangulia Sabato.

15:43 Hapo akaja Yosefu mwenyeji wa Armathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana. Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato bila uoga, akaomba apewe mwili wa Yesu.

15:44 Pilato alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari, akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo.

15:45 Pilato alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu Yosefu auchukue mwili wake.

15:46 Hapo Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango.

15:47 Nao Maria Magdalene na Maria mama yake Yose walipaona hapo alipolazwa.

16:1 Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalene, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.

16:2 Basi, alfajiri na mapema siku ya Jumapili, jua lilipoanza kuchomoza, walienda kaburini.

16:3 Nao wakawa wanaambiana, "Nani atakayetuondolea lile jiwe mlangoni mwa kaburi?"

16:4 Lakini walipotazama, waliona jiwe limekwisha ondolewa. (Nalo lilikuwa kubwa mno.)

16:5 Walipoingia kaburini, walimwona kijana mmoja aliyevaa vazi jeupe, ameketi upande wa kulia; wakashangaa sana.

16:6 Lakini huyo kijana akawaambia, "Msishangae. Mnamtafuta Yesu wa Nazareti aliyesulubiwa. Amefufuka, hayumo hapa. Tazameni mahali walipokuwa wamemlaza.

16:7 Nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro ya kwamba anawatangulieni kule Galilaya. Huko mtamwona kama alivyowaambieni."

16:8 Basi, wakatoka pale kaburini mbio, maana walitetemeka kwa hofu na kushangaa. Hawakumwambia mtu yeyote kitu, kwa sababu waliogopa mno.

16:9 Yesu alipofufuka mapema Jumapili, alijionyesha kwanza kwa Maria Magdalene, ambaye Yesu alikuwa amemtoa pepo saba.

16:10 Maria Magdalene akaenda, akawajulisha wale waliokuwa pamoja na Yesu, na wakati huo walikuwa wanaomboleza na kulia.

16:11 Lakini waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalene amemwona, hawakuamini.

16:12 Baadaye Yesu aliwatokea wanafunzi wawili akiwa na sura nyingine. Wanafunzi hao walikuwa wanakwenda shambani.

16:13 Nao pia wakaenda wakawaambia wenzao. Hata hivyo hawakuamini.

16:14 Mwishowe, Yesu aliwatokea wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa pamoja mezani. Akawakemea sana kwa sababu ya kutoamini kwao na ukaidi wao, maana hawakuwaamini wale waliokuwa wamemwona baada ya kufufuka.

16:15 Basi, akawaambia, "Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu.

16:16 Anayeamini na kubatizwa ataokolewa; asiyeamini atahukumiwa.

16:17 Na ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: kwa jina langu watatoa pepo na watasema kwa lugha mpya.

16:18 Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawawekea wagonjwa mikono, nao watapona."

16:19 Basi, Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia wa Mungu.

16:20 Wanafunzi wakaenda wakihubiri kila mahali. Bwana akafanya kazi pamoja nao na kuimarisha ujumbe huo kwa ishara zilizoandamana nao.


Next: Luke