Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: 2 Corinthians

1:1 Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya.

1:2 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

1:3 Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote.

1:4 Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.

1:5 Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye.

1:6 Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji ninyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi.

1:7 Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu.

1:8 Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi.

1:9 Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe.

1:10 Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena,

1:11 ninyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu.

1:12 Sisi tunajivunia kitu kimoja: dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali neema ya Mungu.

1:13 Tunawaandikia ninyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa,

1:14 maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile Siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea ninyi fahari.

1:15 Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu.

1:16 Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia, na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea.

1:17 Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema "Ndiyo" na "Siyo" papo hapo?

1:18 Mungu ni ukweli mtupu; basi, kile tulichowaambia ninyi si jambo la "Ndiyo" na "Siyo".

1:19 Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa "Ndiyo" na "Siyo"; bali yeye daima ni "Ndiyo" ya Mungu.

1:20 Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa "Ndiyo". Kwa sababu hiyo, "Amina" yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu.

1:21 Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu;

1:22 ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.

1:23 Mungu ndiye shahidi wangu--yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho, kwa sababu tu ya kuwahurumieni.

1:24 Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; ninyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.

2:1 Basi nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni.

2:2 Maana nikiwahuzunisha ninyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha!

2:3 Ndiyo maana niliwaandikia--sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na ninyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba, mimi nikifurahi, ninyi nyote pia mnafurahi.

2:4 Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha ninyi, bali kwa ajili ya kuwaonyesheni kwamba nawapenda mno.

2:5 Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi--ila amewahuzunisha ninyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi.

2:6 Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha.

2:7 Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa.

2:8 Kwa hiyo nawasihi: mwonyesheni kwamba mnampenda.

2:9 Madhumuni yangu kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo.

2:10 Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe--kama kweli ninacho cha kusamehe--nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,

2:11 ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo.

2:12 Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana.

2:13 Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia.

2:14 Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali.

2:15 Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote wanaookolewa na wanaopotea.

2:16 Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo?

2:17 Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.

3:1 Je, tunaanza tena kujipendekeza? Je, tunahitaji barua ya utambulisho kwenu, au kutoka kwenu, kama watu wengine?

3:2 Ninyi wenyewe ni barua yetu; barua iliyoandikwa mioyoni mwetu kila mtu aione na kuisoma.

3:3 Ni dhahiri kwamba ninyi ni barua ya Kristo aliyoipeleka kwa mikono yetu. Barua yenyewe imeandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu hai; imeandikwa si juu ya kipande cha jiwe, bali juu ya mioyo ya watu.

3:4 Tunaweza kusema hayo kwa sababu ya tumaini letu tulilo nalo kwa Mungu kwa njia ya Kristo.

3:5 Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu:

3:6 maana yeye ndiye aliyetuwezesha kulihudumia Agano Jipya ambalo si agano la sheria iliyoandikwa, bali Agano la Roho. Maana sheria iliyoandikwa huleta kifo, lakini Roho huleta uzima.

3:7 Sheria iliwekwa kwa kuandikwa juu ya vipande vya mawe. Ingawaje mwisho wake umekuwa kifo, utukufu wake ulikuwa mkuu mno hata wana wa Israeli wasiweze kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya mng'ao wake. Tena mng'ao huo ulikuwa wa muda tu. Basi, ikiwa huduma ya kile ambacho kimesababisha kifo imefanyika kwa utukufu mwingi kiasi hicho,

3:8 basi, huduma ya Roho ina utukufu mkuu zaidi.

3:9 Ikiwa basi, kulikuwa na utukufu katika huduma ile iliyoleta hukumu, ni wazi kwamba huduma ile iletayo kukubaliwa kuwa waadilifu itakuwa na utukufu mkuu zaidi.

3:10 Sasa utukufu mkuu zaidi umechukua nafasi ya ule utukufu uliokuja hapo awali, ambao fahari yake imekwisha toweka.

3:11 Maana ikiwa kile kilichokuwa cha muda tu kilikuwa na utukufu wake, bila shaka kile chenye kudumu milele kitakuwa na utukufu mkuu zaidi.

3:12 Kwa vile hili ndilo tumaini letu, sisi twasema kwa uhodari mkuu.

3:13 Sisi hatufanyi kama Mose ambaye alilazimika kuufunika uso wake kwa kitambaa ili watu wa Israeli wasiuone ule mwisho wa mng'ao uliokuwa unafifia.

3:14 Lakini akili zao zilipumbazwa. Mpaka leo hii lisomwapo Agano la Kale, kifuniko hicho bado kipo. Kifuniko hicho kitaondolewa tu mtu anapoungana na Kristo.

3:15 Naam, mpaka hivi leo kila isomwapo Sheria ya Mose akili zao huwa zimefunikwa.

3:16 Lakini, wakati mtu amgeukiapo Bwana, kifuniko hicho huondolewa.

3:17 Hapa "Bwana" ni Roho; na pale alipo Roho wa Bwana ndipo ulipo uhuru.

3:18 Basi, sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, twaonyesha kama katika kioo, utukufu wa Bwana; tunabadilishwa tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi. Hiyo ni kazi yake Roho wa Bwana.

4:1 Basi, Mungu, kwa huruma yake, ametukabidhi kazi hii na hivyo hatufi moyo.

4:2 Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali tunaudhihirisha ukweli kwa kuufanya ukweli, na hivyo kujiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele ya Mungu.

4:3 Maana, kama Habari Njema tunayohubiri imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea.

4:4 Hao hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni mfano kamili wa Mungu.

4:5 Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.

4:6 Mungu ambaye alisema, "Mwanga na uangaze kutoka gizani," ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo.

4:7 Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe.

4:8 Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa;

4:9 twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa.

4:10 Kila wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu pia udhihirike katika miili yetu.

4:11 Naam, katika maisha yetu yote tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa.

4:12 Hii ina maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya kazi.

4:13 Maandiko Matakatifu yasema: "Niliamini, ndiyo maana nilinena." Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena.

4:14 Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi.

4:15 Yote haya ni kwa faida yenu; ili kama vile neema ya Mungu inavyoenea kwa watu wengi zaidi na zaidi vivyo hivyo watu wengi zaidi watoe shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.

4:16 Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku.

4:17 Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu: lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho.

4:18 Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.

5:1 Maana tunajua kwamba hema hii ambayo ndani yake tunaishi sasa hapa duniani, yaani mwili wetu, itakapong'olewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono.

5:2 Na sasa, katika hali hii, tunaugua, tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni.

5:3 Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi.

5:4 Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai.

5:5 Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea.

5:6 Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana.

5:7 Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona.

5:8 Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana.

5:9 Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko.

5:10 Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya.

5:11 Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga.

5:12 Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa ninyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni.

5:13 Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu.

5:14 Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake.

5:15 Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao.

5:16 Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena.

5:17 Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika.

5:18 Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, akatupa nasi jukumu la kuwapatanisha watu naye.

5:19 Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye.

5:20 Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu.

5:21 Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu.

6:1 Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure.

6:2 Mungu asema hivi: "Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia." Basi, sasa ndio wakati wa kufaa, sasa ndiyo siku ya wokovu!

6:3 Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuio chochote.

6:4 Badala yake, tunajionyesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu.

6:5 Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula.

6:6 Tunajionyesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki,

6:7 kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu upande wa kulia na upande wa kushoto.

6:8 Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli;

6:9 kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote, kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni wazima kabisa.

6:10 Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini hohehahe, lakini twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu.

6:11 Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa.

6:12 Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu ninyi wenyewe, na si kwa upande wetu.

6:13 Sasa nasema nanyi kama watoto wangu, wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.

6:14 Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja?

6:15 Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Muumini ana uhusiano gani na asiyeamini?

6:16 Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: "Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao; Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu."

6:17 Kwa hiyo Bwana asema pia: "Ondokeni kati yao, mkajitenge nao, msiguse kitu najisi, nami nitawapokea.

6:18 Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa watoto wangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Uwezo."

7:1 Basi, wapenzi wangu, tukiwa tumepewa ahadi hizi zote, na tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu, tuwe watakatifu kabisa, na tuishi kwa kumcha Mungu.

7:2 Tunaomba mtupe nafasi mioyoni mwenu! Hatujamkosea mtu yeyote, hatujamdhuru wala kumdanganya mtu yeyote.

7:3 Sisemi mambo haya kwa ajili ya kumhukumu mtu; maana, kama nilivyokwisha sema, ninyi mko mioyoni mwetu, tufe pamoja, tuishi pamoja.

7:4 Nina imani kubwa sana ninaposema nanyi; naona fahari kubwa juu yenu! Katika taabu zetu nimepata kitulizo kikubwa na kufurahi mno.

7:5 Hata baada ya kufika Makedonia hatukuweza kupumzika. Kila upande tulikabiliwa na taabu: nje ugomvi; ndani hofu.

7:6 Lakini Mungu, mwenye kuwapa shime wanyonge alitupa moyo sisi pia kwa kuja kwake Tito.

7:7 Si tu kwa kule kuja kwake Tito, bali pia kwa sababu ya moyo mliompa ninyi. Yeye ametuarifu jinsi mnavyotamani kuniona, jinsi mlivyo na huzuni, na mnavyotaka kunitetea. Jambo hili linanifurahisha sana.

7:8 Maana, hata kama kwa barua ile yangu nimewahuzunisha, sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini kwa muda.

7:9 Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru ninyi kwa vyovyote.

7:10 Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu, husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo.

7:11 Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: ninyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Ninyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili.

7:12 Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu.

7:13 Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo.

7:14 Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia ninyi mbele ya Tito kumekuwa jambo la ukweli mtupu.

7:15 Hivyo upendo wake wa moyo kwenu unaongezeka zaidi akikumbuka jinsi ninyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu nyingi na kutetemeka.

7:16 Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea ninyi kabisa katika kila jambo.

8:1 Ndugu, tunapenda kuwapa habari juu ya neema ambazo Mungu ameyajalia makanisa ya Makedonia.

8:2 Waumini wa huko walijaribiwa sana kwa taabu; lakini furaha yao ilikuwa kubwa hivi hata wakawa wakarimu kupita kiasi, ingawaje walikuwa maskini sana.

8:3 Naweza kushuhudia kwamba walikuwa wakarimu kadiri ya nguvu zao na hata zaidi. Kwa hiari yao wenyewe,

8:4 walitusihi sana wapewe nafasi ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watu wa Mungu.

8:5 Hilo lilikuwa jambo ambalo hatukulitazamia kabisa! Kwanza walijitolea wao wenyewe kwa Bwana, kisha wakajitolea wenyewe kwetu pia, kufuatana na mapenzi ya Mungu.

8:6 Kwa sababu hiyo, tulimsihi Tito aliyeianza kazi hiyo awasaidieni pia muitekeleze huduma hii ya upendo miongoni mwenu.

8:7 Ninyi mna kila kitu: imani, uwezo wa kusema, elimu; bidii yote ya kutenda mema, na upendo wenu kwetu. Hivyo, tunatazamia muwe wakarimu katika huduma hii ya upendo.

8:8 Siwapi ninyi amri, lakini nataka tu kuonyesha jinsi wengine walivyo na bidii ya kusaidia ili nipate kujua jinsi upendo wenu ulivyo wa kweli.

8:9 Maana, ninyi mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: yeye, ingawa alikuwa na kila kitu, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili kutokana na umaskini wake, awatajirishe.

8:10 Kuhusu jambo hili, basi, nawapeni shauri hili: inafaa kwenu kutekeleza sasa yale mliyoanza mwaka jana. Ninyi mlikuwa wa kwanza kuchukua hatua na kuamua kufanya hivyo.

8:11 Basi, kamilisheni shughuli hiyo; na kama vile mlivyokuwa na hamu kubwa ya kusaidia, basi, fanyeni bidii vivyo hivyo, kadiri ya uwezo wenu, kuikamilisha.

8:12 Maana ikiwa mtu ana moyo wa kusaidia, Mungu hupokea kila anachoweza kutoa: hadai zaidi.

8:13 Ninyi hampaswi kuongezewa taabu kusudi wengine wapunguziwe mzigo wao; sivyo, ila ni lazima tujali usawa na haki.

8:14 Kila mlicho nacho sasa cha ziada kiwasaidie wale wanaohitaji, ili nao wakati watakapokuwa na ziada, wawasaidie ninyi katika mahitaji yenu, na hivyo kuwe na usawa.

8:15 Kama Maandiko yasemavyo: "Aliyekusanya kwa wingi hakuwa na ziada, na yule aliyekusanya kidogo hakupungukiwa."

8:16 Namshukuru Mungu aliyeweka ndani ya moyo wa Tito hamu hiyo niliyo nayo mimi ya kuwasaidia.

8:17 Si tu kwamba alikubali ombi letu, ila pia alikuwa na hamu kubwa ya kusaidia, hata akaamua kwa hiari yake mwenyewe kuja kwenu.

8:18 Pamoja naye, tunamtuma ndugu mmoja ambaye sifa zake katika kueneza Habari Njema zimeenea katika makanisa yote.

8:19 Zaidi ya hayo, yeye amechaguliwa na makanisa awe mwenzetu safarini wakati tunapopeleka huduma hii yetu ya upendo, huduma tunayoifanya kwa ajili ya utukufu wa Bwana na uthibitisho wa nia yetu njema.

8:20 Tunataka kuepa lawama zinazoweza kutokea kuhusu usimamizi wetu juu ya zawadi hii karimu.

8:21 Nia yetu ni kufanya vema, si tu mbele ya Bwana, lakini pia mbele ya watu.

8:22 Basi, pamoja na ndugu hao, tumemtuma ndugu yetu mwingine ambaye mara nyingi tumempa majaribio mbalimbali, tukamwona kuwa ni mwenye hamu kubwa ya kusaidia; hata sasa amekuwa na moyo zaidi kwa sababu ana imani sana nanyi.

8:23 Tito ni mwenzangu; tunafanya kazi pamoja kwa ajili yenu; lakini kuhusu hawa ndugu zetu wengine, wanaokuja pamoja nao, hao ni wajumbe wa makanisa, na utukufu kwa Kristo.

8:24 Basi, waonyesheni uthabiti wa upendo wenu, makanisa yapate kuona kweli kwamba fahari ninayoona juu yenu ni ya halali.

9:1 Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma hiyo yenu kwa ajili ya watu wa Mungu.

9:2 Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: "Ndugu zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana." Hivyo, moto wenu umekwisha wahimiza watu wengi zaidi.

9:3 Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu kama nilivyosema.

9:4 Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika--bila kutaja aibu mtakayopata ninyi wenyewe--kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi.

9:5 Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ionyeshe kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa.

9:6 Kumbukeni: "Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi."

9:7 Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha.

9:8 Mungu anaweza kuwapeni ninyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema.

9:9 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini, wema wahudumu milele."

9:10 Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa ninyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, ziwe na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu.

9:11 Yeye atawatajirisha ninyi daima kwa kila kitu, ili watu wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu.

9:12 Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si tu kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu.

9:13 Kutokana na uthibitisho unaoonyeshwa kwa huduma hii yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote.

9:14 Kwa hiyo watawaombea ninyi kwa moyo kwa sababu ya neema ya pekee aliyowajalieni Mungu.

9:15 Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na kifani!

10:1 Mimi Paulo mwenyewe ambaye naonekana kuwa mpole nikiwa pamoja nanyi, lakini mkali wakati nikiwa mbali nanyi, nawasihini kwa huruma na wema wake Kristo.

10:2 Nawaombeni msinisababishe kuwa mkali wakati nitakapokuja, maana nina hakika naweza kuwa mkali kwa wote wale wanaotudhania kwamba tunaishi kidunia.

10:3 Kweli tunaishi duniani, lakini hatupigani vita kidunia.

10:4 Maana, silaha tunazotumia katika vita vyetu si silaha za kidunia, ila ni nguvu za Mungu zenye kuharibu ngome zote. Tunaharibu hoja zote za uongo,

10:5 na kubomoa kila kizuizi cha majivuno kilichowekwa kuipinga elimu ya Mungu; tunaziteka fikira zote na kuzifanya zimtii Kristo.

10:6 Mkisha kuwa wakamilifu katika kutii, sisi tuko tayari kuadhibu kila namna ya kutotii.

10:7 Ninyi hutazama mambo kwa nje tu. Je, yupo mtu yeyote anayedhani kwamba yeye ni wa Kristo? Sawa! Basi, afikirie vilevile kwamba sisi pia ni wa Kristo kama yeye alivyo wa Kristo.

10:8 Hata kama nimezidi katika kujivuna kwangu juu ya ule uwezo aliotupa--uwezo wa kuwajenga na sio wa kubomoa--hata hivyo sijutii hata kidogo.

10:9 Sipendi mfikiri kwamba nataka kuwatisha ninyi kwa barua zangu.

10:10 Mtu anaweza kusema: "Barua za Paulo ni kali na zenye maneno mazito, lakini yeye mwenyewe anapokuwa pamoja nasi ni mtu dhaifu, na hata anapoongea maneno yake ni kama si kitu."

10:11 Mtu asemaye hivyo heri akumbuke kwamba hakuna tofauti ya yale tunayoandika katika barua wakati tuko mbali, na yale tutakayofanya wakati tutakapokuwa nanyi.

10:12 Kwa vyovyote hatungethubutu kujiweka au kujilinganisha na wale watu wanaojisifia wenyewe. Watu wenye kujifanya wao kuwa kipimo cha kujipimia, na watu wanaojilinganisha wenyewe kwa wenyewe, ni wapumbavu.

10:13 Lakini sisi hatutajivuna kupita kiasi; kujivuna huko kutabaki katika kile kipimo cha kazi aliyotukabidhi Mungu, kazi ambayo tunaifanya pia kwenu.

10:14 Na kwa vile ninyi mu katika mipaka hiyo, hatukuipita tulipokuja kwenu, tukiwaleteeni Habari Njema juu ya Kristo.

10:15 Basi, hatujivunii kazi waliyofanya wengine zaidi ya kipimo tulichopewa; ila tunatumaini kwamba imani yenu itazidi miongoni mwenu kufuatana na kipimo alichotuwekea Mungu.

10:16 Hapo tutaweza kuihubiri Habari Njema katika nchi nyingine, mbali nanyi; na haitakuwa shauri la kujivunia kazi waliyofanya watu wengine mahali pengine.

10:17 Lakini kama yasemavyo Maandiko: "Mwenye kuona fahari na aone fahari juu ya alichofanya Bwana."

10:18 Anayekubaliwa si yule anayejisifu mwenyewe, bali yule anayesifiwa na Bwana.

11:1 Laiti mngenivumilia kidogo, hata kama mimi ni mjinga kiasi fulani! Naam, nivumilieni kidogo.

11:2 Ninawaoneeni wivu lakini ni wivu wa Mungu; maana ninyi ni kama bikira safi niliyemposa kwa mwanamume mmoja tu ambaye ndiye Kristo.

11:3 Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo.

11:4 Maana mtu yeyote ajaye na kumhubiri Yesu aliye tofauti na yule tuliyemhubiri, ninyi mwampokea kwa mikono miwili; au mnakubali roho au habari njema tofauti kabisa na ile mliyopokea kutoka kwetu!

11:5 Sidhani kwamba mimi ni mdogo kuliko hao "mitume wakuu."

11:6 Labda sina ufasaha wa lugha, lakini elimu ninayo; jambo hili tumelionyesha wazi kwenu, kila mahali na kila wakati.

11:7 Mimi niliihubiri kwenu Habari Njema ya Mungu bila kudai mshahara; nilijinyenyekeza ili nipate kuwakweza ninyi. Je, nilifanya vibaya?

11:8 Nilipofanya kazi kati yenu, mahitaji yangu yaligharimiwa na makanisa mengine. Kwa namna moja au nyingine niliwapokonya wao mali yao nipate kuwatumikia ninyi.

11:9 Nilipokuwa nanyi sikumsumbua mtu yeyote nilipohitaji fedha; ndugu waliotoka Makedonia waliniletea kila kitu nilichohitaji. Nilikuwa mwangalifu sana nisiwe mzigo kwa namna yoyote ile, na nitaendelea kufanya hivyo.

11:10 Naahidi kwa ule ukweli wa Kristo ulio ndani yangu, kwamba hakuna kitakachoweza kunizuia kujivunia jambo hilo popote katika Akaya.

11:11 Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu eti siwapendi ninyi? Mungu anajua kwamba nawapenda!

11:12 Nitaendelea kufanya kama ninavyofanya sasa, ili nisiwape nafasi wale wanaotafuta nafasi, nafasi ya kujivuna kwamba eti wanafanya kazi kama sisi.

11:13 Maana, hao ni mitume wa uongo, wafanyakazi wadanganyifu wanojisingizia kuwa mitume wa Kristo.

11:14 Wala si ajabu, maana hata Shetani mwenyewe hujisingizia kuwa malaika wa mwanga!

11:15 Kwa hiyo si jambo la kushangaza ikiwa na hao watumishi wake wanajisingizia kuwa watumishi wa haki. Mwisho wao watapata kile wanachostahili kufuatana na matendo yao.

11:16 Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo.

11:17 Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu.

11:18 Maadam wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna.

11:19 Ninyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu!

11:20 Mnamvumilia hata mtu anayewafanya ninyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni!

11:21 Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu--nasema kama mtu mpumbavu--mimi nathubutu pia.

11:22 Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi.

11:23 Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi--nanena hayo kiwazimu--ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi.

11:24 Mara tano nilichapwa vile viboko thelathini na tisa vya Wayahudi.

11:25 Nilipigwa viboko mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa.

11:26 Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo

11:27 Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo.

11:28 Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote.

11:29 Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi.

11:30 Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu.

11:31 Mungu na Baba wa Bwana Yesu--jina lake litukuzwe milele--yeye anajua kwamba sisemi uongo.

11:32 Nilipokuwa Damasko, mkuu wa mkoa, aliyekuwa chini ya mfalme Areta, alikuwa akiulinda mji wa Damasko ili apate kunikamata.

11:33 Lakini, ndani ya kapu kubwa, niliteremshwa nje kupitia katika nafasi ukutani, nikachopoka mikononi mwake.

12:1 Nitajivuna basi, ingawa haifai! Lakini sasa nitasema juu ya maono na ufunuo alivyonijalia Bwana.

12:2 Namjua mtu mmoja Mkristo, ambaye miaka kumi na minne iliyopita alinyakuliwa mpaka katika mbingu ya tatu. (Sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua.)

12:3 Narudia: najua kwamba mtu huyo alinyakuliwa mpaka peponi. (Lakini sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua.)

12:4 Huko akasikia mambo ya siri ambayo binadamu hastahili kuyatamka.

12:5 Basi, nitajivunia juu ya mtu wa namna hiyo, na si juu yangu mimi binafsi, isipokuwa tu juu ya udhaifu wangu.

12:6 Kama ningetaka kujivuna singekuwa mpumbavu hata kidogo, maana ningekuwa nasema ukweli mtupu. Lakini sitajivuna; sipendi mtu anifikirie zaidi ya vile anavyoona na kusikia kutoka kwangu.

12:7 Lakini, kusudi mambo haya makuu niliyofunuliwa yasinifanye nilewe majivuno, nilipewa maumivu mwilini kama mwiba, mjumbe wa Shetani mwenye kunipiga nisijivune kupita kiasi.

12:8 Nilimsihi Bwana mara tatu kuhusu jambo hili ili linitoke.

12:9 Lakini akaniambia: "Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu." Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu.

12:10 Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, madharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu.

12:11 Nimekuwa kama mpumbavu, lakini, ninyi mmenilazimisha kuwa hivyo. Ninyi ndio mngalipaswa kunisifu. Maana, ingawa mimi si kitu, kwa vyovyote, mimi si mdogo zaidi kuliko hao "mitume wakuu."

12:12 Miujiza na maajabu yaonyeshayo wazi kwamba mimi ni mtume yalifanyika miongoni mwenu kwa uvumilivu wote.

12:13 Je, mlipungukiwa nini zaidi kuliko makanisa mengine, isipokuwa tu kwamba mimi kwa upande wangu sikuwasumbueni kupata msaada wenu? Samahani kwa kuwakoseeni haki hiyo!

12:14 Sasa niko tayari kabisa kuja kwenu mara ya tatu, na sitawasumbua. Maana ninachotafuta si mali zenu, bali ni ninyi wenyewe. Ni kawaida ya wazazi kuwawekea watoto wao akiba, na si watoto kuwawekea wazazi wao.

12:15 Mimi ni radhi kabisa kutumia nilicho nacho, na hata kujitolea mimi mwenyewe kabisa, kwa faida ya roho zenu. Je, mtanipenda kidogo ati kwa kuwa mimi nawapenda ninyi mno?

12:16 Basi, mtakubali kwamba sikuwa mzigo kwenu. Lakini labda mtu mwingine atasema: "Kwa vile Paulo ni mwerevu, amewafanyieni ulaghai."

12:17 Je, mimi niliwanyonyeni kwa njia ya mjumbe yeyote niliyemtuma kwenu?

12:18 Mimi nilimwita Tito, nikamtuma kwenu na ndugu yetu mwingine. Je, Tito aliwanyonyeni? Je, hamjui kwamba sisi tumekuwa tukiongozwa na roho yuleyule, na mwenendo wetu ni mmoja?

12:19 Labda mnafikiri kwamba mpaka sasa tumekuwa tukijitetea wenyewe mbele yenu! Lakini, tunasema mambo haya mbele ya Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo. Mambo hayo, yote, wapenzi wangu, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi.

12:20 Naogopa, huenda nitakapokuja kwenu nitawakuta katika hali nisiyopenda, nami itanilazimu kuwa katika hali msiyoipenda. Naogopa huenda kukawa na ugomvi, wivu, uhasama, ubishi, masengenyano, kunong'ona, majivuno na fujo kati yenu.

12:21 Naogopa huenda hapo nitakapokuja safari ijayo Mungu wangu atanifanya niaibike mbele yenu, nami nitaomboleza kwa ajili ya wengi wa wale waliotenda dhambi lakini hawakujutia huo uchafu, tamaa zao mbaya na uzinzi waliokuwa wamefanya.

13:1 Hii ni mara yangu ya tatu kuja kwenu. "Kila tatizo litatatuliwa kwa ushahidi wa watu wawili au watatu," yasema Maandiko.

13:2 Nilikwisha sema, na kama ilivyokuwa safari ya pili, sasa nasema tena nikiwa mbali: wale wote waliotenda uovu bila kutubu, na pia wale wengine, nitakapokuja, watakiona cha mtema kuni.

13:3 Mtajionea wenyewe kwamba Kristo anasema ndani yangu. Kwenu Kristo si dhaifu; bali nguvu yake yafanya kazi miongoni mwenu.

13:4 Maana hata kama alisulubiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye lakini tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu.

13:5 Jichunguzeni ninyi wenyewe mpate kujua kama kweli mnayo imani. Jichunguzeni ninyi wenyewe. Je, hamjui kwamba Kristo Yesu yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi ninyi mmeshindwa.

13:6 Lakini natumaini kwamba ninyi mnajua kuwa sisi hatukushindwa.

13:7 Tunamwomba Mungu msifanye uovu wowote, lakini si kusudi tuonekane kama watu waliokwisha faulu, bali mpate kutenda mema, hata kama sisi tunaonekana kuwa tumeshindwa.

13:8 Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa kuuendeleza ukweli.

13:9 Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu.

13:10 Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa.

13:11 Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa mapendo na amani atakuwa pamoja nanyi.

13:12 Salimianeni kwa ishara ya upendo.

13:13 (G13-12) Watu wote wa Mungu huku wanawasalimuni.

13:14 (G13-13) Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote.


Next: Galatians