Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: Acts

1:1 Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake

1:2 mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua.

1:3 Kwa muda wa siku arobaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu.

1:4 Wakati walipokutana pamoja aliwaamuru hivi: "Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeeni ile zawadi aliyoahidi Baba, zawadi ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake.

1:5 Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu."

1:6 Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, "Je Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?"

1:7 Lakini Yesu akawaambia, "Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini.

1:8 Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni ninyi, mtajazwa nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia."

1:9 Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena.

1:10 Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao,

1:11 wakasema, "Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mliivyomwona akienda mbinguni."

1:12 Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini.

1:13 Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo.

1:14 Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.

1:15 Siku chache baadaye, kulikuwa na mkutano wa waumini, karibu watu mia moja na ishirini. Petro alisimama mbele yao,

1:16 akasema, "Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni.

1:17 Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu.

1:18 ("Mnajua kwamba yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu. Akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje.

1:19 Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba Hekeli Dama, maana yake, Shamba la Damu.)

1:20 Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi: Nyumba yake ibaki mahame; mtu yeyote asiishi ndani yake. Tena imeandikwa: Mtu mwingine achukue nafasi yake katika huduma hiyo.

1:21 Kwa hiyo, ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi kama shahidi wa ufufuo wake Bwana Yesu.

1:22 Anapaswa kuwa mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana alipokuwa anasafiri pamoja nasi, tangu wakati Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni."

1:23 Basi, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia.

1:24 Kisha wakasali: "Bwana, wewe unajua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua

1:25 ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe."

1:26 Hapo, wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.

2:1 Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika pamoja.

2:2 Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikajaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa.

2:3 Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao.

2:4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha.

2:5 Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani.

2:6 Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

2:7 Walistaajabu na kushangaa, wakisema, "Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya?

2:8 Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe?

2:9 Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelami; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia,

2:10 Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libya karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma,

2:11 Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu."

2:12 Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, "Hii ina maana gani?"

2:13 Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, "Watu hawa wamelewa divai mpya!"

2:14 Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: "Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu.

2:15 Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi?

2:16 Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli:

2:17 Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, wanaume kwa wanawake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.

2:18 Naam, hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, nitawamiminia Roho wangu, siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu.

2:19 Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito;

2:20 jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana.

2:21 Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.

2:22 "Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua.

2:23 Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe.

2:24 Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge.

2:25 Maana Daudi alisema juu yake hivi: Nilimwona Bwana mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia, na hivyo sitatikisika.

2:26 Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini;

2:27 kwa kuwa hutaiacha roho yangu katika kuzimu, wala kumruhusu mtakatifu wako aoze.

2:28 Umenionyesha njia za kuufikia uzima, kuwako kwako kwanijaza furaha!

2:29 "Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo.

2:30 Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake.

2:31 Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.

2:32 Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo.

2:33 Yesu aliinuliwa juu mpaka upande wa kulia wa Mungu, akapokea kutoka kwa Baba ile zawadi aliyoahidi yaani Roho Mtakatifu; na mnachoona sasa na kusikia ni mmiminiko wa huyo Roho.

2:34 Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia,

2:35 hadi nitakapowafanya adui zako kibao cha kukanyagia miguu yako.

2:36 "Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha ninyi, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo."

2:37 Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: "Ndugu zetu, tufanye nini?"

2:38 Petro akajibu, "Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile zawadi ya Roho Mtakatifu.

2:39 Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali; na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake."

2:40 Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, "Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu."

2:41 Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao elfu tatu wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo.

2:42 Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kidugu, kumega mkate na kusali.

2:43 Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila mtu akajawa na hofu.

2:44 Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana pamoja.

2:45 Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja.

2:46 Waliendelea kukutana pamoja kila siku Hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu.

2:47 Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.

3:1 Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wanakwenda Hekaluni, wakati wa sala.

3:2 Na pale karibu na mlango wa Hekalu uitwao "Mlango Mzuri", palikuwa na mtu mmoja, kiwete tangu kuzaliwa. Watu walimbeba huyo mtu kila siku na kumweka hapo ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia Hekaluni.

3:3 Alipowaona Petro na Yohane wakiingia Hekaluni, aliwaomba wampe chochote.

3:4 Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, "Tutazame!"

3:5 Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.

3:6 Kisha Petro akamwambia, "Sina fedha wala dhahabu lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!"

3:7 Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu.

3:8 Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao Hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu.

3:9 Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu.

3:10 Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule "Mlango Mzuri" wa Hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.

3:11 Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa "Ukumbi wa Solomoni," ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane.

3:12 Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, "Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea?

3:13 Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Yesu mtumishi wake. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru.

3:14 Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini ninyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe.

3:15 Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uzima. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo.

3:16 Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote.

3:17 "Sasa ndugu zangu, nafahamu kwamba ninyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutojua kwenu.

3:18 Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke.

3:19 Basi, tubuni mkamrudie Mungu ili afute dhambi zenu.

3:20 Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu.

3:21 Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani.

3:22 Kwa maana Mose alisema, Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu ninyi wenyewe.

3:23 Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.

3:24 Manabii wote, kuanzia Samweli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi.

3:25 Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.

3:26 Basi, ilikuwa kwa ajili yenu kwanza kwamba Mungu alimfufua mtumishi wake, alimtuma awabariki kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake."

4:1 Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa Hekalu pamoja na Masadukayo walifika.

4:2 Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonyesha wazi kwamba wafu watafufuka.

4:3 Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake.

4:4 Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu elfu tano.

4:5 Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na walimu wa Sheria, walikusanyika pamoja huko Yerusalemu.

4:6 Walikutana pamoja na Anasi, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa Kuhani Mkuu.

4:7 Waliwasimamisha mitume mbele yao, wakawauliza, "Ninyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?"

4:8 Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, "Viongozi na wazee wa watu!

4:9 Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima,

4:10 basi, ninyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye ninyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka wafu.

4:11 Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: Jiwe mlilokataa ninyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.

4:12 Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye."

4:13 Hao wazee wa baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu.

4:14 Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu.

4:15 Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha.

4:16 Wakaulizana, "Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba mwujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo.

4:17 Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu."

4:18 Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu.

4:19 Lakini Petro na Yohane wakawajibu, "Amueni ninyi wenyewe kama ni haki mbele ya Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii yeye.

4:20 Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia."

4:21 Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo.

4:22 Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arobaini.

4:23 Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee.

4:24 Waliposikia habari hiyo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, "Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo!

4:25 Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, babu yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure?

4:26 Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, ili kumwasi Bwana na Kristo wake.

4:27 "Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye umemtia mafuta.

4:28 Naam, walikutana ili wafanye yale ambayo ulikusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako.

4:29 Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari.

4:30 Nyosha mkono wako uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu."

4:31 Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila uoga.

4:32 Jumuiya yote ya waumini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo.

4:33 Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi.

4:34 Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza

4:35 na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake.

4:36 Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita jina Barnaba (maana yake, "Mtu mwenye kutia moyo").

4:37 Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

5:1 Mtu mmoja aitwaye Anania na mkewe Safira waliuza shamba lao vilevile.

5:2 Lakini, mkewe akiwa anajua, Anania akajiwekea sehemu ya fedha alizopata na ile sehemu nyingine akawakabidhi mitume.

5:3 Basi, Petro akamwuliza, "Anania, mbona Shetani ameuingia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba?

5:4 Kabla ya kuliuza lilikuwa mali yako, na baada ya kuliuza, bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo. Kwa nini basi, uliamua moyoni mwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu; umemdanganya Mungu!"

5:5 Anania aliposikia hayo, akaanguka chini, akafa. Watu wote waliosikia habari ya tukio hilo waliogopa sana.

5:6 Vijana wakafika wakaufunika mwili wake, wakamtoa nje, wakamzika.

5:7 Baada ya muda wa saa tatu hivi, mke wake, bila kufahamu mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani.

5:8 Petro akamwambia, "Niambie! Je, kiasi hiki cha fedha ndicho mlichopata kwa kuuza lile shamba?" Yeye akamjibu, "Naam, ni kiasi hicho."

5:9 Naye Petro akamwambia, "Mbona mmekula njama kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Wale watu waliokwenda kumzika mume wako, sasa wako mlangoni na watakuchukua wewe pia."

5:10 Mara Safira akaanguka mbele ya miguu ya Petro, akafa. Wale vijana walipoingia, walimkuta amekwisha kufa; hivyo wakamtoa nje, wakamzika karibu na mume wake.

5:11 Kanisa lote pamoja na wote waliosikia habari ya tukio hilo, waliogopa sana.

5:12 Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Waumini walikuwa wakikutana pamoja katika ukumbi wa Solomoni.

5:13 Mtu yeyote mwingine ambaye hakuwa mwamini hakuthubutu kujiunga nao. Hata hivyo, watu wengine wasiokuwa wa imani hiyo waliwasifu.

5:14 Idadi ya watu waliomwamini Bwana, wanaume kwa wanawake, iliongezeka zaidi na zaidi.

5:15 Kwa sababu hiyo, watu walikuwa wakipeleka wagonjwa barabarani na kuwalaza juu ya vitanda na mikeka ili Petro akipita, walau kivuli chake kiwaguse baadhi yao.

5:16 Watu wengi walifika kutoka katika miji ya kando kando ya Yerusalemu, wakiwaleta wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa.

5:17 Kisha, Kuhani Mkuu na wenzake waliokuwa wa kikundi cha Masadukayo wa mahali hapo, wakawaonea mitume wivu.

5:18 Basi, wakawatia nguvuni, wakawafunga ndani ya gereza kuu.

5:19 Lakini usiku malaika wa Bwana aliifungua milango ya gereza, akawatoa nje, akawaambia,

5:20 "Nendeni mkasimame Hekaluni na kuwaambia watu kila kitu kuhusu maisha haya mapya."

5:21 Mitume walitii, wakaingia Hekaluni asubuhi na mapema, wakaanza kufundisha. Kuhani Mkuu na wenzake walipofika, waliita mkutano wa Baraza kuu, yaani halmashauri yote ya wazee wa Wayahudi halafu wakawatuma watu gerezani wawalete wale mitume.

5:22 Lakini hao watumishi walipofika huko hawakuwakuta mle gerezani. Hivyo walirudi, wakatoa taarifa mkutanoni,

5:23 wakisema, "Tulikuta gereza limefungwa kila upande na walinzi wakilinda milango. Lakini tulipofungua hatukumkuta mtu yeyote ndani."

5:24 Mkuu wa walinzi wa Hekalu na makuhani wakuu waliposikia habari hiyo wakawa na wasiwasi, wasijue yaliyowapata.

5:25 Akafika mtu mmoja, akawaambia, "Wale watu mliowafunga gerezani, hivi sasa wamo Hekaluni, wanawafundisha watu."

5:26 Hapo mkuu wa walinzi wa Hekalu pamoja na watu wake walikwenda Hekaluni, akawaleta. Lakini hawakuwakamata kwa kutumia nguvu, maana waliogopa kwamba watu wangewapiga mawe.

5:27 Basi, wakawapeleka, wakawasimamisha mbele ya Baraza. Kuhani Mkuu akawaambia,

5:28 "Tuliwakatazeni waziwazi kufundisha kwa jina la mtu huyu; sasa mmeyaeneza mafundisho yenu pote katika Yerusalemu na mnakusudia kutuwekea lawama ya kifo cha mtu huyo."

5:29 Hapo Petro, akiwa pamoja na wale mitume wengine, akajibu, "Lazima tumtii Mungu, na siyo binadamu.

5:30 Mungu wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya ninyi kumwua kwa kumtundika msalabani.

5:31 Huyu ndiye yule aliyekwezwa na Mungu mpaka upande wake wa kulia, akawa kiongozi na Mwokozi, ili awawezeshe watu wa Israeli watubu, wapate kusamehewa dhambi zao.

5:32 Sisi ni mashahidi wa tukio hilo, naye Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii, anashuhudia pia tukio hilo."

5:33 Wajumbe wote wa lile Baraza waliposikia hayo, wakawaka hasira, hata wakaamua kuwaua.

5:34 Lakini Mfarisayo mmoja aitwaye Gamalieli ambaye alikuwa mwalimu wa Sheria na aliyeheshimika sana mbele ya watu wote, alisimama mbele ya lile Baraza, akataka wale mitume watolewe nje kwa muda mfupi.

5:35 Kisha akawaambia wale wajumbe wa Baraza, "Wananchi wa Israeli, tahadhari kabla ya kutekeleza hicho mnachotaka kuwatenda watu hawa!

5:36 Zamani kidogo, kulitokea mtu mmoja jina lake Theuda, akajisema kuwa mtu wa maana na watu karibu mia nne wakajiunga naye. Lakini aliuawa, kisha wafuasi wake wote wakatawanyika na kikundi chake kikafa.

5:37 Tena, baadaye, wakati ule wa kuhesabiwa watu, alitokea Yuda wa Galilaya. Huyu naye, aliwavuta watu wakamfuata; lakini naye pia aliuawa, na wafuasi wake wakatawanyika.

5:38 Na sasa pia mimi nawaambieni, msiwachukulie watu hawa hatua yoyote; waacheni! Kwa maana, ikiwa mpango huu au shughuli hii yao imeanzishwa na binadamu, itatoweka yenyewe.

5:39 Lakini kama imeanzishwa na Mungu, siyo tu kwamba hamtaweza kuwashinda, bali mtajikuta mnapigana na Mungu." Basi, wakakubaliana naye.

5:40 Hivyo wakawaita wale mitume, wakaamuru wachapwe viboko na kuwaonya wasifundishe tena kwa jina la Yesu; kisha wakawaacha waende zao.

5:41 Basi, mitume wakatoka nje ya ule mkutano wa halmashauri wakiwa wamejaa furaha, kwani walistahili kuaibishwa kwa ajili ya jina la Yesu.

5:42 Wakaendelea kila siku kufundisha na kuhubiri Habari Njema ya Kristo, Hekaluni na nyumbani mwa watu.

6:1 Baadaye, idadi ya wanafunzi ilipokuwa inazidi kuongezeka, kulitokea manung'uniko kati ya wanafunzi waliosema Kigiriki na wale waliosema Kiebrania. Wale waliosema Kigiriki walinung'unika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji wa mahitaji ya kila siku.

6:2 Kwa hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema, "Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji wa mahitaji.

6:3 Hivyo, ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo.

6:4 Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri neno la Mungu."

6:5 Jambo hilo likaipendeza jumuiya yote ya waumini. Wakawachagua Stefano, mtu mwenye imani kubwa na mwenye kujawa na Roho Mtakatifu, Filipo, Prokoro, Nikanora, Timona, Parmena na Nikolao wa Antiokia ambaye hapo awali alikuwa ameongokea dini ya Kiyahudi.

6:6 Wakawaweka mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono.

6:7 Neno la Mungu likazidi kuenea na idadi ya waumini huko Yerusalemu ikaongezeka zaidi, na kundi kubwa la makuhani wakaipokea imani.

6:8 Mungu alimjalia Stefano neema tele, akampa nguvu nyingi hata akawa anatenda miujiza na maajabu kati ya watu.

6:9 Lakini watu fulani wakatokea ili wabishane na Stefano. Baadhi ya watu hao walikuwa wa sunagogi moja lililoitwa "Sunagogi la Watu Huru", nao walitoka Kurene na Aleksandria; wengine walitoka Kilikia na Asia.

6:10 Lakini hawakuweza kumshinda kwa sababu ya hekima yake na kwa sababu ya yule Roho aliyeongoza maneno yake.

6:11 Kwa hiyo waliwahonga watu kadhaa waseme: "Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kumkashifu Mose na kumkashifu Mungu."

6:12 Kwa namna hiyo, waliwachochea watu, wazee na walimu wa Sheria. Basi, wakamjia Stefano, wakamkamata na kumleta mbele ya Baraza kuu.

6:13 Walileta Barazani mashahidi wa uongo ambao walisema, "Mtu huyu haachi kamwe kusema maneno ya kupakashifu mahali hapa patakatifu na Sheria ya Mose.

6:14 Kwa maana tulikwisha msikia akisema eti huyo Yesu wa Nazareti atapaharibu kabisa mahali hapa na kufutilia mbali desturi zile tulizopokea kutoka kwa Mose."

6:15 Wote waliokuwa katika kile kikao cha Baraza walimkodolea macho Stefano, wakauona uso wake umekuwa kama wa malaika.

7:1 Basi, Kuhani Mkuu akamwuliza, "Je, mambo haya ni kweli?"

7:2 Naye Stefano akasema, "Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni! Mungu alimtokea baba yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia kabla hajaenda kukaa kule Harani.

7:3 Mungu alimwambia: Ondoka katika nchi yako; waache watu wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonyesha!

7:4 Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa.

7:5 Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake; hata hivyo, alimwahidia kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje wakati huu hakuwa na mtoto.

7:6 Mungu alimwambia hivi: Wazao wako watapelekwa katika nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa vibaya kwa muda wa miaka mia nne.

7:7 Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.

7:8 Halafu Mungu aliifanya tohara iwe ishara ya agano. Hivyo, Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka, siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka, vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na wawili vivyo hivyo.

7:9 "Wale mababu walimwonea wivu Yosefu, wakamuuza utumwani Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye,

7:10 akamwokoa katika taabu zake zote. Mungu alimjalia fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri, hata Farao akamweka awe mkuu wa ile nchi na nyumba ya kifalme.

7:11 Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula chochote.

7:12 Basi, Yakobo alipopata habari kwamba huko Misri kulikuwa na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya kwanza.

7:13 Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu.

7:14 Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla watu sabini na tano, waje Misri.

7:15 Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu wengine walikufa.

7:16 Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi Abrahamu alilonunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.

7:17 "Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi.

7:18 Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza kutawala huko Misri.

7:19 Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe.

7:20 Mose alizaliwa wakati huo. Alikuwa mtoto mzuri sana. Alilelewa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu,

7:21 na alipotolewa nje, binti wa Farao alimchukua, akamlea kama mtoto wake.

7:22 Mose alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa mashuhuri kwa maneno na matendo.

7:23 "Alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli.

7:24 Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri.

7:25 (Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo.)

7:26 Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha, akisema: Ninyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya ninyi kwa ninyi?

7:27 Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wa watu?

7:28 Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?

7:29 Baada ya kusikia hayo Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili.

7:30 "Miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai.

7:31 Mose alistaajabu sana kuona jambo hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana:

7:32 Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo! Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi.

7:33 Bwana akamwambia: Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu.

7:34 Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.

7:35 "Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu? Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi.

7:36 Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa muda wa miaka arobaini.

7:37 Mose ndiye aliyewaambia watu wa Israeli: Mungu atawateulieni nabii kama mimi kutoka katika ndugu zenu ninyi wenyewe.

7:38 Wakati watu wa Israeli walipokutana pamoja kule jangwani, Mose ndiye aliyekuwako huko pamoja nao. Alikuwa huko pamoja na babu zetu na yule malaika aliyeongea naye mlimani Sinai; ndiye aliyekabidhiwa yale maneno yaletayo uzima atupe sisi.

7:39 "Lakini yeye ndiye babu zetu waliyemkataa kumsikiliza; walimsukuma kando, wakatamani kurudi Misri.

7:40 Walimwambia Aroni: Tutengenezee miungu itakayotuongoza njiani, maana hatujui yaliyompata Mose huyu aliyetuongoza kutoka Misri!

7:41 Hapo ndipo walipojitengenezea sanamu ya ndama, wakaitambikia na kukifanyia sherehe kitu ambacho ni kazi ya mikono yao wenyewe.

7:42 Lakini Mungu aliondoka kati yao, akawaacha waabudu nyota za anga, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii: Enyi watu wa Israeli! Si mimi mliyenitolea dhabihu na sadaka kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani!

7:43 Ninyi mlikibeba kibanda cha mungu Moloki, na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani. Sanamu mlizozifanya ndizo mlizoabudu. Kwa sababu hiyo nitakupeleka mateka mbali kupita Babuloni!

7:44 Kule jangwani babu zetu walikuwa na lile hema lililoshuhudia kuweko kwa Mungu. Lilitengenezwa kama Mungu alivyomwambia Mose alifanye; nakala kamili ya kile alichoonyeshwa.

7:45 Kisha babu zetu walilipokezana wao kwa wao mpaka wakati wa Yoshua, walipoinyakua ile nchi kutoka kwa mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao. Hapo lilikaa mpaka nyakati za Daudi.

7:46 Daudi alipata upendeleo kwa Mungu, akamwomba Mungu ruhusa ya kumjengea makao yeye aliye Mungu wa Yakobo.

7:47 Lakini Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.

7:48 "Hata hivyo, Mungu Mkuu haishi katika nyumba zilizojengwa na binadamu; kama nabii asemavyo:

7:49 Bwana asema: Mbingu ni kiti changu cha enzi na dunia ni kiti changu cha kuwekea miguu.

7:50 Ni nyumba ya namna gani basi mnayoweza kunijengea, na ni mahali gani nitakapopumzika? Vitu hivi vyote ni mimi nimevifanya, au sivyo?

7:51 "Enyi wakaidi wakuu! Mioyo na masikio yenu ni kama ya watu wa mataifa. Ninyi ni kama baba zenu. Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu.

7:52 Je, yuko nabii yeyote ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua hao Mungu aliowatuma watangaze kuja kwake yule Mwenye Haki. Na sasa, ninyi mmemsaliti, mkamuua.

7:53 Ninyi mliipokea ile Sheria iliyoletwa kwenu na Malaika, lakini hamkuitii."

7:54 Wale wazee wa Baraza waliposikia hayo, walighadhibika sana, wakamsagia meno kwa hasira.

7:55 Lakini Stefano akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akatazama juu mbinguni, akauona utukufu wa Mungu na Yesu amekaa upande wa kulia wa Mungu.

7:56 Akasema, "Tazameni! Ninaona mbingu zimefunuliwa na Mwana wa Mtu amesimama upande wa kulia wa Mungu."

7:57 Hapo, watu wote katika kile kikao cha Baraza, wakapiga kelele na kuziba masikio yao kwa mikono yao. Kisha wakamrukia wote kwa pamoja,

7:58 wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe. Wale mashahidi wakayaweka makoti yao chini ya ulinzi wa kijana mmoja jina lake Saulo.

7:59 Waliendelea kumpiga mawe Stefano, huku akiwa anasali: "Bwana Yesu, ipokee roho yangu!"

7:60 Akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa: "Bwana, usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii." Baada ya kusema hivyo, akafa.

8:1 Saulo naye alikiona kitendo hicho cha kumwua Stefano kuwa sawa. Siku hiyo kanisa la Yerusalemu lilianza kuteswa vibaya. Waumini wote, isipokuwa tu wale mitume, walilazimika kutawanyika katika sehemu za mashambani za Yudea na Samaria.

8:2 Watu wamchao Mungu, walimzika Stefano na kumfanyia maombolezo makubwa.

8:3 Wakati huohuo, Saulo alijaribu kuliangamiza kanisa. Alikwenda katika kila nyumba, akawatoa nje waumini, wanaume kwa wanawake, akawatia gerezani.

8:4 Wale waumini waliotawanyika, walikwenda kila mahali wakihubiri ule ujumbe.

8:5 Naye Filipo aliingia katika mji wa Samaria na kumhubiri Kristo kwa wenyeji wa hapo.

8:6 Watu walijiunga kusikiliza kwa makini ule ujumbe wa Filipo na kuona ile miujiza aliyoifanya.

8:7 Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa.

8:8 Kukawa na furaha kubwa katika mji ule.

8:9 Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni ambaye alikuwa amekwisha fanya uchawi wake katika mji huo kwa muda na kuwashangaza watu wa Samaria, akijiona kuwa yeye ni mtu maarufu.

8:10 Watu wote, wadogo na wakubwa, walimsikiliza kwa makini wakisema, "Simoni ndiye ile nguvu ya kimungu inayoitwa Nguvu Kubwa."

8:11 Walivutiwa sana naye kwa vile alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake kwa muda mrefu.

8:12 Lakini walipouamini ujumbe wa Filipo juu ya Habari Njema ya Ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, walibatizwa, wanawake na wanaume.

8:13 Hata Simoni aliamini; baada ya kubatizwa ilikuwa akiandamana na Filipo, akastaajabia maajabu na miujiza iliyokuwa inafanyika.

8:14 Wale mitume waliokuwa kule Yerusalemu walipopata habari kwamba wenyeji wa Samaria nao wamelipokea neno la Mungu, waliwatuma kwao Petro na Yohane.

8:15 Walipofika waliwaombea hao waumini ili wampokee Roho Mtakatifu;

8:16 maana wakati huo Roho Mtakatifu hakuwa ameshukia yeyote kati yao; walikuwa wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu.

8:17 Basi, Petro na Yohane wakawawekea mikono hao waumini, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

8:18 Hapo Simoni aling'amua kwamba kwa kuwekewa mikono ya mitume waumini walipewa Roho Mtakatifu. Hivyo aliwapa Petro na Yohane fedha akisema,

8:19 "Nipeni na mimi uwezo huo ili yeyote nitakayemwekea mikono, apokee Roho Mtakatifu."

8:20 Lakini Petro akamjibu, "Potelea mbali na fedha zako kwa vile unafikiri kwamba unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha!

8:21 Huna sehemu yoyote wala haki katika kazi hiyo kwa maana moyo wako hauko sawa mbele ya macho ya Mungu.

8:22 Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu na umwombe Bwana naye anaweza kukusamehe fikira kama hizo.

8:23 Ni dhahiri kwangu kwamba umejaa wivu mkali na mfungwa wa dhambi!"

8:24 Simoni akajibu, "Tafadhali, niombeeni kwa Bwana lisije likanipata lolote kati ya hayo mliyosema."

8:25 Baada ya Petro na Yohane kutoa ushuhuda wao na kuutangaza ujumbe wa Bwana, walirudi Yerusalemu. Walipokuwa wanarudi walihubiri Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria.

8:26 Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, "Jitayarishe uende kusini kupitia njia inayotoka Yerusalemu kwenda Gaza." (Njia hiyo hupita jangwani.)

8:27 Basi, Filipo akajiweka tayari, akaanza safari. Wakati huohuo kulikuwa na Mwethiopia mmoja, towashi, ambaye alikuwa anasafiri kuelekea nyumbani. Huyo mtu alikuwa ofisa maarufu wa hazina ya Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa amekwenda huko Yerusalemu kuabudu na wakati huo alikuwa anarudi akiwa amepanda gari la kukokotwa.

8:28 Alipokuwa anasafiri, alikuwa akijisomea kitabu cha nabii Isaya.

8:29 Basi, Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, "Nenda karibu na gari hilo ukafuatane nalo."

8:30 Filipo akakimbilia karibu na gari, akamsikia huyo mtu akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. Hapo Filipo akamwuliza, "Je, unaelewa hayo unayosoma?"

8:31 Huyo mtu akamjibu, "Ninawezaje kuelewa bila mtu kunielewesha?" Hapo akamwalika Filipo apande juu, aketi pamoja naye.

8:32 Basi, sehemu ya Maandiko Matakatifu aliyokuwa anasoma ilikuwa hii: "Alikuwa kama kondoo anayepelekwa kuchinjwa; kimya kama vile mwana kondoo anaponyolewa manyoya, yeye naye hakutoa sauti hata kidogo.

8:33 Alifedheheshwa na kunyimwa haki. Hakuna atakayeweza kuongea juu ya kizazi chake, kwa maana maisha yake yameondolewa duniani."

8:34 Huyo Mwethiopia akamwambia Filipo, "Niambie, huyu nabii anasema juu ya nani? Anasema mambo haya juu yake yeye mwenyewe au juu ya mtu mwingine?"

8:35 Basi, Filipo akianzia na sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu, akamweleza Habari Njema juu ya Yesu.

8:36 Walipokuwa bado wanaendelea na safari walifika mahali penye maji na huyo ofisa akasema, "Mahali hapa pana maji; je, kuna chochote cha kunizuia nisibatizwe?"

8:37 Filipo akasema, "Kama unaamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa." Naye akajibu, "Naam, ninaamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu."

8:38 Basi, huyo ofisa akaamuru lile gari lisimame; na wote wawili, Filipo na huyo ofisa wakashuka majini, naye Filipo akambatiza.

8:39 Walipotoka majini Roho wa Bwana akamfanya Filipo atoweke. Na huyo Mwethiopia hakumwona tena; lakini akaendelea na safari yake akiwa amejaa furaha.

8:40 Filipo akajikuta yuko Azoto, akapita katika miji yote akihubiri Habari Njema mpaka alipofika Kaisarea.

9:1 Wakati huo Saulo alikuwa akizidisha vitisho vikali vya kuwaua wafuasi wa Bwana. Alikwenda kwa Kuhani Mkuu,

9:2 akaomba apatiwe barua za utambulisho kwa masunagogi ya Kiyahudi kule Damasko, ili akikuta huko wanaume au wanawake wanaofuata Njia ya Bwana, awakamate na kuwaleta Yerusalemu.

9:3 Lakini alipokuwa njiani karibu kufika Damasko, ghafla mwanga kutoka angani ulimwangazia pande zote.

9:4 Akaanguka chini na kusikia sauti ikimwambia: "Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?"

9:5 Naye Saulo akauliza, "Ni nani wewe Bwana?" Na ile sauti ikajibu, "Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.

9:6 Lakini simama sasa, uingie mjini na huko utaambiwa unachopaswa kufanya."

9:7 Wale watu waliokuwa wanasafiri pamoja na Saulo walisimama pale, wakiwa hawana la kusema; walisikia ile sauti lakini hawakumwona mtu.

9:8 Saulo aliinuka, na alipofumbua macho yake hakuweza kuona chochote; hivyo wale watu wakamwongoza kwa kumshika mkono mpaka mjini Damasko.

9:9 Saulo alikaa siku tatu bila kuona, na wakati huo hakula au kunywa chochote.

9:10 Basi, huko Damasko kulikuwa na mfuasi mmoja aitwaye Anania. Bwana akamwambia katika maono, "Anania!" Anania akaitika, "Niko hapa, Bwana."

9:11 Naye Bwana akamwambia, "Jitayarishe uende kwenye barabara inayoitwa Barabara ya Moja kwa Moja, na katika nyumba ya Yuda umtake mtu mmoja kutoka Tarso aitwaye Saulo. Sasa anasali;

9:12 na katika maono ameona mtu aitwaye Anania akiingia ndani na kumwekea mikono ili apate kuona tena."

9:13 Lakini Anania akajibu, "Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kutoka kwa watu wengi; nimesikia juu ya mabaya aliyowatendea watu wako huko Yerusalemu.

9:14 Na amekuja hapa akiwa na mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwatia nguvuni wote wanaoomba kwa jina lako."

9:15 Lakini Bwana akamwambia, "Nenda tu, kwa maana nimemchagua awe chombo changu, alitangaze jina langu kwa mataifa na wafalme wao na kwa watu wa Israeli.

9:16 Mimi mwenyewe nitamwonyesha mengi yatakayomlazimu kuteswa kwa ajili ya jina langu."

9:17 Basi, Anania akaenda, akaingia katika hiyo nyumba. Kisha akaweka mikono yake juu ya Saulo, akasema, "Ndugu Saulo, Bwana ambaye ndiye Yesu mwenyewe aliyekutokea ulipokuwa njiani kuja hapa, amenituma ili upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu."

9:18 Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka macho ya Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa.

9:19 Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko.

9:20 Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.

9:21 Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, "Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!"

9:22 Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa.

9:23 Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi walikusanyika na kufanya mpango wa kumwua Saulo.

9:24 Lakini Saulo alipata habari ya mpango huo. Usiku na mchana walilinda milango ya kuingia mjini ili wapate kumwua.

9:25 Lakini wakati wa usiku wanafunzi wake walimchukua, wakamteremsha chini ndani ya kapu kubwa kwa kupitia nafasi iliyokuwako ukutani.

9:26 Saulo alipofika Yerusalemu alijaribu kujiunga na wale wanafunzi. Lakini wote walimwogopa, na hawakuweza kuamini kwamba yeye amekuwa mfuasi.

9:27 Hapo, Barnaba alikuja akamchukua Saulo, akampeleka kwa mitume na kuwaeleza jinsi Saulo alivyomwona Bwana njiani na jinsi Bwana alivyoongea naye. Aliwaambia pia jinsi Saulo alivyokuwa amehubiri bila uoga kule Damasko.

9:28 Basi, Saulo alikaa pamoja nao, akatembelea Yerusalemu yote akihubiri neno la Bwana bila hofu.

9:29 Pia aliongea na kubishana na Wayahudi wasemao Kigiriki, lakini wao walijaribu kumwua.

9:30 Wale ndugu walipogundua jambo hilo walimchukua Saulo, wakampeleka Kaisarea, wakamwacha aende zake Tarso.

9:31 Wakati huo kanisa likawa na amani popote katika Yudea, Galilaya, na Samaria. Lilijengwa na kukua katika kumcha Bwana, na kuongezeka likitiwa moyo na Roho Mtakatifu.

9:32 Petro alipokuwa anasafirisafiri kila mahali alifika pia kwa watu wa Mungu waliokuwa wanaishi Luda.

9:33 Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Enea ambaye kwa muda wa miaka minane alikuwa amelala kitandani kwa sababu alikuwa amepooza.

9:34 Basi, Petro akamwambia, "Enea, Yesu Kristo anakuponya. Amka utandike kitanda chako." Enea akaamka mara.

9:35 Wakazi wote wa Luda na Saroni walimwona Enea, na wote wakamgeukia Bwana.

9:36 Kulikuwa na mfuasi mmoja mwanamke mjini Yopa aitwaye Tabitha (kwa Kigiriki ni Dorka, maana yake, Paa). Huyo mwanamke alikuwa akitenda mema na kuwasaidia maskini daima.

9:37 Wakati huo ikawa kwamba aliugua, akafa. Watu wakauosha mwili wake, wakauzika katika chumba ghorofani.

9:38 Yopa si mbali sana na Luda; kwa hiyo wafuasi waliposikia kwamba Petro alikuwa Luda, wakawatuma watu wawili kwake na ujumbe: "Njoo kwetu haraka iwezekanavyo."

9:39 Basi, Petro akaenda pamoja nao. Alipofika alipelekwa ghorofani katika kile chumba. Huko wajane wengi walimzunguka Petro wakilia na kumwonyesha makoti na nguo ambazo Dorka alikuwa akitengeneza wakati alipokuwa hai.

9:40 Petro aliwatoa nje wote, akapiga magoti, akasali. Kisha akamgeukia yule maiti, akasema, "Tabitha, amka" Naye akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi.

9:41 Petro akamsaidia kusimama, halafu akawaita wale watu wa Mungu na wale wajane, akamkabidhi kwao akiwa mzima.

9:42 Habari ya tukio hili ilienea kila mahali huko Yopa, na watu wengi wakamwamini Bwana.

9:43 Petro alikaa siku kadhaa huko Yopa, akiishi kwa mtu mmoja mtengenezaji wa ngozi aitwaye Simoni.

10:1 Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, Jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho "Kikosi cha Italia."

10:2 Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima.

10:3 Yapata saa tisa mchana, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, "Kornelio!"

10:4 Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, "Kuna nini Mheshimiwa?" Huyo malaika akamwambia, "Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini.

10:5 Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro.

10:6 Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari."

10:7 Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu,

10:8 akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa.

10:9 Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali.

10:10 Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, alipatwa na usingizi mzito akaona maono.

10:11 Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne.

10:12 Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani.

10:13 Akasikia sauti ikimwambia: "Petro, amka uchinje, ule!"

10:14 Petro akajibu, "La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu."

10:15 Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: "Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!"

10:16 Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni.

10:17 Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hilo maono alilokuwa ameliona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni,

10:18 Wakaita kwa sauti: "Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?"

10:19 Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa lile maono, na hapo Roho akamwambia, "Sikiliza! kuna watu watatu hapa, wanakutafuta.

10:20 Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma."

10:21 Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, "Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?"

10:22 Wao wakamjibu, "Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema."

10:23 Petro akawaalika ndani, akawapa mahali pa kulala usiku ule. Kesho yake, Petro alianza safari pamoja nao, na baadhi ya ndugu wa huko Yopa walifuatana naye.

10:24 Siku ya pili yake, walifika Kaisarea na huko Kornelio alikuwa anawangojea pamoja na jamaa na marafiki aliokuwa amewaalika.

10:25 Petro alipokuwa anaingia, Kornelio alitoka nje kumlaki, akapiga magoti mbele yake na kuinama chini kabisa.

10:26 Lakini Petro alimwinua, akamwambia, "Simama, kwa maana mimi ni binadamu tu."

10:27 Petro aliendelea kuongea na Kornelio wakiwa wanaingia nyumbani ambamo aliwakuta watu wengi wamekusanyika.

10:28 Petro akawaambia, "Ninyi wenyewe mnajua kwamba Myahudi yeyote amekatazwa na Sheria yake ya dini kushirikiana na watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amenijulisha nisimfikirie mtu yeyote kuwa najisi au mchafu.

10:29 Kwa sababu hiyo, mliponiita nimekuja bila kusita. Basi, nawaulizeni: kwa nini mmeniita?"

10:30 Kornelio akasema, "Siku tatu zilizopita saa kama hii, saa tisa alasiri, nilikuwa nikisali chumbani mwangu. Ghafla, mtu aliyekuwa amevaa mavazi yenye kun'gaa alisimama mbele yangu,

10:31 akasema: Kornelio! Sala yako na sadaka zako kwa maskini vimekubaliwa na Mungu.

10:32 Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petroi; yuko nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi karibu na bahari.

10:33 Kwa hiyo nilikutumia ujumbe bila kuchelewa, nawe umefanya vyema kuja. Sasa, sisi tuko mbele ya Mungu, kusikiliza chochote ambacho bwana amekuamuru kusema."

10:34 Hapo Petro akaanza kusema: "Sasa nimetambua kwamba hakika Mungu hana ubaguzi.

10:35 Mtu wa taifa lolote anayemcha Mungu na kutenda haki anapokelewa naye.

10:36 Huu ndio ule ujumbe Mungu alioupeleka kwa watu wa Israeli, akitangaza Habari Njema iletayo amani kwa njia ya Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote.

10:37 Ninyi mnajua jambo lililotukia katika nchi yote ya Wayahudi kuanzia Galilaya baada ya ule ubatizo aliohubiri Yohane.

10:38 Mnajua Yesu wa Nazareti na jinsi Mungu alivyomteua kwa kummiminia Roho Mtakatifu na nguvu. Mungu alikuwa pamoja naye; yeye alikwenda huko na huko akitenda mema na kuwaponya wote waliokuwa wamevamiwa na Ibilisi.

10:39 Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyotenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu. Walimuua kwa kumtundika msalabani;

10:40 lakini Mungu alimfufua siku ya tatu, akamfanya aonekane

10:41 si kwa watu wote ila kwa wale Mungu aliokwisha wachagua wawe mashahidi wake, yaani sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka wafu.

10:42 Alituamuru kuihubiri Habari Njema kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyeteuliwa na Mungu awe Mwamuzi wa wazima na wafu.

10:43 Manabii wote waliongea juu yake kwamba kila mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake."

10:44 Wakati Petro alipokuwa bado anasema maneno hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanasikiliza ujumbe huo.

10:45 Wale Wayahudi waumini waliokuja pamoja na Petro kutoka Yopa walishangaa kuona kuwa Mungu aliwamiminia zawadi ya Roho Mtakatifu watu wa mataifa mengine pia;

10:46 maana waliwasikia wakiongea kwa lugha mbalimbali wakimtukuza Mungu. Hapo Petro akasema,

10:47 "Watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi wenyewe tulivyompokea. Je, kuna yeyote atakayeweza kuwazuia wasibatizwe kwa maji?"

10:48 Basi, akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba akae nao kwa siku chache.

11:1 Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu.

11:2 Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema:

11:3 "Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao!

11:4 Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo:

11:5 "Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa likishushwa chini kutoka mbinguni likiwa limeshikwa pembe zake nne, likawekwa kando yangu.

11:6 Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani.

11:7 Kisha nikasikia sauti ikiniambia: Petro amka, chinja, ule.

11:8 Lakini mimi nikasema: La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.

11:9 Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.

11:10 Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni.

11:11 Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba niliyokuwa nakaa.

11:12 Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio.

11:13 Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro.

11:14 Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.

11:15 Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali.

11:16 Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: Yohane alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.

11:17 Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine zawadi ileile aliyotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?"

11:18 Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, "Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu na kuwa na uzima!"

11:19 Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu.

11:20 Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria ile Habari Njema juu ya Bwana Yesu.

11:21 Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana.

11:22 Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia.

11:23 Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana.

11:24 Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana.

11:25 Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo

11:26 Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na lile kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko, kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo.

11:27 Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu.

11:28 Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote (Njaa hiyo ilitokea wakati Klaudio alipokuwa akitawala).

11:29 Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea.

11:30 Basi, wakafanya hivyo na kupeleka mchango wao kwa wazee wa kanisa kwa mikono ya Barnaba na Saulo.

12:1 Karibu wakati huohuo, mfalme Herode alianza kuwatesa baadhi ya Wakristo.

12:2 Alimwua kwa upanga Yakobo ndugu yake Yohane.

12:3 Alipoona kuwa kitendo hiki kiliwapendeza Wayahudi, aliendelea, akamkamata Petro. (Hiyo ilifanyika wakati wa sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu.)

12:4 Baada ya kutiwa nguvuni, Petro alifungwa gerezani, akawekwa chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari wannewanne. Herode alikusudia kumtoa hadharani baada ya sikukuu ya Pasaka.

12:5 Basi, Petro alipokuwa gerezani, kanisa lilikuwa linamwombea kwa Mungu kwa moyo.

12:6 Usiku, kabla ya siku ile ambayo Herode angemtoa Petro hadharani, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili. Alikuwa amefungwa minyororo miwili, na walinzi walikuwa wanalinda lango la gereza.

12:7 Ghafla, malaika wa Bwana akasimama karibu naye na mwanga ukaangaza kile chumba cha gereza. Malaika akamgusa akisema, "Amka upesi!" Mara ile minyororo ikaanguka kutoka katika mikono yake.

12:8 Malaika akamwambia, "Jifunge mshipi wako, vaa viatu vyako." Akafanya hivyo. Kisha huyo malaika akamwambia, "Vaa koti lako, unifuate."

12:9 Petro akamfuata nje lakini hakujua kama hayo yaliyofanywa na huyo malaika yalikuwa ya kweli; alidhani alikuwa anaota ndoto.

12:10 Walipita kituo cha kwanza cha ulinzi na cha pili, halafu wakafika kwenye mlango wa chuma wa kuingilia mjini. Huo mlango ukawafungukia wenyewe, nao wakatoka nje. Wakawa wanatembea katika barabara moja na mara yule malaika akamwacha Petro peke yake.

12:11 Hapo ndipo Petro alipotambua yaliyotukia, akasema, "Sasa najua kwa hakika kwamba Bwana amemtuma malaika wake akaniokoa kutoka katika mkono wa Herode na kutoka katika mambo yale yote watu wa Israeli waliyotazamia."

12:12 Alipotambua hivyo alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Maria mama yake Yohane aitwaye Marko. Humo watu wengi walikuwa wamekusanyika wakisali.

12:13 Petro alibisha mlango wa nje na mtumishi mmoja msichana aitwaye Roda, akaenda mlangoni kuitikia.

12:14 Huyo msichana aliitambua sauti ya Petro akafurahi mno, hata badala ya kuufungua ule mlango, akakimbilia ndani na kuwaambia kwamba Petro alikuwa amesimama nje mlangoni.

12:15 Wakamwambia yule msichana, "Una wazimu!" Lakini yeye akasisitiza kwamba ilikuwa kweli. Nao wakamwambia, "Huyo ni malaika wake."

12:16 Wakati huo Petro alikuwa anaendelea kupiga hodi. Mwishowe walifungua mlango, wakamwona, wakashangaa.

12:17 Petro aliwaashiria kwa mkono wakae kimya, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Kisha akawaambia watoe taarifa ya jambo hilo kwa Yakobo na wale ndugu wengine, halafu akatoka akaenda mahali pengine.

12:18 Kulipokucha, ulitokea wasiwasi mkubwa kati ya wale askari kuhusu yaliyokuwa yamempata Petro.

12:19 Herode aliamuru ufanywe msako lakini hawakuweza kumpata. Hivyo aliamuru wale askari wahojiwe, akatoa amri wauawe. Halafu akatoka huko Yudea akaenda Kaisarea ambako alikaa.

12:20 Herode alikasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Lakini wao walimpelekea wajumbe. Nao wakafaulu kwanza kumpata Blasto awe upande wao. Blasto alikuwa msimamizi mkuu wa ikulu ya mfalme. Kisha, wakamwendea Herode wakamwomba kuwe na amani, kwa maana nchi yao ilitegemea nchi ya mfalme kwa chakula.

12:21 Siku moja iliyochaguliwa, Herode akiwa amevaa mavazi rasmi na kuketi katika kiti cha kifalme aliwahutubia watu.

12:22 Wale watu walimpigia kelele za shangwe wakisema, "Hii ni sauti ya mungu, si ya mtu."

12:23 Papo hapo malaika wa Bwana akamwangusha Herode chini kwa sababu hakumpa Mungu hizo sifa. Akaliwa na wadudu, akafa.

12:24 Neno la Mungu likazidi kuenea na kukua.

12:25 Baada ya Barnaba na Saulo kutekeleza shughuli zao, walitoka tena Yerusalemu wakamchukua Yohane aitwaye pia Marko.

13:1 Katika kanisa la Antiokia kulikuwa na watu wengine waliokuwa manabii na walimu; miongoni mwao akiwa Barnaba, Simoni aitwaye pia Mweusi, Lukio wa Kurene, Manaeni ambaye alikuwa amelelewa pamoja na mfalme Herode, na Saulo.

13:2 Walipokuwa wanafanya ibada yao kwa Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu alisema: "Niteulieni Barnaba na Saulo kwa ajili ya kazi niliyowaitia."

13:3 Basi, baada ya kusali na kufunga zaidi, wakawawekea mikono, wakawaacha waende zao.

13:4 Basi, Barnaba na Saulo walipokwisha tumwa na Roho Mtakatifu, walishuka hadi Seleukia, na kutoka huko walipanda meli hadi kisiwa cha Kupro.

13:5 Walipofika Salami walihubiri neno la Mungu katika masunagogi ya Kiyahudi. Yohane (Marko) alikuwa msaidizi wao.

13:6 Walitembea toka upande mmoja wa kisiwa mpaka Pafo upande wa pili, na huko walimkuta mchawi mmoja Myahudi aitwaye Baryesu ambaye alijisingizia kuwa nabii.

13:7 Huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mkuu wa kile kisiwa, ambaye alikuwa mtu mwelewa sana. Sergio Paulo aliwaita Barnaba na Saulo ili asikie neno la Mungu.

13:8 Lakini huyo mchawi Elima (kama alivyokuwa anaitwa kwa Kigiriki), alijaribu kuwapinga ili kumzuia huyo mkuu wa kisiwa asije akaigeukia imani ya Kikristo.

13:9 Basi, Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho huyo mchawi,

13:10 akasema, "Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka.

13:11 Sasa, mkono wa Bwana utakuadhibu: utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa kitambo." Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda huku na huku akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze.

13:12 Yule mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa muumini; akastaajabia sana mafundisho aliyosikia juu ya Bwana.

13:13 Kutoka Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia; lakini Yohane (Marko) aliwaacha, akarudi Yerusalemu.

13:14 Lakini wao waliendelea na safari toka Pisga hadi mjini Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya Sunagogi, wakakaa.

13:15 Baada ya masomo katika kitabu cha Sheria ya Mose na katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu: "Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni."

13:16 Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza kuongea: "Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni!

13:17 Mungu wa taifa hili la Israeli aliwateua babu zetu na kuwafanya wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko kwa uwezo wake mkuu.

13:18 Aliwavumilia kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani.

13:19 Aliyaangamiza mataifa ya nchi ya Kanaani akawapa hao watu wake ile nchi kuwa mali yao.

13:20 Miaka mia nne na hamsini ilipita, halafu akawapatia waamuzi wawaongoze mpaka wakati wa nabii Samweli.

13:21 Hapo wakapendelea kuwa na mfalme, na Mungu akawapa Saulo, mtoto wa Kishi wa kabila la Benyamini, awe mfalme wao kwa muda wa miaka arobaini.

13:22 Baada ya kumwondoa Saulo, Mungu alimteua Daudi kuwa mfalme wao. Mungu alionyesha kibali chake kwake akisema: Nimemwona Daudi mtoto wa Yese; ni mtu anayepatana na moyo wangu; mtu ambaye atatimiza yale yote ninayotaka kuyatenda.

13:23 Kutokana na ukoo wake mtu huyu, Mungu, kama alivyoahidi, amewapelekea watu wa Israeli Mwokozi, ndiye Yesu.

13:24 Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa.

13:25 Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake aliwaambia watu: Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu na mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake.

13:26 "Ndugu, ninyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu.

13:27 Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi. Wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu Yesu adhabu ya kifo.

13:28 Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe, walimwomba Pilato amhukumu auawe.

13:29 Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini.

13:30 Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu.

13:31 Naye, kwa siku nyingi aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli.

13:32 Sisi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi tulio wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka wafu.

13:33 Kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili: Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.

13:34 Na juu ya kumfufua kutoka wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi: Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi.

13:35 Naam, na katika sehemu nyingine za zaburi asema: Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.

13:36 Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza mapenzi ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza.

13:37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza.

13:38 Jueni wazi, ndugu zangu, kwamba ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu kwa njia ya Yesu Kristo;

13:39 na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya Sheria ya Mose.

13:40 Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii:

13:41 Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni."

13:42 Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika ile sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee zaidi juu ya mambo hayo.

13:43 Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu.

13:44 Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule mji alikuja kusikiliza neno la Bwana.

13:45 Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana.

13:46 Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari zaidi, wakasema, "Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni ninyi kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uzima wa milele, basi, tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine.

13:47 Maana Bwana alituagiza hivi: Nimekuteua wewe uwe mwanga kwa mataifa, uwe njia ya wokovu kwa ulimwengu wote."

13:48 Watu wa mataifa mengine waliposikia jambo hilo walifurahi, wakausifu ujumbe wa Mungu; na wale waliokuwa wamechaguliwa kupata uzima wa milele, wakawa waumini.

13:49 Neno la Bwana likaenea kila mahali katika sehemu ile.

13:50 Lakini Wayahudi waliwachochea wanawake wa tabaka ya juu wa mataifa mengine ambao walikuwa wacha Mungu, na wanaume maarufu wa mji huo. Wakaanza kuwatesa Paulo na Barnaba, wakawafukuza kutoka katika eneo lao.

13:51 Basi, mitume wakayakung'uta mavumbi yaliyokuwa katika miguu yao kama onyo, kisha wakaenda Ikonio.

13:52 Lakini hao wafuasi walikuwa wamejaa furaha na Roho Mtakatifu.

14:1 Kule Ikonio, mambo yalikuwa kama yalivyokuwa kule Antiokia; Paulo na Barnaba walikwenda katika sunagogi la Wayahudi wakaongea kwa uhodari hata Wayahudi wengi na Wagiriki wakawa waumini.

14:2 Lakini Wayahudi wengine waliokataa kuwa waumini walichochea na kutia chuki katika mioyo ya watu wa mataifa mengine ili wawapinge hao ndugu.

14:3 Paulo na Barnaba waliendelea kukaa huko kwa muda mrefu. Waliongea kwa uhodari juu ya Bwana, naye Bwana akathibitisha ukweli wa ujumbe walioutoa juu ya neema yake, kwa kuwawezesha kutenda miujiza na maajabu.

14:4 Watu wa mji huo waligawanyika: wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa upande wa mitume.

14:5 Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe.

14:6 Mitume walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na katika sehemu za jirani,

14:7 wakawa wanahubiri Habari Njema huko.

14:8 Kulikuwa na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa amelemaa miguu tangu kuzaliwa, na alikuwa hajapata kutembea kamwe.

14:9 Mtu huyo alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa,

14:10 akasema kwa sauti kubwa, "Simama wima kwa miguu yako!" Huyo mtu aliyelemaa akainuka ghafla, akaanza kutembea.

14:11 Umati wa watu walipoona alichofanya Paulo, ulianza kupiga kelele kwa lugha ya Kilukaonia: "Miungu imetujia katika sura za binadamu!"

14:12 Barnaba akaitwa Zeu, na Paulo, kwa vile yeye ndiye aliyekuwa anaongea, akaitwa Herme.

14:13 Naye kuhani wa hekalu la Zeu lililokuwa nje ya mji akaleta fahali na shada za maua mbele ya mlango mkuu wa mji, na pamoja na ule umati wa watu akataka kuwatambikia mitume.

14:14 Barnaba na Paulo walipopata habari hiyo waliyararua mavazi yao na kukimbilia katika lile kundi la watu wakisema kwa sauti kubwa:

14:15 "Ndugu, kwa nini mnafanya mambo hayo? Sisi pia ni binadamu kama ninyi. Na, tuko hapa kuwahubirieni Habari Njema, mpate kuziacha hizi sanamu tupu, mkamgeukie Mungu aliye hai, Mungu aliyeumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo.

14:16 Zamani Mungu aliruhusu kila taifa lifanye lilivyopenda.

14:17 Hata hivyo, Mungu hakuacha kujidhihirisha kwa mambo mema anayowatendea: huwanyeshea mvua toka angani, huwapa mavuno kwa wakati wake, huwapa chakula na kuijaza mioyo yenu furaha."

14:18 Ingawa walisema hivyo haikuwa rahisi kuwazuia wale watu wasiwatambikie.

14:19 Lakini Wayahudi kadhaa walikuja kutoka Antiokia na Ikonio, wakawafanya watu wajiunge nao, wakampiga mawe Paulo na kumburuta hadi nje ya mji wakidhani amekwisha kufa.

14:20 Lakini waumini walipokusanyika na kumzunguka, aliamka akarudi mjini. Kesho yake, yeye pamoja na Barnaba walikwenda Derbe.

14:21 Baada ya Paulo na Barnabas kuhubiri Habari Njema huko Derbe na kupata wafuasi wengi, walifunga safari kwenda Antiokia kwa kupitia Lustra na Ikonio.

14:22 Waliwaimarisha waumini wa miji hiyo na kuwatia moyo wabaki imara katika imani. Wakawaambia, "Ni lazima sisi sote tupitie katika taabu nyingi ili tuingie katika ufalme wa Mungu."

14:23 Waliteua wazee katika kila kanisa kwa ajili ya waumini, na baada ya kusali na kufunga, wakawaweka chini ya ulinzi wa Bwana ambaye walikuwa wanamwamini.

14:24 Baada ya kupitia katika nchi ya Pisidia, walifika Pamfulia.

14:25 Baada ya kuhubiri ule ujumbe huko Perga, walikwenda Atalia.

14:26 Kutoka huko walisafiri kwa meli wakarudi Antiokia ambako hapo awali walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi wa neema ya Mungu kwa ajili ya kazi ambayo sasa walikuwa wameitimiza.

14:27 Walipofika huko Antiokia walifanya mkutano wa kanisa la mahali hapo, wakawapa taarifa juu ya mambo Mungu aliyofanya pamoja nao, na jinsi alivyowafungulia mlango watu wa mataifa mengine mlango wa kuingia katika imani.

14:28 Wakakaa pamoja na wale waumini kwa muda mrefu.

15:1 Basi, watu wengine walifika Antiokia kutoka Yudea wakaanza kuwafundisha wale ndugu wakisema, "Kama hamtatahiriwa kufuatana na mapokeo ya Sheria ya Mose, hamtaweza kuokolewa."

15:2 Jambo hili lilisababisha ubishi mkubwa, na baada ya Paulo na Barnaba kujadiliana nao, ikaamuliwa Paulo na Barnaba pamoja na waumini kadhaa wa lile kanisa la Antiokia waende Yerusalemu kuwaona wale mitume na wazee kuhusu jambo hilo.

15:3 Basi, kanisa liliwaaga, nao walipokuwa wanapitia Foinike na Samaria waliwaeleza watu jinsi mataifa mengine yalivyomgeukia Mungu. Habari hizo zikawafurahisha sana ndugu hao wote.

15:4 Walipofika Yerusalemu walikaribishwa na kanisa, mitume na wazee; nao wakawapa taarifa juu ya yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.

15:5 Lakini waumini wengine waliokuwa wa kikundi cha Mafarisayo walisimama, wakasema, "Ni lazima watu wa mataifa mengine watahiriwe na kufundishwa kuifuata Sheria ya Mose."

15:6 Basi, mitume na wazee walifanya mkutano maalum wa kuchunguza jambo hilo.

15:7 Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema, "Ndugu zangu, ninyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua mimi miongoni mwenu niihubiri Habari Njema, ili watu wa mataifa wapate kusikia na kuamini.

15:8 Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.

15:9 Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani.

15:10 Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba?

15:11 Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tunaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu."

15:12 Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine.

15:13 Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: "Ndugu zangu, nisikilizeni!

15:14 Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake.

15:15 Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:

15:16 Baada ya mambo haya nitarudi. Nitaijenga tena ile nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitayatengeneza magofu yake na kuijenga tena.

15:17 Hapo watu wengine wote, watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu, watamtafuta Bwana.

15:18 Ndivyo asemavyo Bwana, aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.

15:19 "Kwa hiyo, uamuzi wangu ni huu: tusiwataabishe watu wa mataifa wanomgeukia Mungu.

15:20 Bali tuwapelekee barua kuwaambia wasile vyakula vilivyotiwa najisi kwa kutambikiwa sanamu za miungu; wajiepushe na uasherati; wasile mnyama yeyote aliyenyongwa, na wasinywe damu.

15:21 Kwa maana kwa muda mrefu maneno ya Mose yamekuwa yakihubiriwa katika kila mji na kusomwa katika masunagogi yote kila siku ya Sabato."

15:22 Mitume, wazee na kanisa lote waliamua kuwachagua watu fulani miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Basi, wakamchagua Yuda aitwaye pia Barsaba, na Sila ambao wote walikuwa wanajulikana zaidi kati ya ndugu.

15:23 Wakawapa barua hii: "Sisi mitume na wazee, ndugu zenu, tunawasalimuni ninyi ndugu wa mataifa mengine mlioko huko Antiokia, Siria na Kilikia.

15:24 Tumesikia kwamba watu wengine kutoka huku kwetu waliwavurugeni kwa maneno yao, wakaitia mioyo yenu katika wasiwasi. Lakini wamefanya hivyo bila ya idhini yoyote kutoka kwetu.

15:25 Hivyo, tumeamua kwa pamoja kuwachagua watu kadhaa na kuwatuma kwenu pamoja na wapenzi wetu Barnaba na Paulo,

15:26 ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

15:27 Kwa hiyo, tunawatuma Yuda na Sila kwenu; hawa watawaambieni wao wenyewe haya tuliyoandika.

15:28 Basi, Roho Mtakatifu na sisi tumekubali tusiwatwike mzigo zaidi ya mambo haya muhimu:

15:29 Msile vyakula vilivyotambikiwa sanamu; msinywe damu; msile nyama ya mnyama aliyenyongwa; na mjiepushe na uasherati. Mtakuwa mmefanya vema kama mkiepa kufanya mambo hayo. Wasalaam!"

15:30 Baada ya kuwaaga, hao wajumbe walielekea Antiokia ambako waliita mkutano wa waumini, wakawapa hiyo barua.

15:31 Walipoisoma hiyo barua, maneno yake yaliwatia moyo, wakafurahi sana.

15:32 Yuda na Sila, ambao nao walikuwa manabii, walizungumza na hao ndugu kwa muda mrefu wakiwatia moyo na kuwaimarisha.

15:33 Baada ya kukaa huko kwa muda fulani, ndugu wa Antiokia waliwaaga wakiwatakia amani, kisha wakarudi kwa wale waliokuwa wamewatuma.

15:34 Lakini Sila aliamua kubaki.

15:35 Paulo na Barnaba walibaki huko Antiokia kwa muda; wakafundisha na kuhubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi.

15:36 Baada ya siku kadhaa, Paulo alimwambia Barnaba, "Turudi tukawatembelee wale ndugu katika kila mji tulikolihubiri neno la Bwana tukajionee jinsi wanavyoendelea."

15:37 Barnaba alitaka wamchukue pia Yohane aitwaye Marko.

15:38 Lakini Paulo hakupendelea kumchukua Marko, ambaye awali aliwaacha kule Pamfulia na kukataa kushiriki katika kazi yao.

15:39 Basi kukatokea ubishi mkali kati yao, na wakaachana. Barnaba akamchukua Marko, wakapanda meli kwenda Kupro.

15:40 Naye Paulo akamchagua Sila, na baada ya ndugu wa mahali hapo kumweka chini ya ulinzi wa neema ya Bwana, akaondoka.

15:41 Katika safari hiyo alipitia Siria na Kilikia akiyaimarisha makanisa.

16:1 Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki.

16:2 Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio.

16:3 Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki.

16:4 Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie.

16:5 Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku.

16:6 Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia.

16:7 Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu.

16:8 Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa.

16:9 Usiku huo, Paulo aliona ono ambalo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: "Vuka, uje Makedonia ukatusaidie."

16:10 Mara baada ya Paulo kuona ono hilo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwapelekee Habari Njema.

16:11 Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli.

16:12 Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa.

16:13 Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo.

16:14 Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema.

16:15 Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, "Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae." Akatuhimiza twende.

16:16 Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake.

16:17 Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, "Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu."

16:18 Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, "Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!" Mara huyo pepo akamtoka.

16:19 Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu.

16:20 Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, "Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu.

16:21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata."

16:22 Kundi la watu likajiunga nao, likawashambulia. Wale mahakimu wakawatatulia Paulo na Sila mavazi yao, wakaamuru wapigwe viboko.

16:23 Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali.

16:24 Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo.

16:25 Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza.

16:26 Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana.

16:27 Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua.

16:28 Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: "Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa."

16:29 Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu.

16:30 Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, "Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?"

16:31 Wao wakamjibu, "Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote."

16:32 Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake.

16:33 Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo.

16:34 Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa wanamwamini Mungu.

16:35 Kesho yake asubuhi, mahakimu waliwatuma maofisa wao wakisema, "Wafungueni wale watu."

16:36 Yule askari wa gereza alimpasha habari Paulo: "Mahakimu wametuma ujumbe ili mfunguliwe. Sasa mnaweza kutoka na kwenda zenu kwa amani."

16:37 Lakini Paulo alimjibu, "Ati nini? Ingawa hatukuwa na kosa, walitupiga viboko hadharani hali sisi ni raia wa Roma. Tena, walitutia ndani na sasa wanataka kutufungulia kwa siri! Hata kidogo! Ni lazima wao wenyewe waje hapa watufungulie."

16:38 Hao maofisa waliwapasha habari mahakimu juu ya jambo hilo, nao waliposikia kwamba Paulo na Sila walikuwa raia wa Roma, waliogopa.

16:39 Hivyo, walikwenda kuwataka radhi na baada ya kuwatoa ndani waliwaomba watoke katika mji ule.

16:40 Paulo na Sila walitoka gerezani, wakaenda nyumbani kwa Ludia. Huko walionana na ndugu waumini na baada ya kuwatia moyo wakaondoka.

17:1 Kwa kupitia Amfipoli na Apolonia, walisafiri mpaka Thesalonika ambako kulikuwa na sunagogi la Wayahudi.

17:2 Paulo alijiunga nao kama ilivyokuwa desturi yake akajadiliana nao Sabato tatu mfululizo, akatumia Maandiko Matakatifu.

17:3 Aliyaeleza na kuonyesha kwamba ilimbidi Kristo kuteswa na kufufuka kutoka wafu. Akawaambia, "Yesu ambaye mimi namhubiri kwenu ndiye Kristo."

17:4 Baadhi yao walikubali wakajiunga na Paulo na Sila. Kadhalika, idadi kubwa ya Wagiriki waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wa tabaka la juu, walijiunga nao.

17:5 Lakini Wayahudi wakaona wivu; wakawakodi wafidhuli sokoni, wakafanya kikundi na kuzusha fujo mjini kote. Wakaivamia nyumba ya Yasoni wakitumaini kuwapata humo Paulo na Sila ili wawalete hadharani.

17:6 Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: "Watu hawa wamekuwa wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini.

17:7 Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti Kuna mfalme mwingine aitwaye Yesu."

17:8 Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu.

17:9 Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao.

17:10 Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi.

17:11 Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonika. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli.

17:12 Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia.

17:13 Lakini, Wayahudi wa Thesalonika walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu.

17:14 Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea.

17:15 Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo.

17:16 Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa sanamu za miungu.

17:17 Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano sokoni pamoja na wowote wale waliojitokeza.

17:18 Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana naye. Wengine walisema, "Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?" Kwa kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema, "Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni."

17:19 Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema, "Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia.

17:20 Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani."

17:21 Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya.

17:22 Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago, akasema, "Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba ninyi, kwa vyovyote, ni watu wa dini sana.

17:23 Sababu yenyewe ni kwamba katika pitapita yangu niliangalia sanamu zenu za ibada nikakuta madhabahu moja ambayo imeandikwa: Kwa ajili ya Mungu yule Asiyejulikana. Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua, ndiye ninayemhubiri kwenu.

17:24 Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na nchi; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu.

17:25 Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na anawapa kila kitu.

17:26 Kutokana na mtu mmoja aliumba mataifa yote na kuyawezesha kuishi duniani kote. Aliamua na kupanga kabla kabisa lini na wapi mataifa hayo yangeishi.

17:27 Alifanya hivyo, ili mataifa hayo yapate kumfuata, na kama vile kwa kupapasapapasa, yapate kumfikia. Hata hivyo lakini, Mungu hayuko mbali na kila mmoja wetu.

17:28 Kama alivyosema mtu mmoja: Ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu, na tuko! Ni kama washairi wenu wengine walivyosema: Sisi ni watoto wake.

17:29 Ikiwa basi, sisi ni watoto wa Mungu, haifai kumfikiria Mungu kuwa kama dhahabu, fedha au hata jiwe lililochongwa na kutiwa nakshi na binadamu.

17:30 Mungu alifanya kama kwamba haoni nyakati zile watu walipokuwa wajinga. Lakini sasa, anaamuru watu wote kila mahali watubu.

17:31 Kwa maana amekwisha weka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki kwa njia ya mtu mmoja aliyemteua. Mungu amewathibitishia wote jambo hili kwa kumfufua mtu huyo kutoka wafu!"

17:32 Walipomsikia Paulo anasema juu ya jambo la kufufuka kwa wafu, wengine wao waliangua kicheko; lakini wengine walisema, "Tunataka kukusikia tena juu ya jambo hili!"

17:33 Hivyo, Paulo aliwaacha, akatoka barazani.

17:34 Lakini watu kadhaa waliandamana naye, wakawa waumini. Miongoni mwao walikuwa Dionisio wa Areopago, mwanamke mmoja aitwaye Damari na wengineo.

18:1 Baada ya hayo, Paulo aliondoka Athene, akaenda Korintho.

18:2 Huko Korintho, alimkuta Myahudi mmoja aitwaye Akula, mzaliwa wa Ponto. Akula pamoja na mkewe aitwaye Priskila, walikuwa wamerudi kutoka Italia siku hizohizo kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Roma. Paulo alikwenda kuwaona,

18:3 na kwa vile wao walikuwa mafundi wa kushona mahema kama alivyokuwa yeye, Paulo alikaa nao akafanya kazi.

18:4 Kila Sabato alifanya majadiliano katika sunagogi akijaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki.

18:5 Baada ya Sila na Timotheo kuwasili kutoka Makedonia, Paulo alianza kutumia wakati wake wote kwa ajili ya kuhubiri, akawathibitishia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo.

18:6 Walipompinga na kuanza kumtukana, aliyakung'uta mavazi yake mbele yao akisema, "Mkipotea ni shauri lenu wenyewe; mimi sina lawama yoyote juu ya jambo hilo. Na tangu sasa nitawaendea watu na mataifa mengine."

18:7 Basi, akatoka hapo akaenda kukaa nyumbani kwa mtu mmoja mcha Mungu aitwaye Tito Yusto. Nyumba yake Tito ilikuwa karibu na lile sunagogi.

18:8 Lakini Krispo, mkuu wa sunagogi, alimwamini Bwana yeye pamoja na jamaa yake yote. Wakorintho wengi waliusikiliza ujumbe huo, wakaamini na kubatizwa.

18:9 Siku moja usiku, Bwana alimwambia Paulo katika maono: "Usiogope, endelea kuhubiri tu bila kufa moyo,

18:10 maana mimi niko pamoja nawe. Hakuna mtu atakayejaribu kukudhuru maana hapa mjini pana watu wengi walio upande wangu."

18:11 Basi, Paulo alikaa huko akifundisha neno la Mungu kati yao kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

18:12 Lakini wakati Galio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Akaya, Wayahudi walimvamia Paulo kwa pamoja na kumpeleka mahakamani.

18:13 Wakasema, "Tunamshtaki mtu huyu kwa sababu ya kuwashawishi watu wamwabudu Mungu kwa namna inayopingana na Sheria."

18:14 Kabla tu Paulo hajaanza kusema, Galio aliwaambia Wayahudi, "Sikilizeni enyi Wayahudi! Kama kweli jambo hili lingekuwa juu ya uhalifu au uovu ningekuwa tayari kuwasikilizeni.

18:15 Lakini kama ni shauri la ubishi kuhusu maneno na majina ya Sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo haya!"

18:16 Basi, akawafukuza kutoka mahakamani.

18:17 Nao wote wakamkamata Sosthene ambaye alikuwa kiongozi wa sunagogi, wakampiga palepale mbele ya mahakama. Lakini Galio hakujali kitendo hicho hata kidogo.

18:18 Paulo alikaa bado na wale ndugu huko Korintho kwa siku nyingi. Kisha aliwaaga, akapanda meli kwenda Siria pamoja na Priskila na Akula. Huko Kenkrea, alinyoa nywele zake kwa sababu ya nadhiri aliyokuwa ameweka.

18:19 Walifika Efeso na hapo Paulo aliwaacha Priskila na Akula, akaenda katika sunagogi, akajadiliana na Wayahudi.

18:20 Walimwomba akae nao muda mrefu zaidi, lakini hakupenda.

18:21 Bali alipokuwa anaondoka, alisema, "Mungu akipenda nitakuja kwenu tena." Akaondoka Efeso kwa meli.

18:22 Meli ilitia nanga Kaisarea, naye Paulo akaenda Yerusalemu kulisalimia lile kanisa, kisha akaenda Antiokia.

18:23 Alikaa huko muda mfupi, halafu akaendelea na safari kwa kupitia sehemu za Galatia na Frugia akiwatia moyo wafuasi wote.

18:24 Myahudi mmoja aitwaye Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, alifika Efeso. Alikuwa mtu mwenye ufasaha wa kuongea na mwenye ujuzi mkubwa wa Maandiko Matakatifu.

18:25 Alikuwa amefundishwa juu ya hiyo njia ya Bwana, na akiwa motomoto, aliongea juu ya habari za Yesu. Akafundisha kwa usahihi ingawa alikuwa amepata ubatizo wa Yohane tu.

18:26 Priskila na Akula walipomsikia akiongea kwa uhodari ndani ya sunagogi, walimchukua kwao wakamfundisha hiyo Njia ya Mungu kwa usahihi zaidi.

18:27 Apolo alipoamua kwenda Akaya, wale ndugu walimtia moyo kwa kuwaandikia wafuasi kule Akaya wampokee. Alipofika huko, aliweza kwa msaada wa neema ya Mungu, kuwasaidia sana wale ndugu waliopata kuwa waumini;

18:28 kwa maana aliendelea kwa uhodari kuwashinda Wayahudi hadharani akithibitisha kwa Maandiko Matakatifu kuwa Yesu ni Kristo.

19:1 Wakati Apolo alipokuwa Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso ambako aliwakuta wanafunzi kadhaa.

19:2 Akauliza, "Je, mlipopata kuwa waumini mlipokea Roho Mtakatifu?" Nao wakamjibu, "La! Hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatujasikia."

19:3 Naye akasema, "Sasa mlipata ubatizo wa namna gani?" Wakamjibu, "Ubatizo wa Yohane."

19:4 Naye Paulo akasema, "Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa kuonyesha kwamba watu wametubu. Yohane aliwaambia watu wamwamini yule ambaye alikuwa anakuja baada yake, yaani Yesu."

19:5 Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu.

19:6 Basi, Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kusema lugha mbalimbali na kutangaza ujumbe wa Mungu.

19:7 Wote jumla, walikuwa watu wapatao kumi na wawili.

19:8 Kwa muda wa miezi mitatu Paulo alikuwa akienda katika sunagogi, akawa na majadiliano ya kuvutia sana juu ya Ufalme wa Mungu.

19:9 Lakini wengine walikuwa wakaidi, wakakataa kuamini, wakaanza kuongea vibaya hadharani juu ya Njia ya Bwana. Hapo Paulo alivunja uhusiano nao, akawachukua pembeni wale wanafunzi wake, akawa anazungumza nao kila siku katika jumba la masomo la Turano.

19:10 Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana.

19:11 Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo.

19:12 Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao.

19:13 Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya, walisafiri huko na huko, wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: "Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri."

19:14 Watoto saba wa Skewa, Kuhani Mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo.

19:15 Lakini pepo mbaya aliwajibu, "Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini ninyi ni nani?"

19:16 Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.

19:17 Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.

19:18 Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda.

19:19 Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande vya fedha elfu hamsini.

19:20 Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi.

19:21 Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, "Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia."

19:22 Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia.

19:23 Wakati huo ndipo kulipotokea ghasia kubwa huko Efeso kwa sababu ya hiyo Njia ya Bwana.

19:24 Kulikuwa na mfua fedha mmoja aitwaye Demetrio, ambaye alikuwa na kazi ya kutengeneza sanamu za nyumba ya mungu wa kike aitwaye Artemi. Shughuli hiyo iliwapatia mafundi faida kubwa.

19:25 Demetrio aliwakusanya hao wafanyakazi pamoja na wengine waliokuwa na kazi kama hiyo, akawaambia, "Wananchi, mnafahamu kwamba kipato chetu kinatokana na biashara hii.

19:26 Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si tu hapa Efeso, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo.

19:27 Hivyo iko hatari kwamba biashara yetu itakuwa na jina baya. Si hivyo tu, bali pia jambo hilo linaweza kuifanya nyumba ya mungu Artemi kuwa si kitu cha maana. Hatimaye sifa zake huyo ambaye Asia na dunia yote inamwabudu, zitakwisha."

19:28 Waliposikia hayo, waliwaka hasira, wakaanza kupiga kelele: "Mkuu ni Artemi, wa Efeso!"

19:29 Mji wote ukajaa ghasia. Wakawavamia Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia, ambao walikuwa wasafiri wenzake Paulo, wakakimbia nao mpaka kwenye ukumbi wa michezo.

19:30 Paulo mwenyewe alitaka kuukabili huo umati wa watu, lakini wale waumini walimzuia.

19:31 Maofisa wengine wa huo mkoa wa Asia, waliokuwa rafiki zake, walimtumia Paulo ujumbe wakimsihi asijihatarishe kwa kwenda kwenye ukumbi wa michezo.

19:32 Wakati huo, kila mtu alikuwa anapayuka; wengine hili na wengine lile, mpaka hata ule mkutano ukavurugika. Wengi hawakujua hata sababu ya kukutana kwao.

19:33 Kwa vile Wayahudi walimfanya Aleksanda ajitokeze mbele, baadhi ya watu katika ule umati walidhani kuwa ndiye. Basi, Aleksanda aliwaashiria watu kwa mkono akitaka kujitetea mbele ya ule umati wa watu.

19:34 Lakini walipotambua kuwa yeye ni Myahudi, wote kwa sauti moja walipiga kelele: "Mkuu ni Artemi wa Efeso!" Wakaendelea kupayukapayuka hivyo kwa muda wa saa mbili.

19:35 Hatimaye karani wa mji alifaulu kuwanyamazisha, akawaambia, "Wananchi wa Efeso, kila mtu anajua kwamba mji huu wa Efeso ni mlinzi wa nyumba ya mungu Artemi na mlinzi wa ile sanamu iliyoanguka kutoka mbinguni.

19:36 Hakuna anayeweza kukana mambo haya. Hivyo basi, tulieni; msifanye chochote bila hadhari.

19:37 Mmewaita watu hawa hapa ingawaje hawakuikufuru nyumba ya mungu wala kumtukana mungu wetu wa kike.

19:38 Kama, basi Demetrio na wafanyakazi wake wana mashtaka yao kuhusu watu hawa, yapo mahakama na wakuu wa mikoa; wanaweza kushtakiana huko.

19:39 Kama mna matatizo mengine, yapelekeni katika kikao halali.

19:40 Kwa maana tungaliweza kushtakiwa kwa kusababisha ghasia kutokana na vituko vya leo. Ghasia hii haina msingi halali na hatungeweza kutoa sababu za kuridhisha za ghasia hiyo."

19:41 Baada ya kusema hayo aliuvunja mkutano.

20:1 Ile ghasia ya Efeso ilipokwisha tulia Paulo aliwaita pamoja wale waumini, akawatia moyo. Kisha akawaaga, akasafiri kwenda Makedonia.

20:2 Alipitia sehemu za nchi zile akiwatia watu moyo kwa maneno mengi. Halafu akafika Ugiriki.

20:3 ambako alikaa kwa miezi mitatu. Alipokuwa anajitayarisha kwenda Siria, aligundua kwamba Wayahudi walikuwa wanamfanyia mpango mbaya; hivyo aliamua kurudi kwa kupitia Makedonia.

20:4 Sopatro, mwana wa Pirho kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonika, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia.

20:5 Hao walitutangulia na kutungojea kule Troa.

20:6 Sisi, baada ya sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja.

20:7 Jumamosi jioni, tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane.

20:8 Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka.

20:9 Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa.

20:10 Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, "Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake."

20:11 Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka.

20:12 Wale watu walimchukua yule kijana nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa.

20:13 Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu.

20:14 Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene.

20:15 Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto.

20:16 Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana.

20:17 Kutoka Mileto Paulo alituma ujumbe kwa wazee wa Efeso wakutane naye.

20:18 Walipofika kwake aliwaambia, "Mnajua jinsi nilivyotumia wakati wote pamoja nanyi tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia.

20:19 Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi.

20:20 Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni.

20:21 Niliwaonya wote--Wayahudi kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu.

20:22 Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko.

20:23 Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea.

20:24 Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa ni kitu sana kwangu. Nataka tu nikamilishe ule utume wangu na kumaliza ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nitangaze Habari Njema ya neema ya Mungu.

20:25 "Nimekuwa nikienda huko na huko kati yenu nikiuhubiri Ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu atakayeniona tena.

20:26 Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote.

20:27 Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio lote la Mungu.

20:28 Jihadharini wenyewe; lilindeni lile kundi ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi muwe walezi wake. Lichungeni kanisa la Mungu ambalo amejipatia kwa damu ya Mwanae.

20:29 Nafahamu vizuri sana kwamba baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali watawavamieni, na hawatakuwa na huruma kwa kundi hilo.

20:30 Hata kutoka miongoni mwenu watatokea watu ambao watasema mambo ya uongo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate wao tu.

20:31 Kwa hiyo, muwe macho mkikumbuka kwamba kwa muda wa miaka mitatu, usiku na mchana, sikuchoka kumwonya kila mmoja wenu kwa machozi.

20:32 "Na sasa basi, ninawaweka ninyi chini ya ulinzi wa Mungu na ujumbe wa neema yake. Yeye anao uwezo wa kuwajenga ninyi na kuwawezesha mzipate zile baraka alizowawekea watu wake.

20:33 Mimi sikutamani hata mara moja fedha, wala dhahabu, wala nguo za mtu yeyote.

20:34 Mnajua ninyi wenyewe kwamba nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe, ili kujipatia mahitaji yangu na ya wenzangu.

20:35 Nimekuwa nikiwapeni daima mfano kwamba kwa kufanya kazi mithili hiyo tunapaswa kuwasaidia walio dhaifu, tukikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe: Heri zaidi kutoa kuliko kupokea."

20:36 Baada ya kusema hayo, Paulo alipiga magoti pamoja nao wote, akasali.

20:37 Wote walikuwa wanalia; wakamwaga kwa kumkumbatia na kumbusu.

20:38 Jambo lililowahuzunisha zaidi lilikuwa neno alilosema kwamba hawangemwona tena. Basi, wakamsindikiza hadi melini.

21:1 Tulipokwisha agana nao, tulipanda meli tukaenda moja kwa moja mpaka Kosi. Kesho yake tulifika Rodo, na kutoka huko tulikwenda Patara.

21:2 Huko, tulikuta meli iliyokuwa inakwenda Foinike, hivyo tulipanda, tukasafiri.

21:3 Baada ya kufika mahali ambapo tuliweza kuona Kupro, tulipitia upande wake wa kusini tukaelekea Siria. Tulitia nanga katika mji wa Tiro ambapo ile meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake.

21:4 Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa waongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.

21:5 Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali.

21:6 Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli nao wakarudi makwao.

21:7 Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja.

21:8 Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko Kaisarea tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu.

21:9 Alikuwa na binti watatu ambao walikuwa na kipaji cha unabii.

21:10 Baada ya kukaa huko siku kadhaa, nabii mmoja aitwaye Agabo alifika kutoka Yudea.

21:11 Alitujia, akachukua mkanda wa Paulo, akajifunga mikono na miguu, akasema "Roho Mtakatifu asema hivi: Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga namna hii mtu mwenye ukanda na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa."

21:12 Tuliposikia hayo, sisi na wale watu wengine waliokuwa hapo tulimsihi Paulo asiende Yerusalemu.

21:13 Lakini yeye alijibu, "Mnataka kufanya nini? Mnataka kuvunja moyo wangu kwa machozi? Niko tayari siyo tu kutiwa ndani kule Yerusalemu, ila hata kufa kwa ajili ya Bwana Yesu."

21:14 Tuliposhindwa kumshawishi tulinyamaza, tukasema tu: "Mapenzi ya Bwana yafanyike"

21:15 Baada ya kukaa pale kwa muda, tulifunga mizigo yetu, tukaendelea na safari kwenda Yerusalemu.

21:16 Wengine kati ya wale wafuasi wa Kaisarea walienda pamoja nasi, wakatupeleka nyumbani kwa Mnasoni ambaye tulikuwa tunakwenda kukaa naye kwa muda. Mnasoni alikuwa mwenyeji wa Kupro na alikuwa amekuwa muumini kwa siku nyingi.

21:17 Tulipofika Yerusalemu, ndugu waumini walitupokea vizuri sana.

21:18 Kesho yake Paulo alikwenda pamoja nasi kumwamkia Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwako pia.

21:19 Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwapa taarifa kamili kuhusu yote Mungu aliyokuwa ametenda kati ya mataifa kwa njia ya utumishi wake.

21:20 Waliposikia hayo, walimtukuza Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, "Ndugu, unaweza kuona kwamba kuna maelfu ya Wayahudi ambao sasa wamekuwa waumini na wote hao wanashika kwa makini Sheria ya Mose.

21:21 Wamepata habari zako kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wanaoishi kati ya mataifa mengine kuwa wasiijali Sheria ya Mose, wasiwatahiri watoto wao na kwamba wasizifuate mila za Wayahudi.

21:22 Sasa, mambo yatakuwaje? Ni dhahiri kuwa watapata habari kwamba umekwisha wasili hapa.

21:23 Basi, fanya kama tunavyokushauri. Tunao hapa watu wanne ambao wameweka nadhiri.

21:24 Jiunge nao katika ibada ya kujitakasa, ukalipe na gharama zinazohusika, kisha wanyolewe nywele zao. Hivyo watu wote watatambua kwamba habari zile walizoambiwa juu yako hazina msingi wowote, na kwamba wewe binafsi bado unaishi kufuatana na maagizo ya Sheria za Mose.

21:25 Kuhusu wale watu wa mataifa mengine ambao wamekuwa waumini, tumekwisha wapelekea barua tukiwaambia mambo tuliyoamua: wasile chochote kilichotambikiwa miungu ya uongo, wasinywe damu, wasile nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati."

21:26 Basi, kesho yake Paulo aliwachukua wale watu akafanya ibada ya kujitakasa pamoja nao. Kisha akaingia Hekaluni kutoa taarifa kuhusu mwisho wa siku za kujitakasa na kuhusu dhabihu itakayotolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

21:27 Wakati siku hizo saba zilipokaribia kuisha, Wayahudi waliokuwa wametoka katika mkoa wa Asia walimwona Paulo Hekaluni. Wakachochea hasira kati ya kundi lote la watu, wakamtia nguvuni

21:28 wakipiga kelele: "Wananchi wa Israeli, msaada, msaada! Huyu ndiye yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo yanayopinga watu wa Israeli, yanayopinga Sheria ya Mose na mahali hapa patakatifu. Hata sasa amewaingiza watu wa mataifa mengine Hekaluni na kupatia najisi mahali hapa patakatifu."

21:29 Sababu ya kusema hivyo ni kwamba walikuwa wamemwona Trofimo mwenyeji, wa Efeso, akiwa pamoja na Paulo mjini, wakadhani kwamba Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.

21:30 Mji wote ulienea ghasia; watu wakaja kutoka pande zote, wakamkamata Paulo, wakamburuta, wakamtoa nje ya Hekalu na papo hapo milango ya Hekalu ikafungwa.

21:31 Walikuwa tayari kumuua, lakini habari zilimfikia mkuu wa jeshi la Kiroma kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia.

21:32 Mara, mkuu wa jeshi akawachukua askari na jemadari, akalikabili lile kundi la watu. Nao walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo.

21:33 Mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamtia nguvuni na kuamuru afungwe minyororo miwili. Kisha akauliza, "Ni mtu gani huyu, na amefanya nini?"

21:34 Wengine katika lile kundi la watu walikuwa wanapayuka kitu hiki na wengine kitu kingine. Kwa sababu ya ghasia hiyo, mkuu wa jeshi hakufaulu kujua kisa kamili. Hivyo, aliamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome.

21:35 Paulo alipofika kwenye ngazi, askari walilazimika kumbeba kwa sababu ya fujo za watu.

21:36 Kwa maana kundi kubwa la watu walimfuata wakipiga kelele, "Muulie mbali!"

21:37 Walipokuwa wanamwingiza ndani ya ngome, Paulo alimwomba mkuu wa jeshi akisema, "Naweza kukwambia kitu?" Yule mkuu wa jeshi akamjibu, "Je unajua Kigiriki?

21:38 Kwani wewe si yule Mmisri ambaye hivi majuzi alianzisha uasi na kuwaongoza majahili elfu nne hadi jangwani?"

21:39 Paulo akajibu, "Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia; mimi ni raia wa mji maarufu. Tafadhali, niruhusu niongee na watu.

21:40 Yule mkuu wa jeshi akamruhusu. Hivyo Paulo alisimama juu ya ngazi, akawapungia mkono wale watu na walipokaa kimya, akaanza kuongea nao kwa Kiebrania.

22:1 "Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa nikijitetea mbele yenu!"

22:2 Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema,

22:3 "Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia. Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli. Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti Sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo wote kwa Mungu kama ninyi wenyewe mlivyo hivi leo.

22:4 Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata Njia hii. Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani.

22:5 Kuhani Mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe.

22:6 "Basi, nilipokuwa njiani karibu kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwangu mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote.

22:7 Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?

22:8 Nami nikauliza: Nani wewe, Bwana? Naye akaniambia: Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.

22:9 Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami.

22:10 Basi, mimi nikauliza: Nifanye nini Bwana? Naye Bwana akaniambia: Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.

22:11 Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko.

22:12 "Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii Sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko.

22:13 Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema: Ndugu Saulo! Ona tena. Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia.

22:14 Halafu Anania akasema: Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea.

22:15 Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia.

22:16 Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama ubatizwe na uondolewe dhambi zako kwa kuliungama jina lake.

22:17 "Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali Hekaluni, niliona maono.

22:18 Nilimwona Bwana akiniambia: Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa binadamu hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.

22:19 Nami nikamjibu: Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini.

22:20 Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.

22:21 Naye Bwana akaniambia: Nenda; ninakutuma mbali kwa mataifa mengine."

22:22 Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiza, lakini aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, "Mwondoe duniani! Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi."

22:23 Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na kurusha vumbi angani.

22:24 Mkuu wa jeshi aliwaamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome, akawaambia wamchape viboko ili wapate kujua kisa cha Wayahudi kumpigia kelele.

22:25 Lakini walipokwisha mfunga ili wamchape viboko, Paulo alimwuliza jemadari mmoja aliyesimama hapo, "Je, ni halali kwenu kumpiga viboko raia wa Roma kabla hajahukumiwa?"

22:26 Yule jemadari aliposikia hayo, alimpasha habari mkuu wa jeshi akisema, "Unataka kufanya nini? Mtu huyu ni raia wa Roma!"

22:27 Basi, mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamwambia, "Niambie; je, wewe ni raia wa Roma?" Paulo akamjibu, "Naam."

22:28 Mkuu wa jeshi akasema, "Mimi nami nimekuwa raia wa Roma kwa kulipa gharama kubwa." Paulo akasema, "Lakini mimi ni raia wa Roma kwa kuzaliwa."

22:29 Wale watu ambao walikuwa tayari kumchunguza Paulo walitoweka mara. Hata yule mkuu wa jeshi aliogopa alipojua kwamba Paulo ni raia wa Roma na kwamba alikuwa amekwisha mfunga minyororo.

22:30 Kesho yake, mkuu wa jeshi alitaka kujua mashtaka kamili ambayo Wayahudi walikuwa wamemwekea Paulo. Hivyo, alimfungua Paulo minyororo, akaamuru makuhani wakuu na Baraza lote wafanye kikao. Kisha alimleta Paulo, akamsimamisha mbele ya Baraza.

23:1 Paulo aliwakodolea macho wale wanabaraza, halafu akaanza kusema, "Ndugu zangu, mpaka hivi leo nimekuwa nikiishi na dhamiri njema mbele ya Mungu."

23:2 Hapo Kuhani Mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wampige kofi mdomoni.

23:3 Basi, Paulo akamwambia, "Mungu mwenyewe atakupiga kofi wewe uliye kama ukuta uliopakwa chokaa! Unawezaje kukaa hapo ili unihukumu kisheria na huku wewe mwenyewe unaivunja Sheria kwa kuamuru nipigwe?"

23:4 Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo, "Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu!"

23:5 Paulo akajibu, "Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni Kuhani Mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako."

23:6 Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaaza sauti yake mbele ya Baraza: "Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu watafufuka."

23:7 Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili.

23:8 Kisa chenyewe kilikuwa hiki: Masadukayo hushikilia kwamba wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo husadiki hayo yote matatu.

23:9 Kelele ziliongezeka na baadhi ya walimu wa Sheria wa kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu: "Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho au malaika ameongea naye."

23:10 Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome.

23:11 Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo, akamwambia, "Jipe moyo! Umenishuhudia katika Yerusalemu, utafanya vivyo hivyo mjini Roma."

23:12 Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: "Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo."

23:13 Watu zaidi ya arobaini ndio waliokula njama kufanya hivyo.

23:14 Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, "Sisi tumeapa kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo tutakapokuwa tumemuua Paulo.

23:15 Sasa basi, ninyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumuua hata kabla hajafika karibu."

23:16 Lakini mtoto wa kiume wa dada yake Paulo alisikia juu ya mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo.

23:17 Hapo Paulo akamwita mmoja wa askari, akamwambia, "Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia."

23:18 Askari akamchukua huyo kijana, akamwongoza mpaka kwa mkuu wa jeshi, akasema, "Yule mfungwa Paulo ameniita akaniomba nimlete kijana huyu kwako kwa maana ana jambo la kukwambia."

23:19 Mkuu wa jeshi alimshika huyo kijana mkono, akampeleka mahali pa faragha, akamwuliza, "Una nini cha kuniambia?"

23:20 Yeye akasema, "Wayahudi wamepatana wakuombe umpeleke Paulo Barazani wakijisingizia kwamba Baraza lingependa kupata habari kamili zaidi juu yake.

23:21 Lakini wewe usikubali kwa maana kuna watu zaidi ya arobaini walio tayari kumvamia. Wameapa kutokula wala kunywa mpaka watakapokuwa wamemuua. Sasa wako tayari, wanangojea tu uamuzi wako."

23:22 Mkuu wa jeshi alimwacha aende zake akimwonya asimwambie mtu yeyote kwamba amemletea habari hizo.

23:23 Basi, mkuu wa jeshi aliwaita askari wawili akawaambia, "Wekeni tayari askari mia mbili, wapanda farasi sabini na askari mia mbili wa mikuki, waende Kaisarea; muwe tayari kuondoka kabla ya saa tatu leo usiku.

23:24 Wekeni farasi kadhaa kwa ajili ya Paulo; mfikisheni salama kwa Felisi, mkuu wa mkoa."

23:25 Halafu mkuu huyo wa jeshi akaandika barua hivi:

23:26 "Mimi Klaudio Lusia ninakuandikia wewe Mheshimiwa Felisi, mkuu wa mkoa. Salamu!

23:27 "Wayahudi walimkamata mtu huyu na karibu wangemuua kama nisingalifahamishwa kwamba yeye ni raia wa Roma na hivyo nikaenda pamoja na askari nikamwokoa.

23:28 Nilimpeleka mbele ya Baraza lao kuu nikitaka kujua kisa cha mashtaka yao.

23:29 Niligundua kwamba mashtaka yenyewe yalihusu ubishi juu ya sehemu kadha wa kadha za Sheria yao na hivyo sikuona kwamba amefanya chochote kinachostahili auawe au afungwe gerezani.

23:30 Nilipofahamishwa kwamba Wayahudi walikuwa wamefanya njama za kumuua, niliamua kumleta kwako. Nikamwambia washtaki wake walete mashtaka yao mbele yako."

23:31 Basi, hao askari walimchukua Paulo kama walivyoamriwa; wakampeleka usiku uleule mpaka Antipatri.

23:32 Kesho yake askari wa miguu walirudi ngomeni, wakawaacha wale askari wapanda farasi waendelee na safari pamoja na Paulo.

23:33 Walipofika Kaisarea walimpa mkuu wa mkoa ile barua na kumweka Paulo chini ya mamlaka yake.

23:34 Felisi alipoisoma hiyo barua aliwauliza Paulo ametoka mkoa gani. Alipofahamishwa kwamba alikuwa ametoka mkoa wa Kilikia,

23:35 akasema, "Nitasikiliza kesi yako baada ya washtaki wako kufika." Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi ndani ya ukumbi wa Herode.

24:1 Baada ya siku tano, Kuhani Mkuu Anania aliwasili Kaisarea pamoja na wazee kadhaa na wakili mmoja wa sheria aitwaye Tertulo. Walimwendea yule mkuu wa mkoa wakamweleza mashtaka yao juu ya Paulo.

24:2 Paulo aliitwa na Tertulo akafungua mashtaka hivi: "Mheshimiwa Felisi, uongozi wako bora umeleta amani kubwa na marekebisho ya lazima yanafanywa kwa manufaa ya taifa letu.

24:3 Tunalipokea jambo hili kwa furaha daima na kutoa shukrani nyingi kwako kila mahali.

24:4 Lakini, bila kupoteza wakati wako zaidi, tunakusihi kwa wema wako, usikilize taarifa yetu fupi.

24:5 Tumegundua kwamba mtu huyu ni wa hatari mno. Yeye huanzisha ghasia kati ya Wayahudi kila mahali duniani na pia ni kiongozi wa kile chama cha Wanazareti.

24:6 Tena alijaribu kulikufuru Hekalu nasi tukamtia nguvuni. Kama ukimhoji wewe mwenyewe, utaweza kubainisha mambo haya yote tunayomshtaki kwayo." Tulitaka kumhukumu kufuatana na Sheria yetu.

24:7 Lakini Lusia, mkuu wa jeshi, aliingilia kati, akamchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwetu.

24:8 Kisha akaamuru washtaki wake waje mbele yako.

24:9 Nao Wayahudi waliunga mkono mashtaka hayo wakisema kwamba hayo yote yalikuwa kweli.

24:10 Basi, mkuu wa mkoa alimwashiria Paulo aseme. Naye Paulo akasema, "Nafurahi kujitetea mbele yako nikijua kwamba umekuwa hakimu wa taifa hili kwa miaka mingi.

24:11 Unaweza kujihakikishia kwamba si zaidi ya siku kumi na mbili tu zimepita tangu nilipokwenda kuabudu Yerusalemu.

24:12 Wayahudi hawakunikuta nikijadiliana na mtu yeyote. Hawakunikuta nikichochea watu Hekaluni wala katika masunagogi yao, wala mahali pengine popote katika mji huo.

24:13 Wala hawawezi kuthibitisha mashtaka waliyotoa juu yangu.

24:14 Ninachokubali mbele yako ni hiki: Mimi ninamwabudu Mungu na wazee wetu nikiishi kufuatana na Njia ile ambayo wao wanaiita chama cha uzushi. Ninaamini mambo yote yaliyoandikwa katika vitabu vya Sheria na manabii.

24:15 Mimi namtumainia Mungu, na wao wanalo tumaini hilo, kwamba watu, wema na wabaya, watafufuka.

24:16 Kwa hiyo ninajitahidi daima kuwa na dhamiri njema mbele ya Mungu na mbele ya watu.

24:17 "Baada ya kukaa mbali kwa miaka kadhaa, nilirudi Yerusalemu ili kuwapelekea wananchi wenzangu msaada na kutoa dhabihu.

24:18 Wakati nilipokuwa nikifanya hayo ndipo waliponikuta Hekaluni, nilipokuwa nimekwisha fanya ile ibada ya kujitakasa. Hakukuwako kundi la watu wala ghasia.

24:19 Lakini kulikuwa na Wayahudi wengine kutoka mkoa wa Asia; hao ndio wangepaswa kuwa hapa mbele yako na kutoa mashtaka yao kama wana chochote cha kusema dhidi yangu.

24:20 Au, waache hawa walio hapa waseme kosa waliloliona kwangu wakati niliposimama mbele ya Baraza lao kuu,

24:21 isipokuwa tu maneno haya niliyosema niliposimama mbele yao: Mnanihukumu leo hii kwa sababu ya kushikilia kwamba wafu watafufuliwa!"

24:22 Hapo, Felisi, ambaye mwenyewe alikuwa anaifahamu hiyo Njia vizuri, aliahirisha kesi hiyo. Akawaambia, "Nitatoa hukumu juu ya kesi hiyo wakati Luisa, mkuu wa jeshi, atakapokuja hapa."

24:23 Kisha akamwamuru yule jemadari amweke Paulo kizuizini, lakini awe na uhuru kiasi, na rafiki zake wasizuiwe kumpatia mahitaji yake.

24:24 Baada ya siku chache, Felisi alifika pamoja na mkewe Drusila ambaye alikuwa Myahudi. Aliamuru Paulo aletwe, akamsikiliza akiongea juu ya kumwamini Yesu Kristo.

24:25 Lakini wakati Paulo alipoanza kuongea juu ya uadilifu, juu ya kuwa na kiasi na juu ya siku ya hukumu inayokuja, Felisi aliogopa, akasema, "Kwa sasa unaweza kwenda; nitakuita tena nitakapopata nafasi."

24:26 Wakati huohuo alikuwa anatumaini kwamba Paulo angempa fedha. Kwa sababu hii alimwita Paulo mara kwa mara na kuzungumza naye.

24:27 Baada ya miaka miwili, Porkio Festo alichukua nafasi ya Felisi, akawa mkuu wa Mkoa. Kwa kuwa alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi, Felisi alimwacha Paulo kizuizini.

25:1 Siku tatu baada ya kufika mkoani, Festo alitoka Kaisarea, akaenda Yerusalemu.

25:2 Makuhani wakuu pamoja na viongozi wa Wayahudi walimpa habari kuhusu mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Paulo. Walimsihi Festo

25:3 awafanyie fadhili kwa kumleta Paulo Yerusalemu; walikuwa wamekula njama wamuue akiwa njiani.

25:4 Lakini Festo alijibu, "Paulo atabaki kizuizini kule Kaisarea na mimi nitakwenda huko karibuni.

25:5 Waacheni viongozi wenu waende huko pamoja nami wakatoe mashtaka yao juu yake kama amefanya chochote kiovu."

25:6 Festo alikaa nao kwa muda wa siku nane au kumi hivi, kisha akarudi Kaisarea. Kesho yake alikwenda barazani, akaamuru Paulo aletwe ndani.

25:7 Wakati Paulo alipofika, Wayahudi waliokuwa wametoka Yerusalemu walimzunguka wakaanza kutoa mashtaka mengi mazitomazito ambayo hawakuweza kuthibitisha.

25:8 Kwa kujitetea, Paulo alisema, "Mimi sikufanya kosa lolote kuhusu Sheria ya Wayahudi, wala kuhusu Hekalu, wala kumhusu Kaisari."

25:9 Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi na hivyo akamwuliza Paulo, "Je, ungependa kwenda Yerusalemu na huko ukahukumiwe mbele yangu kuhusu mashtaka haya?"

25:10 Paulo akajibu, "Nasimama mbele ya mahakama ya Kaisari na papa hapa ndipo ninapopaswa kupewa hukumu. Kama unavyojua vizuri, sikuwatendea Wayahudi ubaya wowote.

25:11 Basi, ikiwa nimepatikana na kosa linalostahili adhabu ya kifo, siombi kusamehewa adhabu hiyo. Lakini kama hakuna ukweli katika mashtaka waliyotoa watu hawa, hakuna awezaye kunikabidhi kwao. Nakata rufani kwa Kaisari!"

25:12 Basi, baada ya Festo kuzungumza na washauri wake, akamwambia Paulo, "Umekata rufani kwa Kaisari, basi, utakwenda kwa Kaisari."

25:13 Siku chache baadaye, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisarea ili kutoa heshima zao kwa Festo.

25:14 Walikuwa huko siku kadhaa naye Festo akamweleza mfalme kesi ya Paulo: "Kuna mtu mmoja hapa ambaye Felisi alimwacha kizuizini.

25:15 Nilipokwenda Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walimshtaki na kuniomba nimhukumu.

25:16 Lakini mimi niliwajibu kwamba si desturi ya Waroma kumtoa mtu aadhibiwe kabla mshtakiwa hajakutana na washtaki wake ana kwa ana na kupewa fursa ya kujitetea kuhusu hayo mashtaka.

25:17 Basi, walipofika hapa sikukawia, ila nilifanya kikao mahakamani kesho yake, nikaamuru mtu huyo aletwe.

25:18 Washtaki wake walisimama lakini hawakutoa mashtaka maovu kama nilivyokuwa ninatazamia.

25:19 Ila tu walikuwa na mabishano kadhaa pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu mmoja aitwaye Yesu ambaye alikufa, lakini Paulo anashikilia kwamba yu hai.

25:20 Sikujua la kufanya kuhusu shauri hilo. Basi, nilimwuliza Paulo kama angependa kwenda mahakamani kule Yerusalemu kwa ajili ya mashtaka hayo.

25:21 Lakini Paulo alikata rufani, akaomba aachwe kizuizini mpaka uamuzi wa shauri hilo ufanywe na Kaisari. Kwa hiyo niliamua akae kizuizini mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari."

25:22 Basi Agripa akamwambia Festo, "Ningependa kumsikia mtu huyu mimi mwenyewe." Festo akamwambia, "Utamsikia kesho."

25:23 Hivyo, kesho yake, Agripa na Bernike walifika kwa shangwe katika ukumbi wa mkutano wakiwa wameandamana na wakuu wa majeshi na viongozi wa mji. Festo aliamuru Paulo aletwe ndani,

25:24 Kisha akasema, "Mfalme Agripa na wote mlioko hapa pamoja nasi! Hapa mbele yenu yuko mtu ambaye jumuiya yote ya Wayahudi hapa na kule Yerusalemu walinilalamikia wakipiga kelele kwamba hastahili kuishi tena.

25:25 Lakini mimi sikuona kuwa alikuwa ametenda chochote kibaya hata astahili kupewa adhabu ya kifo. Lakini, kwa vile Paulo mwenyewe alikata rufani kwa Kaisari, niliamua kumpeleka.

25:26 Kwa upande wangu sina habari kamili ambayo naweza kumwandikia Kaisari juu yake. Ndiyo maana nimemleta hapa mbele yenu na mbele yako mfalme Agripa, ili baada ya kumchunguza, niweze kuwa na la kuandika.

25:27 Kwa maana nadhani itakuwa kichekesho kumpeleka mfungwa bila kutaja wazi mashtaka yanayomkabili."

26:1 Basi, Agripa akamwambia Paulo, "Unaruhusiwa kujitetea." Hapo Paulo alinyosha mkono wake akajitetea hivi:

26:2 "Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu.

26:3 Hasa kwa vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao, ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu.

26:4 "Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu.

26:5 Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali zaidi katika dini yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo.

26:6 Na sasa niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu aliwaahidia babu zetu.

26:7 Ahadi hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu, wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo!

26:8 Kwa nini ninyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu?

26:9 Kwa kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi kulipinga jina la Yesu wa Nazareti.

26:10 Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu. Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali.

26:11 Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali.

26:12 "Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu.

26:13 Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu.

26:14 Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama punda anayepiga teke fimbo ya bwana wake.

26:15 Mimi nikauliza: Ni nani wewe Bwana? Naye Bwana akajibu: Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.

26:16 Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonyesha.

26:17 Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao.

26:18 Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.

26:19 "Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hilo la mbinguni.

26:20 Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonyesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao.

26:21 Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa Hekaluni, wakajaribu kuniua.

26:22 Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia;

26:23 yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine."

26:24 Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, "Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!"

26:25 Lakini Paulo akasema, "Sina wazimu mheshimiwa Festo: Ninachosema ni ukweli mtupu.

26:26 Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila uoga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni.

26:27 Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini."

26:28 Agripa akamjibu Paulo, "Kidogo tu utanifanya Mkristo!"

26:29 Paulo akamjibu, "Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo."

26:30 Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama.

26:31 Walipokwisha ondoka, waliambiana, "Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo."

26:32 Naye Agripa akamwambia Festo, "Mtu huyu angeweza kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari."

27:1 Walipokwisha amua tusafiri mpaka Italia, walimweka Paulo pamoja na wafungwa wengine chini ya ulinzi wa Yulio aliyekuwa ofisa wa jeshi katika kikosi kiitwacho "Kikosi cha Augusto."

27:2 Tulipanda meli ya Adiramito iliyokuwa inasafiri na kupitia bandari kadhaa za mkoa wa Asia, tukaanza safari. Aristarko, mwenyeji wa Makedonia kutoka Thesalonika, alikuwa pamoja nasi.

27:3 Kesho yake tulitia nanga katika bandari ya Sidoni. Yulio alimtendea Paulo vizuri kwa kumruhusu awaone rafiki zake na kupata mahitaji yake.

27:4 Kutoka huko tuliendelea na safari, lakini kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kwa kasi kutujia kwa mbele, tulipitia upande wa kisiwa cha Kupro ambapo upepo haukuwa mwingi.

27:5 Halafu tulivuka bahari ya Kilikia na Pamfulia, tukatia nanga Mura, mji wa Lukia.

27:6 Hapo yule ofisa alikuta meli moja ya Aleksandria iliyokuwa inakwenda Italia, na hivyo akatupandisha ndani.

27:7 Kwa muda wa siku nyingi tulisafiri polepole, na kwa shida tulifika karibu na Nido. Kwa sababu upepo ulikuwa bado unatupinga, tuliendelea mbele moja kwa moja tukapitia upande wa Krete karibu na rasi Salmone ambapo upepo haukuwa mwingi.

27:8 Tulipita kando yake polepole tukafika mahali paitwapo "Bandari Nzuri", karibu na mji wa Lasea.

27:9 Muda mrefu ulikuwa umepita, na hata siku ya kufunga ilikuwa imekwisha pita. Sasa ilikuwa hatari sana kusafiri kwa meli. Basi, Paulo aliwapa onyo:

27:10 "Waheshimiwa, nahisi kwamba safari hii itakuwa ya shida na hasara nyingi si kwa shehena na meli tu, bali pia kwa maisha yetu."

27:11 Lakini yule ofisa alivutiwa zaidi na maoni ya nahodha na ya mwenye meli kuliko yale aliyosema Paulo.

27:12 Kwa kuwa bandari hiyo haikuwa mahali pazuri pa kukaa wakati wa baridi, wengi walipendelea kuendelea na safari, ikiwezekana mpaka Foinike. Foinike ni bandari ya Krete inayoelekea kusini-magharibi na kaskazini-magharibi; na huko wangeweza kukaa wakati wa baridi.

27:13 Basi, upepo mzuri wa kusi ulianza kuvuma, nao wakadhani wamefanikiwa lengo lao; hivyo wakang'oa nanga, wakaiendesha meli karibu sana na pwani ya Krete.

27:14 Lakini haukupita muda, upepo mkali uitwao "Upepo wa Kaskazi" ulianza kuvuma kutoka kisiwani.

27:15 Upepo uliipiga ile meli, na kwa kuwa hatukuweza kuukabili, tukaiacha ikokotwe na huo upepo.

27:16 Kisiwa kimoja kiitwacho Kanda kilitukinga kidogo na ule upepo; na tulipopita kusini mwake tulifaulu, ingawa kwa shida, kuusalimisha ule mtumbwi wa meli.

27:17 Wale wanamaji waliuvuta mtumbwi ndani, kisha wakaizungushia meli kamba na kuifunga kwa nguvu. Waliogopa kwamba wangeweza kukwama kwenye ufuko wa bahari, pwani ya Libya. Kwa hiyo walishusha matanga na kuiacha meli ikokotwe na upepo.

27:18 Dhoruba iliendelea kuvuma na kesho yake wakaanza kutupa nje shehena ya meli.

27:19 Siku ya tatu, wakaanza pia kutupa majini vifaa vya meli kwa mikono yao wenyewe.

27:20 Kwa muda wa siku nyingi hatukuweza kuona jua wala nyota; dhoruba iliendelea kuvuma sana, hata matumaini yote ya kuokoka yakatuishia.

27:21 Baada ya kukaa muda mrefu bila kula chakula, Paulo alisimama kati yao, akasema, "Waheshimiwa, ingalikuwa afadhali kama mngalinisikiliza na kuacha kusafiri kutoka Krete. Kama mngalifanya hivyo tungaliiepuka shida hii na hasara hizi zote.

27:22 Lakini sasa ninawaombeni muwe na moyo; hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake; meli tu ndiyo itakayopotea.

27:23 Kwa maana jana usiku malaika wa yule Mungu ambaye mimi ni wake na ambaye mimi ninamwabudu alinitokea,

27:24 akaniambia: Paulo usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri nawe wasiangamie.

27:25 Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa.

27:26 Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa fulani."

27:27 Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku na huku katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi kuwa karibu na nchi kavu.

27:28 Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arobaini. Baadaye wakapima tena wakapata mita thelathini.

27:29 Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba, waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi.

27:30 Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa mbele wa meli.

27:31 Lakini Paulo alimwambia yule ofisa wa jeshi na askari wake, "Kama wanamaji hawa hawabaki ndani ya meli, hamtaokoka."

27:32 Hapo wale askari walizikata kamba zilizokuwa zimeshikilia ule mtumbwi, wakauacha uchukuliwe na maji.

27:33 Karibu na alfajiri, Paulo aliwahimiza wote wale chakula: "Kwa siku kumi na nne sasa mmekuwa katika mashaka na bila kula; hamjala kitu chochote.

27:34 Basi, ninawasihi mle chakula kwa maana mnakihitaji ili mweze kuendelea kuishi. Maana hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea."

27:35 Baada ya kusema hivyo, Paulo alichukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega, akaanza kula.

27:36 Hapo wote wakapata moyo, nao pia wakala chakula.

27:37 Jumla tulikuwa watu mia mbili na sabini na sita katika meli.

27:38 Baada ya kila mmoja kula chakula cha kutosha, walipunguza uzito wa meli kwa kutupa nafaka baharini.

27:39 Kulipokucha, wanamaji hawakuweza kuitambua nchi ile, ila waliona ghuba moja yenye ufuko; wakaamua kutia nanga huko kama ikiwezekana.

27:40 Hivyo walikata nanga na kuziacha baharini, na wakati huohuo wakazifungua kamba zilizokuwa zimeufunga usukani, kisha wakatweka tanga moja mbele kushika upepo, wakaelekea ufukoni.

27:41 Lakini walifika mahali ambapo mikondo miwili ya bahari hukutana, na meli ikakwama. Sehemu ya mbele ilikuwa imezama mchangani bila kutikisika. Sehemu ya nyuma ya meli ilianza kuvunjika vipandevipande kwa mapigo ya nguvu ya mawimbi.

27:42 Askari walitaka kuwaua wafungwa wote kwa kuogopa kwamba wangeogelea hadi pwani na kutoroka.

27:43 Lakini kwa vile yule ofisajeshi alitaka kumwokoa Paulo, aliwazuia wasifanye hivyo. Aliamuru wale waliojua kuogelea waruke kutoka melini na kuogelea hadi pwani,

27:44 na wengine wafuate wakijishikilia kwenye mbao au kwenye vipande vya meli iliyovunjika. Ndivyo sisi sote tulivyofika salama pwani.

28:1 Tulipokwisha fika salama kwenye nchi kavu, tuligundua kwamba kile kisiwa kinaitwa Malta.

28:2 Wenyeji wa hapo walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inaanza kunyesha na kulikuwa na baridi, hivyo waliwasha moto, wakatukaribisha.

28:3 Paulo aliokota mzigo mdogo wa kuni akawa anazitia motoni. Hapo, kwa sababu ya lile joto la moto, nyoka akatoka katika kuni akamnasa Paulo mkononi na kujishikilia hapo.

28:4 Wenyeji wa pale walipokiona kile kiumbe kinaning'inia kwenye mkono wake waliambiana, "Bila shaka mtu huyu amekwisha ua mtu, na ingawa ameokoka kuangamia baharini, Haki haitamwacha aendelee kuishi!"

28:5 Lakini Paulo alikikung'utia kile kiumbe motoni na hakuumizwa hata kidogo.

28:6 Wale watu walikuwa wakitazamia kwamba angevimba au hapohapo angeanguka chini na kufa. Baada ya kungojea kwa muda mrefu bila kuona kwamba Paulo amepatwa na jambo lolote lisilo la kawaida, walibadilisha fikira zao juu yake, wakasema kuwa ni mungu.

28:7 Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya Publio, mkuu wa kile kisiwa. Publio alitukaribisha kirafiki, tukawa wageni wake kwa siku tatu.

28:8 Basi, ikawa kwamba baba yake Publio alikuwa amelala kitandani, mgonjwa, ana homa na kuhara. Paulo alikwenda kumwona na baada ya kusali, akaweka mikono yake juu ya mgonjwa, akamponya.

28:9 Kutokana na tukio hilo, wagonjwa wote katika kile kisiwa walikuja wakaponywa.

28:10 Watu walitupatia zawadi mbalimbali na wakati tulipoanza tena safari, walitia ndani ya meli masurufu tuliyohitaji.

28:11 Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli moja ya Aleksandria iitwayo "Miungu Pacha". Meli hiyo ilikuwa imetia nanga kisiwani wakati wote wa baridi.

28:12 Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku tatu.

28:13 Toka huko tuling'oa nanga, tukazunguka na kufika Regio. Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili tulifika bandari ya Potioli.

28:14 Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma.

28:15 Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akapata moyo.

28:16 Tulipofika Roma, Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake pamoja na askari mmoja wa kumlinda.

28:17 Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, "Wananchi wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma.

28:18 Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yeyote, walitaka kuniacha.

28:19 Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha kuwashtaki wananchi wenzangu.

28:20 Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi, maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli."

28:21 Wao wakamwambia, "Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako.

28:22 Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali."

28:23 Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na kuwafafanulia juu ya Ufalme wa Mungu akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya Yesu kwa kutumia Sheria ya Mose na maandiko ya manabii.

28:24 Baadhi yao walikubali maneno yake, lakini wengine hawakuamini.

28:25 Basi, kukawa na mtengano wa fikira kati yao. Walipokuwa wanakwenda zao, Paulo alisema jambo hili, "Kweli ni sawa yale aliyoyanena Roho Mtakatifu kwa wazee wenu kwa njia ya nabii Isaya

28:26 akisema: Nenda kwa watu hawa ukawaambie: kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; kutazama mtatazama, lakini hamtaona.

28:27 Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio yao, wamefumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao. Wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya."

28:28 Halafu Paulo akamaliza na kusema, "Jueni basi, kwamba ujumbe wa Mungu juu ya wokovu umepelekwa kwa watu wa mataifa. Wao watasikiliza!"

28:29 Paulo alipokwisha sema hayo, Wayahudi walijiondokea huku wakiwa wanabishana vikali wao kwa wao.

28:30 Kwa muda wa miaka miwili mizima Paulo aliishi katika nyumba aliyoipanga yeye mwenyewe; akawa anawakaribisha wote waliofika kumsalimu.

28:31 Alikuwa akihubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi.


Next: Romans