Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: 2 John

1:1 Mimi Mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule, pamoja na watoto wako ninaowapenda kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli wanawapenda ninyi,

1:2 kwa sababu ukweli unakaa nasi milele.

1:3 Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo.

1:4 Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru.

1:5 Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: tupendane. Ombi hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo.

1:6 Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu. Amri niliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: mnapaswa nyote kuishi katika upendo.

1:7 Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu akawa binadamu. Mtu asemaye hivyo ni mdanganyifu na ni Adui wa Kristo.

1:8 Basi, jihadharini ninyi wenyewe ili msije mkapoteza kile mlichokishugulikia, bali mpate tuzo lenu kamili.

1:9 Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na Mwana.

1:10 Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu.

1:11 Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika matendo yake maovu.

1:12 Ninayo mengi ya kuwaambieni lakini sipendi kufanya hivyo kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike.

1:13 Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu.


Next: 3 John